August 17, 2015

  • Maajabu Niliyoyaona Mwanza Kwenye Mkutano wa LOWASSA Hayajapata Kutokea.....Watu Walipigwa Mabomu bila Kukoma, Wengine Walizimia


    Maajabu Niliyoyaona Mwanza Kwenye Mkutano wa LOWASSA Hayajapata Kutokea.....Watu Walipigwa Mabomu bila Kukoma, Wengine Walizimia

    Haijawahi kutokea. Siyo mabomu ya machozi wala polisi wenye silaha walioweza kuzuia halaiki ya wananchi kufika kwenye viwanja vya Furahisha kuhudhuria mkutano wa mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa.

    Hii ni kwa sababu umati uliojitokeza kuanzia Uwanja wa Ndege wa Mwanza ambako polisi walilazimika kupiga mabomu yasiyohesabika kuwatawanya wananchi ambao walifunga barabara inayoingia uwanjani hapo, kutozaa matunda.

    Msafara wa Lowassa anayeungwa na mkono na vyama vinavyounda Ukawa vya Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na Cuf, ulilisimamisha Jiji la Mwanza kwa takriban saa tatu kutokana na msafara kutembea kilomita sifuri kwa saa.

    Pamoja na polisi kupiga mabomu mita chache kutoka uwanjani hapo, Lowassa alipotoka tu uwanjani, umati mkubwa wa wafuasi wake na wa Ukawa, waliokuwa wamejificha waliibuka wakiwa na chupa za maji; mbele ya askari waliokuwa kwenye magari wakiwa na silaha za moto na mabomu ya machozi.
    Kilichochangia msafara kutembea mwendo mdogo ni baadhi yao kumwaga maji barabarani kama ishara ya kupiga deki ili Lowassa apite huku wengine waliokuwa na fagio za chelewa, wakifagia.

    Wananchi wengine walikuwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali ikiwamo 'Richmond ilikuwa ni maagizo ya juu'; 'pombe mwisho kaunta, Ikulu ni Lowassa''kufuli mwisho mlangoni'; na 'Tanzania bila Lowassa haiwezekani.'

    Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo, akizungumza na waandishi wa habari uwanjani hapo, alisema polisi hawajawazuia wananchi kushiriki mkutano bali wamepiga mabomu kuzuia wale ambao wamekwenda uwanja wa ndege ambako siyo eneo la mkutano.

    "Hatuna nia ya kuzuia mkutano, wananchi tumewaambia kwamba waende Furahisha kwa sababu wakija huku watasababisha usumbufu kwa watumiaji wengine wa uwanja," alisema.

    Ikiwa uwanjani hapo, Michapo ilisikia milipuko ya mabomu zaidi ya 30 yaliyopigwa kwa takriban saa moja kabla msafara wa Lowassa haujaondoka kuelekea Furahisha.

    Tofauti na mikoa mingine, maandamano ya Mwanza hayakuwa na pikipiki, bajaj wala magari zaidi ya yale ya viongozi wa Ukawa taifa na wabunge wa Chadema kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa, bali ni wananchi wasiohesabika ambao walilazimisha mkutano kutembea kilomita sifuri kwa saa.

    Idadi ya watu waliojitokeza kwenye uwanja wa Furahisha, nusura usababishe mkutano kuahirishwa baada ya watu kuanza kuzimia na kupoteza fahamu, jambo ambalo lilisababisha kikosi cha Msalaba Mwekundu uwanjani kuzidiwa nguvu.

    Kutokana na hali hiyo,  Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliwaambia wananchi warudi nyuma na wengine wakae chini ili kutoa nafasi kwa viongozi, waandishi na wapigapicha wafanya kazi yao.

    Hata hivyo, tangazo hilo halikufua dafu kwani baadhi ya wananchi waliokuwa mbele, walikaa chini lakini halaiki hiyo iliendelea kusababisha usumbufu mkubwa kutokana na idadi ya watu walioendelea kupoteza fahamu.

    Baada ya kuanza kusukumana, wananchi wengine walianza kulia na kusema kuwa walilala uwanjani kumsubiri Lowassa na viongozi wa Ukawa, lakini wanasikitika kusukumwa na kukanyagwa.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.