Mahakama ya hakimu                    mkazi Kinondoni jijini Dar es salaam imesitisha kwa                    muda shughuli zake baada ya zomeazomea iliyosababishwa                    na umati mkubwa wa watu waliofika mahakamani hapo                    kushuhudia kesi inayomkabili Amina Maige                    aliyeshitakiwa kwa kosa la kumjeruhi binti kwa                    kumng'ata na kumuunguza kwa pasi.Ndivyo                hali ilivyokuwa katika mahakama hiyo mara baada ya                mtuhumiwa huyo kufikishwa mahakamani hapo akiwa chini ya                ulinzi mkali wa polisi ambapo kabla ya kuteremka kutoka                ndani ya gari alifunika uso wake na mtandio hali                iliyosababisha umati huo kuanza kupiga kelele wakitaka                afunuliwe ili aonekane.
          Hata mara baada ya                kuhifadhiwa katika chumba cha maabusu ya mahakama hiyo                wakati akisubiri kupandishwa kizimbani baadhi ya                wanaharakati waliofika mahakamani hapo nao walisikika                wakilaani kitendo cha polisi kumsaidia kufunika uso.
            Zoezi la kuwatuliza                    wananchi hao lilionekana kuwashinda askari wa jeshi la                    polisi hali iliyowalazimu askari magereza kuingilia                    kati na kusaidiana nao ili shughuli za mahakama ziweze                    kuendelea kama askari Mmoja alivyosikika akiwaomba                    waondoke katika eneo hilo.
          Akisoma shitaka                    linalomkabili mtuhumiwa huyo wakili wa serikali                    Mohamed Salum mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya                    Kinondoni Yohana Yongolo amesema mtuhumiwa Amina Maige                    anakabiliwa na kosa la kumjeruhi vibaya Binti Eusta                    Hashim kinyume na kifungu kidogo cha sheria 225, kosa                    alililolitenda huko eneo la Mwananyamala Manjunju.
          Wakili Mohamed amesema upelelezi                    umekamilika ambapo mshitakiwa amekana shitaka hilo na                    kurudishwa rumande baada ya mwendesha mashitaka huyo                    kumuomba hakimu asimpatie dhamana kwa ajili ya usalama                    wake, ombi ambalo hakimu alikubaliana nalo ambapo                    mtuhumiwa amerudishwa rumande hadi June 26 mwaka huu                    kesi hiyo itakapotajwa kwa ajili ya masikilizo ya                    awali.
        
 
 
 
 
 
0 comments:
Post a Comment