Tunakujali, Tunakuthamini na Pia Tunakupenda!

August 31, 2015

  • WATUMIAJI WA MITANDAO VIBAYA SHERIA KUWADHIBITI KUANZA LEO SAA 6:00 USIKU



    WATUMIAJI WA MITANDAO VIBAYA SHERIA KUWADHIBITI KUANZA LEO SAA 6:00 USIKU
    Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dares Salaam leo.


    Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa kazini jijini Dar es Salaam leo.
     
    Na Magreth Kinabo 
    SHERIA mpya   ya Makosa ya Mtandao ya mwaka   2015 na Sheria ya Miamala ya Kielektroniki ya mwaka 2015 zitaanza kutumika rasmi kesho Septemba Mosi mwaka huu, hivyo watumiaji   na watoa huduma waaswa kuzingatia sheria hizi ili kuepuka mkondo wa sheria.
     
     Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dares Salaam kwenye ukumbi wa mikutano wa wizara hiyo.
     
    "Sheria hizi ni nzuri zitaanza kutumika Septemba Mosi mwaka huu,kuanzia saa 6.00 usiku . zina maslahi katika nchi yetu. Ninatoa wito kwa wananchi kuzingatia matumizi salama ya mtandao kwa manufaa yako na maendeleo ya Taifa letu," alisema Profesa Mbarawa.
     
     Aliongeza kuwa sheria hiyo ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 hazihitaji utungaji wa kanuni kwa kuwa iko wazi.
      Alisema tayari wizara imeanza kuelimisha watu kuhusu sheria hiyo na itendelea kuwajengea uwezo wadau mbalimbali.
    Profesa Mbarawa alisema sheria ya makosa ya mtando ya mwaka 2015 na Tanzania sio nchi ya kwanza kuwa nayo, bali nchi mbalimbali zina sheria kama hiyo ,ambapo alitolea mfano Uingereza,India,Malaysia, Uganda na Korea ya Kusini.
     
    Akizungumzia kuhusu  madai sheria hiyo kuhusika na suala la Uchaguzi Mkuu, alisema si kweli, bali imekamilika katika kipindi hicho ndio maana baadhi ya watu wanadai hivyo.Aliongeza kwamba sheria hiyo imetunga ili kudhibiti matumizi ambayo  si mazuri. 
     
    " Mtu akitumiwa ujumbe akiupokea hapaswi kuisambaza  kwani atakapousambaza atakuwa na amefanya kosa,"alisisitiza.
    Aliyataja baadhi ya makosa kuwa ni usiri, usalama wa upatikanaji wa taarifa za kompyuta na mifumo  kama vilekuingilia mawasiliano ya kompyuta au mifumo ya kompyuta kinyume cha sheria na wizi wa taarifa kimtandao.
    Makosa  dhidi ya kompyuta ikiwa ni pamoja na,udanganyifu kwa kutumia kompyuta,kugushi kwa kutumia kompyuta wizi wa utambulisho wa mtu binafsi  mtandaoni, matumizi ya vifaa kinyume cha sheria
     Makosa yanayohusiana kimaudhui kama vile usambazaji wa ponografia, ponografia za watoto makosa dhidi ya ubaguzi wa rangi na chuki, michezo ya kmari mtanadaoni kiunyume cha sheria, kashfa na habari za uongo na makosa dhidi ya haki na hati miliki.
     
    Pia inatambua muungano wa makosa inajumuisha kama vile utakatishaji wa fedha haramu na ugaidi kwa kutumia mtandao.
     
    Kwa upande wa sheria ya miamala ya kieletroniki ya mwaka 2015, baadhi ya makosa likiwemo la wajibu wa watoa huduma kwa walaji, bidhaa ,huduma au mawasiliano ambayo hayajaombwa na uhalali wa Muamala wa elektroniki.
     
    Aliongeza kuwa kanuni za sheria hiyo zinatayarishwa zikiwa tayari zitangazwa  na zitaanza kutumika wakati wowote.


  • WAPIGANAJI 10 WA BOKO HARAMU WAUAWA CHAD


    WAPIGANAJI 10 WA BOKO HARAMU WAUAWA CHAD
    Image copyrightAFP
    Image captionWashukiwa 10 wa Boko Haram waliouawa Chad
    Wanachama kumi wa kundi la Boko Haram, wameuawa kwa kupigwa risasi nchini Chad.
    Wapiganaji hao walipewa adhabu hiyo baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika na vitendo vya kigaidi, katika kesi iliyofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo N'Djamena.


    Maafisa wa ulinzi wanasema kwamba waasi hao waliuawa na kitengo maalum cha ulinzi Kaskazini mwa mji mkuu.
    Washukiwa hao kumi walihukumiwa kuhusiana na mashambulio mawili yaliyotokea katika mji mkuu mwezi Juni, mwaka huu, mashambulio yaliyosababisha vifo vya watu 38.
    Lakini mwezi mmoja baada ya shambulio hilo, serikali ya Chad ilirejesha tena adhabu ya kifo, kwa washukiwa wanaopatikana na hatia ya ugaidi.
    Miongoni mwa waliouawa ni Mohamat Mustapha, anayejulikana kwa jina lingine kama Bana Fanaye, ambaye ametajwa kama kiongozi wa mashambulio ya Juni.
    Mahamat Mustapha
    Image captionMahamat Mustapha kiongozi wa mashambulio yaliyofanyika Juni nchini Chad
    Shule moja ya umma na kituo cha polisi kililengwa na walipuaji wa kujitolea waliokuwa kwenye piki piki, na kuwaacha zaidi ya watu mia moja na majeraha, mbali na waliouawa.
    Baada ya mashambulio hayo ya Juni, soko moja maarufu katika mji mkuu ulishambuliwa na watu kumi na watano kuuawa.
    Mashumbulizi hayo yalikuwa ya kwanza kuwahi kutekelezwa na wapiganaji hao kutoka Nigeria, nchini Chad ambayo inawahifadhi wanajeshi wa muungano ambao wanaendeleza harakati za kupambana na kundi hilo.
    Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka mkuu, Bruno Mahouli Louapambe, washukiwa hao walipatikana na hatia ya mashtaka kadhaa yakiwemo, njama ya kutekeleza uhalifu, mauaji, kuharibu mali kimakusudi wakitumia vilipuzi, ulaghai, kumiliki silaha na risasi bila idhini na kutumia bidhaa ambazo zinaweza kusababisha maangamizi.
    Chad imekuwa katika mstari wa mbele kuisaidi Nigeria, kuyakomboa maeneo yaliyotekwa na wapiganaji hao wa Boko Haram.
    Wanamgambo hao wa Kiislamu, ambao wanataka kuunda Jamuhuri yao ya Kiislamu nchini Nigeria, wamewauawa maelfu ya raia na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kukimbia makwao Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo tangu 2009.
    Image copyrightBBC World Service
    Image captionRamani ya Nigeria
    Kundi hilo lilikuwa limetishia kushambulia Chad, baada ya serikali ya nchi hiyo kutuma wanajeshi wake nchini Nigeria, kupambana na kundi hilo na kukomboa maeneo waliyoyateka hasa katika jimbo la Borno.
    Kufuatia mashambulio hayo ya ,Chad ilipiga Marufu watu wote nchini humo kuvalia vitambaaa vinavyofunika nyuso zao, maarufu kama Burka.
    Lakini juhudi ya kudhibiti kundi hilo na ugaidi zimeshutumiwa na upinzani na makundi ya kutetea haki za kibinadam ambao wana wasi wasi kuwa huenda serikali ikahujumu haki za raia, kwa misingi ya kupambana na ugaidi.
    Image copyrightBoko Haram Video
    Image captionwapiganaji wa Boko Haram

    Wasifu wa Boko Haram

    • Boko Haram lilianzishwa mwaka wa 2002, dhamira kuu ikiwa kupinga mfumo wa elimu kutoka mataifa ya Magharibi. Boko Haram linamaanisha Elimu kutoka mataifa ya Magharibi imepigwa marufuku, kwa lugha ya Kihausa.
    • Kundi hilo lilianzisha operesheni za kijeshi 2009.
    • Maelfu ya watu wameuawa, wengi wao kutoka eneo la Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, wamewateka nyara mamia ya wengine wakiwemo wasichana 200 wa shule ya wasichana ya Chibok.
    • Iliijiunga na kundi la Islamic State na sasa limegeuza jina lake na kuwa Islamic State iliyo Magharibi wa Afrika au"West African province".
    • Boko Haram limeteka eneo kubwa Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, ambako limetangaza kuwa ni taifa huru la Kiislamu.
    • Wanajeshi wa Muungano hata hivyo wamefanikiwa kuyakomboa baadhi ya maeneo hayo.
    • BBC.


  • Samwel Sitta Ataka Akutanishwe na Lowassa Katika Mdahalo Ili Aanike Ukweli wa Richmond


    Samwel Sitta Ataka Akutanishwe na Lowassa Katika Mdahalo Ili Aanike Ukweli wa Richmond


    MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na Mbunge wa Urambo aliyemaliza muda wake, Samuel Sitta ametaka uandaliwe mdahalo kwenye vyombo vya habari kati yake na mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa uelezwe ukweli juu ya ukweli wa sakata la Richmond.


    Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge wakati Lowassa alipojiuzulu kutokana na sakata hilo, alisema katika mdahalo huo, ataeleza ukweli juu ya uhusika wa Lowassa katika sakata hilo na atatoa vielelezo kueleza taifa ufisadi uliokuwa ukifanyika.


    Alisema hayo jana kwenye ufunguzi wa kampeni za CCM mkoa wa Shinyanga katika mkutano uliofanyika mjini hapa ambao wagombea wa udiwani na ubunge wa majimbo yote ya mkoani hapa walitambulishwa.


    Katika mkutano huo, alisema kujiuzulu kwa Lowassa mwaka 2008, kulitokana na Kamati Teule iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe, kugundua kwamba fedha za walipa kodi zilikuwa zikipotea bure.


    Alisema yuko tayari kusimulia kwa umma utajiri wa mgombea huyo wa Chadema. 
      
    Makundi, urafiki
    Sitta ambaye ni Waziri wa Afrika Mashariki, ambaye pia alikuwa kwenye kinyang'anyiro cha kutaka kuteuliwa kugombea urais kupitia CCM, alisema wanamwamini Dk John Magufuli katika utendaji wake wa kazi na pia ni kiongozi asiye na makundi au urafiki.


    "Kweli lazima uwapime viongozi, kwani anayetaka urais lazima achaguliwe kwa kufuata utaratibu, achambuliwe usiogope moshi kama unapikia kuni…lakini mwenzetu Lowassa hakukubaliana na hayo, akaona kaonewa kwa madai anafaa kuwa rais mbona sisi tulikubali?," alihoji Sitta.


    Aliendelea kusema, "hali hiyo, ilionesha ndani ya CCM kulikuwa na vyama viwili ambavyo ni 'CCM Katiba' na 'CCM Maslahi' ambayo alikuwa anaongoza Lowassa na mfuasi wake, Mgeja (aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga ambaye pia alihamia Chadema hivi karibuni)."


    Wanachama mapandikizi 
    Sitta alisema CCM ilikuwa imejaa wanachama walio mapandikizi tofauti na sasa ambapo alidai wamekwisha jionesha na kimekuwa chama kizuri kama ilivyokuwa enzi za hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.


    Alisisitiza kwamba kitazidi kuimarika na waliobaki wataendelea kutetea ilani na kuhakikisha chama kinaendelea kushika dola. 
      
    Kwa mujibu wa Sitta, wakati wa mchakato, baada ya kumaliza vikao, Lowassa alikuwa akiitisha vikao vya kundi lake alilolibatiza CCM Maslahi na kuwaagiza wapambe wake kuitisha vyombo vya habari kushambulia watu ambao hawako kwenye mlengo wao.


    Wakati huo huo mjumbe huyo wa NEC, alikumbusha umati uliohudhuria mkutano huo kwamba, uchaguzi wa mwaka huu unatumia Katiba ya zamani ya mwaka 1977 ambayo inatamka matokeo ya rais hayahojiwi hata kama aliyeshinda, amezidi kura moja.


    Sitta ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, alisema alishauri wabunge wasitoke nje ya Bunge hilo waweze kutumia katiba hiyo iliyokuwa na kipengele cha kuhoji matokeo ya rais sasa imekula kwao.




  • August 30, 2015

  • HOTUBA YA MGOMBEA URAIS KUPITIA CHAMA CHA CHADEMA NA UKAWA MH. EDWARD NGOYAI LOWASSA ,,YA KUZINDUA ILANI NA KAMPENI YA UCHAGUZI MKUU



    HOTUBA YA MGOMBEA URAIS KUPITIA CHAMA CHA CHADEMA NA UKAWA MH. EDWARD NGOYAI LOWASSA 

    YA KUZINDUA ILANI NA KAMPENI YA UCHAGUZI MKUU

    Jangwani-Dar-es-Salaam, 29 AGOSTI 2015

    Ndugu Wana Dar es salaam na Watanzania wenzangu

    1. Leo ni siku ya kihistoria. Baada ya miaka ishirini na tano tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe, vyama vya upinzani wa CHADEMA, CUF, NCCR na NLD umeungana chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi kupigania uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kuwa na mgombea mmoja katika ngazi zote.

    2. Miaka zaidi ya hamsini ya utawala wa serikali za CCM na waasisi wake, umekuwa utawala wa wachache walio hodhi madaraka na mali za nchi. 

    3. Leo tunaanza safari ya uhakika ya kuleta mabadiliko ya kweli nchini. 

    a. Mabadiliko yaletayo neema na kujenga upya mfumo wa uchumi, haki na sheria nchini. 

    b. Mabadiliko ya kuimarisha huduma za jamii kama elimu, afya, maji na makazi. 

    c. Mabadiliko ya kuondoa umaskini. 

    d. Mabadiliko tunayatoahidi ni mabadiliko ya kurejesha matumaini kwa Watanzania kwa kubadili hali zao za maisha. 

    4. Kila mwaka hali na ubora wa maisha ya Watanzania imeshuka wakati tunaambiwa kuwa pato laTaifa linakuwa. 

    5. Lakini Watanzania wanachotaka siyo takwimu bali kuona kipato chao kinakua, shule, hospitali na barabara bora zinajengwa. 

    6. Wanataka kupata maji safi na salama ya kunywa. Wanataka makazi bora. 

    7. CHADEMA na UKAWA, tuna dhamira ya kuleta mabadiliko ya kweli ili kuona azma ya Watanzania tangu uhuru ya kuondoa umaskini, maradhi,na ujinga inahitimishwa.

    8. Ili tufanye hivyo tuahitaji tufanye mabadiliko ya fikra, uongozi, sera na utendaji. 

    9. Leo Tanzania inakabiliwa na changamoto nyingi za ki-uchumi, kisiasa na kijamii. Changamoto hizi ni matokeo ya sera za utawala wa Chama kimoja wa miaka hamsini. Sote ni wahanga wa siasa na sera hizi. 

    10. Miaka Hamsini ya CCM imetosha. Tunataka mabadiliko na siyo ahadi zile zile kila mwaka.

    11. Tusidanganyike, CCM hawana jipya.

    12. Chagueni UKAWA wenye dira ya kubadili maisha ya wananchi. 

    13. Mimi ninauchukia umaskini na mimesimamia maendeleo kwa vitendo. Nilipokuwa Waziri Mkuu nilijaribu kubadili hali hii. Nilisimamia ujenzi wa shule za kata, Chuo Kikuu cha Dodoma. Nilihakikisha mikataba mibovu ya maji inavunjwa na sasa wananchi wa kanda ya ziwa wanapata maji safi.

    Ndugu watanzania
    14. CCM wanauliza tuna mpango gani wa kumaliza umaskini. Sisi hatuahidi tu. Tutatenda.

    15. Ilani yetu ni dira ya kuondoa umaskini kwa mikakati sahihi na siyo nadharia.

    16. Mkakati wa kuondoa umaskini si wa sekta kwa sekta bali wa sekta zote kwa pamoja. Ni ujumla wa utendaji na utekelezaji wa sera za kila sekta utakao leta maendeleo.

    17. Mkakati wangu na UKAWA wa kuondoa umaskini utakuwa na nguzo tano:-
    a. Kupunguza matumizi ya serikali na mashirika yake na kuimarisha utendaji na uwajibikaji.
    b. Kukuza pato la serikali kwa kudhibiti ukwepaji na misamaha ya kodi holela na kuhakikisha nchi inawekeza katika sekta muhimu na inapata gawio halisia kutoka wawekezaji
    c. Kukuza uchumi kwa sera na sheria endelevu ikiwa ni pamoja na kukuza biashara na uwekezaji hasa katika sekta za madini, kilimo, viwanda, ufugaji na uvuvi na kuondoa kodi kwa wanyonge.
    d. Kuimarisha huduma za umma kama elimu, afya, maji na makazi, na mazingira
    e. Kuimarisha utawala bora na mfumo wa haki na sheria chini ya Katiba ya Wananchi. 

    18. Chini ya misingi hii na ili kufanikisha mkakati wa kuondoa umaskini, serikali yangu itafanya yafuatayo:-

    ELIMU BORA KWA KILA MTANZANIA
    Nimelisema hili huko nyuma. Nalisema tena leo. Elimu kwanza, Elimu kwanza, Elimu kwanza.

    Kwa hiyo mkakati wetu wa msingi utakuwa kutoa Elimu itatayogharamiwa na serikali kwa kila Mtanzania kutoka elimu ya msingi hadi Chuo Kikuu na pia:-

    1. Kuimarisha elimu ya teknolojia, ustadi na ufundi inayojenga uwezo wa kujiajiri na ushindani katika soko la ajira.
    2. Ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya elimu ikiwa ni pamoja na shule za Kata. 
    3. Kusimamia ubora wa viwango vya elimu kote nchini. 
    4. Kuimarisha taaluma na mitaala katika mashule. 
    5. Kuondoa utoro darasani, na kuboresha afya za wanafunzi.
    6. Kuboresha maslahi na vitendea kazi kwa walimu ikiwa ni pamoja na nyumba, posho ya kufundishia, usafiri na zana za teknolojia. 
    7. Kufuta michango ya maabara ya shule za kata

    AFYA 
    1. Afya na tiba ya kila Mtanzania itagharamiwa kupitia bima za gharama nafuu na mifuko ya hifadhi ya jamii
    2. Tutaimarisha afya ya msingi pamoja na kinga kupunguza gharama za tiba.
    3. Serikali itahakikisha kuna uwiano na upatikanaji wa watumishi wa afya katika kada mbalimbali ili kuleta tija na huduma stahiki.
    4. Itaimarisha miundombinu ya afya pamoja na kujenga hospitali za kisasa ili kusogeza huduma za afya karibu na jamii na pia kuepukana na tiba za nje ya nchi.
    5. Tutarejea kwa lengo la kuboresha maslahi na vitendea kazi katika sekta ya Afya ikiwa ni pamoja na nyumba na usafiri.
    6. Tutathibiti ongezeko la gharama za huduma za afya bila kuathiri uendeshaji wa watoaji huduma za afya kama vile serikali na hospitali za sekta binafsi.

    ARDHI, MAJI NA KILIMO

    1. Tutaimarisha mfumo wa umiliki wa ardhi kwa Watanzania na kudhibiti migogoro ya ardhi hasa kati ya wakulima na wafugaji.
    2. Tutapima ardhi yote ya Tanzania na kumilikisha vijiji na wakulima kwa hati za serikali ili kuipa thamani. 
    3. Tutaleta mapinduzi ya kilimo kwa kuimarisha elimu, ufundi na teknolojia ya kisasa na kumkomboa mkulima kutoka jembe la mkono. 
    4. Tutasimamia kilimo, ufugaji na uvuvi wa kisasa na kuunganisha sekta hizo na ya viwanda. 
    5. Kuhakikisha kuwa wananchi wanatunza na kulinda vyanzo vya maji.
    6. Tutakuza kilimo cha umwagiliaji kwa kuwapa wakulima elimu na mikopo ya riba nafuu ya kuvuna maji na kujenga miundombinu husika.
    7. Tutaweka mazingira rafiki yatakayomhakikishia kwa kila Mtanzania kupata maji safi na salama. Kumaliza kero za maji nchini kutamkomboa mwanamke kutokana na adha ya kuchota maji kwa kichwa
    8. Nitafuta kodi zote za mazao na mifugo kwa wakulima na wafugaji. 
    9. Tutasimamia kilimo cha biashara kinachozingatia maslahi ya nchi na ya Watanzania. 
    10. Tutaanzisha programu maalum ya kufufua mazao asilia ya Tanzania hususan mkonge. 
    11. Tutaanzisha Benki ya Maendelo ya Ufugaji na Uvuvi. 

    MIUNDOMBINU
    1. Tutaboresha bandari zilizopo na kujenga mpya kama vitega uchumi vya Taifa ili kurejesha biashara tulizopoteza kwa bandari za nchi jirani. 
    2. Tutajenga barabara nchini kwa kuzingatia ubora hasa zile za vijijini. 
    3. Tutajenga reli ya kati kwa viwango vya kisasa
    4. Tutajenga shirika la Ndege la Taifa linalojiendesha kwa misingi ya faida. 
    5. Tutajenga miundombinu ya kisasa na kuondosha misongamano ya magari hasa katika majiji ya Dar es salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha 
    6. Tutaimarisha uzalishaji na usambazaji wa umeme vijijini ili kufikia zaidi ya asili mia sabini na tano ya Watanzania 

    VIWANDA 

    1. Tutaimarisha sekta ya viwanda kuwa mhimili wa uchumi kwa uzalishaji wa bidhaa na ajira endelevu 
    2. Tutajenga viwanda vipya vya kusindika mazao ya kilimo, uvuvi na ufugaji.
    3. Tutahakikisha kuwa ndani ya miaka mitano mali ghafi zote za Tanzania zinasindikwa kabla ya kusafirishwa nje ili kuongeza mapato na ajira ya mamilioni ya vijana. 
    4. Tutaanzisha Benki ya Ukuzaji wa Viwanda 

    UCHUMI
    1. Tutabadili mfumo wa Uchumi wa nchi ili kuhakikisha kuwa mfumo wa uchumi wa Tanzania unakuwa ni wa soko-kijamii ambapo nguvu za soko zitatumikia jamii kwa serikali kuweka uwiano wa mapato unaohakikisha huduma za kijamii zinapatikana kwa ufanisi.
    2. Tutalinda sekta binafsi na bidhaa za ndani kwa kuwapa Watanzania upendeleo wa maksudi kwa kipindi cha mpito ili waimarike na waweze kuhimili ushindani. Tutawapa wafanyabiashara wetu upendeleo katika manunuzi ya serikali na kuwajengea mazingira mazuri ya biashara na kodi endelevu. 
    3. Tutawawezesha Watanzania kupata mitaji ya biashara kwa masharti nafuu kabisa.
    4. Tutavutia uwekezaji na wawekezaji wenye tija. Kuweka udhibiti wa wahamiaji wasioleta tija wala maslahi kwa Taifa. 
    5. Tutaimarisha sera ya ubia baina ya Serikali na Sekta binafsi kwenye maeneo muhimu ya kiuchumi na kibiashara. Pia, kuwawezesha Watanzania kuwekeza kwa njia ya ubia na wawekezaji wenye mitaji mikubwa bila kujali wanapotoka.
    6. Tutaimarisha usimamizi kwa kubadilisha mfumo wa Vyama vya Ushirika nchini ili utokane na uendeshwe na wakulima wenyewe ikiwa na pamoja na kuwawezesha kuboresha makazi kwa mpango wa kushirikiana kujenga nyumba bora
    7. Tutaanzisha na kuwezesha uanzishaji wa viwanda vidogovidogo vinavyotoa ajira kwa wingi kwa kuvihusisha na vyuo vya ufundi na benki maalum kwa lengo hilo.

    AJIRA
    1. Tutasimamia swala la ajira hasa kwa vijana kwa kukuza elimu ya ufundi ili waweze kujiajiri
    2. Tutazipa kipaumbele sekta zinazozalisha ajira kwa wingi hasa za viwanda, kilimo, ufugaji, uvuvi na utalii na kuzipa unafuu wa kodi ili zikue kwa haraka.
    3. Tutawapa wawekezaji wakubwa katika sekta hizi upendeleo maalum na viwango vya kodi nafuu.

    NISHATI NA MADINI 
    1. Serikali itashiriki kikamilifu katika uzalishaji wa nishati
    2. Itatengeneza mazingara mazuri ya kisera yatakayovutia na kuwezesha ushiriki wa Watanzania na ubia kati yao na wageni.
    3. Serikali yangu itaupa uzalishaji mkubwa wa umeme wa maji kipaumbele namba moja, umeme wa makaa ya mawe kipaumbele namba mbili, umeme wa gesi asilia kipaumbele namba tatu na umeme wa urana kipaumbele namba nne. 
    4. Serikali itatoa vipaumbele muhimu kwenye usambazaji wa huduma kubwa ya umeme sehemu za uzalishaji uliyolenga masoko ya ndani, ya nchi jirani na ya nchi za kigeni.
    5. Itapitia upya mikataba yote mikubwa ya nishati na madini ili kubaini iliyo mibovu na kuifanyia maboresho.
    6. Serikali yangu itatumia sehemu ya hisa zake kwenye raslimali kubwa ya gesi asilia iliyopatikana hapa nchini kama rehani kwenye kujichukulia mikopo kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya mabomba ya gesi. 
    7. Serikali itatoza kodi na ada ndogo zaidi kwa wazawa wenye ubia kati yao na wageni kuliko zitakazotozwa kwa wageni wasiowekeza kwa kushirikisha wazawa.

    8. Serikali itasitisha utoaji wa misamaha ya kodi isiyo lazima kwenye sekta ya madini, na badala yake itawekeza kwenye kuongeza thamani ya raslimali zake za madini.
    9. Tutakuza nishati mbadala kutamkomboa mwanamke kutokana na adha ya kukata kuni 

    MALIASILI NA UTALII
    1. Tutasimamia uvunaji na matumizi ya rasilimali za Taifa kwa manufaa ya kila Mtanzania wa kizazi hiki na kijacho
    2. Tutapiga vita ujangiri na kuimarisha utunzanji wa hifadhi za taifa na mazingira 
    3. Tutachochea ujenzi wa miundombinu ya utalii nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mahoteli na kuimarisha mafunzo 
    4. Tutaongeza idadi ya watalii kufikia milion mbili ifikapo 2020. 

    UTAWALA BORA, ULINZI WA NCHI NA USALAMA WA RAIA
    1. Tutasimamia Katiba mpya inayolinda haki za msingi za wananchi na kuweka bayana mipaka ya madaraka ya serikali na viongozi, Bunge na Mahakama.
    2. Tutaboresha miundobinu ya sheria na kuimarisha utendaji wa Mahakama na maslahi ya wafanyakazi
    3. Tutasimamia haki za raia na kuangalia upya sheria kandamizi ili wananchi kama Masheik wa Zanzibar hawasoti jela kwa sababu za kisiasa.
    4. Tutaimarisha mafunzo ya vyombo ya Polisi hasa wapelelezi na waongoza mashtaka ili wapate uwezo wa kusimamia utoaji wa haki.
    5. Tutavipa vyombo vyote vya ulinzi na usalama nyenzo na kuboresha mazingira yao ya kazi na maslahi 


    UZALENDO, UTENDAJI NA UWAJIBIKAJI
    1. Tutajenga uzalendo ili kila Mtanzania aweze kutathmini mchango wake kwa taifa kila siku 
    2. Tutaimarisha nidhamu, utendaji na uwajibikaji katika Sekta ya Umma 
    3. Tutaimarisha mchango wa Wataalam wetu, wanawake na vijana katika kusimamia uchumi na kuwajengea mazingira stahiki ya kazi pamoja na mafao.
    4. Tutapiga vita rushwa na ubadhirifu katika sekta ya Umma na binafsi 
    5. Tutadhibiti na kupunguza matumizi ya serikali ikiwa ni pamoja na kufuta safari za watumishi serikalini zisizokuwa muhimu pamoja na zile za Rais na kupiga marufuku matumizi ya mashangingi serikalini. 
    6. Tutadhibiti deni la Taifa kwa kuanza na ukaguzi wa madeni ya serikali ili kuhakiki jinsi yalivyotumika
    7. Tutaimarisha uwazi na kuondoa usiri katika shughuli za serikali na kuweka bayana mikataba yote ya nchi ikiwa ni pamoja na ile ya mafuta, madini na gesi asilia


    KUKUZA PATO LA SERIKALI

    1. Tutadhibiti mapato kutokana na raslimali kwa kupitia upya viwango vya mirabaha kutokana na madini na gesi asilia ili kuhakikisha kuwa Tanzania inapata gawio stahiki. 
    2. Serikali itaanzisha Wizara maalum itakayosimamia nishati ya gesi na mafuta.
    3. Tutaimarisha ofisi ya Msajili wa Hazina ili kusimamia vema uwekezaji wa Serikali katika mashirika na mapato yake. 
    4. Tutahakikisha kuwa mashirika ya umma yanaendeshwa kwa misingi ya faida na uadilifu.
    5. Tutadhibiti ukwepaji kodi za ushuru wa forodha na kupiga marufuku misamaha ya kodi holela ili kuokoa mabilioni ya fedha yanayopotea kila wiki. 
    6. Sambamba na hilo tutarahisisha utaratibu wa kulipa kodi ili kuondoa kero na mazingira ya rushwa. Kwa kudhibiti makusanyo ya kodi tutakusanya fedha za kugharimia huduma za msingi kama afya na elimu kikamilifu.


    KUIMARISHA MUUNGANO 

    1. Tutaimarisha umoja, usalama na udugu wa Watanzania na Muungano kwa misingi ya haki na usawa

    WANAWAKE, WATOTO NA WAZEE

    1. Wanawake watapewa fursa na haki sawa katika elimu na uchumi ili waweze bila kuwezeshwa.
    2. Tutahakikisha wazazi wanapata fursa ya kuwa walezi na wafanyakazi kwa kuongeza urefu wa likizo ya uzazi
    3. Tutaimarisha elimu ya watoto hasa wasichana na kukuza fursa zao na kukomesha ndoa za watoto wadogo.
    4. Tutaongeza uwakilishi wa akina mama katika ngazi zote serikalini na mashirika yake kufikia asili mia hamsini ifikapo 2020.
    5. Wazee na wasiojiweza watapewa posho ya kujikimu inayokidhi mahitaji ya msingi itakayowawezesha kuishi kwa heshima na kulinda utu wao ndani ya familia na jamii zao.

    SANAA, UTAMADUNI NA MICHEZO


    1. Tutaendeleza na kuwezesha vipaji vya sanaa na michezo 
    2. Tutarudisha viwanja vya michezo vilivyovamiwa 
    3. Tutafuta kodi zote za vifaa vya michezo.
    4. Tutadhibiti viwango na maadili ya bidhaa za nje zinazoingizwa nchini na kuzitoza kodi halisia
    5. Tutajenga taasisi na vyuo vya kukuza michezo ili kuhakikisha kuwa ndani ya miaka mitano Tanzania inashiriki kwa ushindi katika mashindano ya kimataifa ya soka na riadha 
    6. Tutalinda Hakimiliki za sanaa nchini
    7. Tutafuta kodi za sanaa kwa wasanii chipukizi ili kuwapa muda kwa kujijenga.

    SERA YA MAMBO YA NJE YENYE TIJA KWA TAIFA


    1. 
    Tutakuza ushirikiano wa Kimataifa wenye tija na Ujirani mwema. 

    2. 
    Tutatetea haki za binadamu, usawa wa nchi na kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika diplomasia ya kimataifa. 

    3. 
    Tutakuza umoja na ushirikiano wa Umoja wa Afrika, Jumuia ya Afrika Mashariki, SADC na Umoja wa Mataifa.

    4. 
    Tutaimarisha Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na kudai mabadiliko ya mfumo ili kuleta usawa wa nchi shiriki.

    Ndugu Watanzania


    Naomba nimalizie kwa kusema yafuatayo


    1. 
    Natambua kuwa uongozi ni dhamana. Mkinichagua nitaienzi dhamana hiyo kwa utendaji uliotukuka. 

    2. 
    Nawaahidi Watanzania kuwa kwa uwezo, akili, uzoefu na nguvu zangu zote nitawatumikia. Nawaomba nanyi mniahidi jasho lenu na uwezo wenu wote ili kwa pamoja tuvuke. Tutajikomboa toka utawala wa CCM unaodumaza uchumi na maendeleo. Tutaanza safari ya uhakika kuondoa umaskini.

    3. 
    Mabadiliko pia ni kuthamini utu na kukataa hadaa ya hongo ili kuuza haki yako ya kuchagua. Msikubali rubuni za uchaguzi kwa kupewa pesa au vitu. Rushwa ya uchaguzi ndiyo sera ya CCM. Ukikubali basi umeuza pia haki na sauti yako ya kuwalalamikia walio madarakani. Imetosha. Tukatae. Tulinde utu na haki zetu. Tuchague mabadiliko.

    4. 
    Mabadiliko ni fikra. Ni kufikiri na kutenda tofauti. Hatuwezi kuendelea kufikiri na kutenda kama kwamba hatuna dharura ya maendeleo. Kwanza tuanze kwa kufanya mabadiliko na tujiamini kuwa sisi kama Taifa tunaweza. Tunaweza kujitegemea na kuleta maendeleo yetu wenyewe bila kutegemea wafadhili. Hii si ndoto. Nchi nyingi zimefanikiwa kuondoa umaskini katika kizazi kimoja. Tujifunze kutoka kwao.

    5. 
    Tuwe taifa linalotumia raslimali zake kujiendeleza na siyo kuwanufaisha wageni na kuwafanya Watanzania watwana katika nchi yao. Inabidi tuache kuwa taifa ombaomba. Tuache kuukubali na kuvaa umaskini kama joho la fahari. 

    6. Mabadiliko ya kweli hayawezi kuletwa na CCM. Tusitegemee kuwa leo wana jipya. Ndiyo maana ahadi walizotoa miaka thelathini iliyopita ndizo wametoa juzi. Tukatae hadaa. Miaka hamsini ya CCM imetosha. 

    7. Tunaamani kwamba tutashinda kwa sababu Watanzania mpo nyuma yetu. Watanzania mmeamua kuleta mabadiliko. Kura yako ndiyo itakayokuwa mkombozi wako. Hakikisha unapiga na kuilinda kura yako. Wakati wa mabadiliko ni sasa.

    Mungu ibariki Tanzania. Asanteni sana
  • Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.