June 28, 2014

  • Wanachama 34 CUF wawakataa Seif, Lipumba


    Wanachama 34 CUF wawakataa Seif, Lipumba
    Wanachama 34 wa Chama cha Wananchi (CUF), wamepiga kura za kuwakataa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad.

    Hata hivyo, pamoja na idadi hiyo ndogo kuwakataa, Profesa Lipumba na Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, walipata ushindi wa kishindo. Katika uchaguzi huo, Maalim Seif ambaye alikuwa mgombea pekee kwa nafasi ya katibu mkuu, alichaguliwa kwa kura 675 kati ya 678 sawa na asilimia 99.5 na Profesa Lipumba alichaguliwa kuwa mwenyekiti baada ya kupata kura  659 kati ya 690 zilizopigwa sawa na asilimia 95.7.

    Wanachama wa CUF ambao walipiga kura kuanzia saa tisa alasiri, walibaki ukumbini hadi saa tatu usiku kusubiri matokeo hayo ambayo baada ya kutangazwa yaliamsha hoihoi, nderemo na vifijo.

    Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi huo, Awadhi Said alisema Profesa Lipumba alimshinda Lutayosa Yemba aliyepata kura 30 sawa na asilimia 4.3. Mgombea mwingine, M'bezi Adam Bakari alijitoa muda mfupi kabla ya wajumbe hao kuanza kupiga kura akisema: "Nilikuwa naonja demokrasia ndani ya chama chetu lakini nimeona mzigo mzito ni bora nimpe Mnyamwezi." Licha ya kufafanua ilionekana alikuwa akimlenga Profesa Lipumba ambaye ni wa kabila hilo. Hii ni mara ya nne kwa Profesa Lipumba kushinda nafasi hiyo.

    Msimamizi huyo pia alimtangaza Waziri wa Afya wa Zanzibar, Dk Juma Duni Haji kuwa makamu mwenyekiti wa chama hicho baada ya kupata kura 662 kati ya kura 667 zilizopigwa sawa na asilimia  99.25.

    Ahadi

    Akitoa shukrani, Maalim Seif alishukuru kwa kuchaguliwa na akawaahidi Watanzania katiba yenye maoni ya wananchi... "Mmenipa heshima kubwa lakini ili kulipa fadhila nitahakikisha napigania kupata Katiba Mpya yenye maoni ya wananchi. Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ndiyo tumaini letu tutapambana hadi tupate katiba yenye maoni ya wananchi."

    Alisema CUF hakitakubali kuburuzwa katika mchakato wa Katiba na kitakuwa mtetezi wa masilahi ya wananchi wote.

    Profesa Lipumba aliwashukuru wajumbe wa mkutano huo kwa kumchagua na kusema kupitia Ukawa, Watanzania watapata katiba iliyo bora.

    "Tutapambana hadi kieleweke kwa kuwa Ukawa ndiyo tumaini letu. Watanzania wafahamu kwamba tuko pamoja tutawapigania ili wapate katiba wanayoitaka," alisema.

    Mgombea wa uenyekiti aliyeshindwa, Yemba alisema uchaguzi huo ulikuwa huru na haki na akawapongeza waliochaguliwa... "Nimeshindwa uchaguzi huu lakini nitaendelea kuwa mwanachama mwaminifu katika chama chetu."



  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.