June 26, 2014

  • Wizara ya Fedha yafanikiwa kusimamia miradi ya maendeleo nchini

     

    Jakaya-Kikwete1

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

    Na Mwandishi wetu – Hazina

    Dhana ya kukua katika maisha ya jamii inahusisha mtu, Wizara, Idara naTaasisi mbalimbali zinazounda jumuiya ya watu au taifa fulani.

    Ni ukweli usiopingika kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekua na kufikisha umri wa nusu karne ambapo Aprili 26 mwaka huu wa 2014 inajivunia kufikisha miaka 50 tangu kuasisiwa kwake (1964- 2014).

    Sherehe za Maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ziliongozwa na kupambwa na kauli mbiu inayosema "Utanzania wetu ni Muungano wetu, tuulinde, tuuimarishe na kuudumisha".

    Tunapoadhimisha sherehe ya dhahabu ya muungano huu, Wizara ya Fedha inajivunia mafanikio makubwa ikiwa nimoja kati ya Wizara muhimu katika muungano huo.

    Serikali ya Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Jemedari wake Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ndio msimamizi mkuu wa Wizara, Idara na taasisi zinazoshughulikia muungano huu adhimu Afrika na dunia nzima.

    Dhana ya kukua Wizara ya Fedha imejitokeza tangu kuundwa kwa Muungano mwaka 1964, ambapo Wizara hiyo imekuwa na majina tofauti kulingana na majukumu inayopewa kwa wakati husika.

    Majina hayo ni Wizara ya Fedha (1962 – 1966), Wizara ya Fedha na Mipango (1977), Wizara ya Nchi, Mipango na Uchumi (1983), Wizara ya Fedha na Uchumi (2008) na Wizara ya Fedha (2010).

    Mabadiliko ya majina haya yalienda sanjari na mabadiliko ya muundo na majukumu ya  Wizara ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa Idara na vitengo mbalimbali kwa lengo la kuchangia uboreshaji wa ufanisi katika uendeshaji wa shughuli za Serikali.

    Idara na taasisi hizo ni pamoja na Idara ya Uchambuzi wa Sera – Kitengo cha Sera za Madeni, Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU), Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Tume ya Pamoja ya Fedha.

    Wizara hii katika kutekeleza majukumu yake imekuwa na mafanikio mengi kupitia Taasisi, Idara na Vitengo mbalimbali vilivyo chini yake. 

    Miongoni mwa mafanikio hayo yanatokana na juhudi na maarifa ya kutekeleza majukumu kupitia Taasisi, Idara na Vitengo vyake.

    Idara ya Uchambuzi wa Sera – Kitengo cha Sera za Madeni katika kipindi cha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na Idara ya Fedha za Nje imeweza kutekeleza kwa mafanikio majukumu yaliyo chini ya idara hizo.

    Kwa kipindi chote cha miaka 50 uchambuzi wa deni la Taifa uliofanyika mwezi Septemba, 2013 unaonesha kwamba deni la Taifa limeendelea kuwa himilivu.

    Uhimilivu huo wadeni la Taifa unaonekana kupitia viashiria mbalimbali vilivyowekwa na kukubaliwa kimataifa. Vinavyohusisha deni la Taifa na Pato la Taifa , mapato ya ndani na mauzo ya nje ya nchi.

    Matokeo ya uchambuzi wa uhimilivu wa deni la taifa kama inavyoonekana kwa uwiano wa thamani ya sasa ya deni la Nje kwa Pato la Taifa kwa mwaka  2013 unaonesha ulikuwa ni asilimia 24.8 wakati na ukomo wake ni  asilimia 50.

    Uwiano wa thamani ya sasa ya deni la nje kwa thamani ya mauzo nje ya Nchi ni asilimia 98.3  na ukomo wake ni asilimia 200. Uwiano wa Thamani ya sasa ya deni la nje kwa Mapato ya Ndani ni asilimia 121.2 na ukomo wake ni asilimia 300.

    Pia Uwiano wa Ulipaji wa deni la nje ikilinganishwa na thamani ya Mauzo ya bidhaa Nje ya Nchi asilimia 3.3  na ukomo wake ni asilimia  25.

    Uwiano wa Ulipaji wa Deni ikilinganishwa na Mapato ya ndani ni asilimia 4.3 na ukomo wake ni asilimia  22 wakati Thamani ya sasa ya deni la Serikali ikilinganishwa na Uwiano wa Pato la Taifa ni asilimia 40.5  na ukomo wake ni asilimia  74.

    Tangu kuasisiwa kwa muungano, Tanzania imeendelea kuwa na mafanikio makubwa katika matumizi ya misaada na mikopo kutoka Ndani na Nje ya nchi katika kujiletea maendeleo yake.

    Katika kipindi chote cha Muungano, Wizara ya Fedha imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali kwa kutumia misaada na mikopo inayopokelewa kutoka kwa wahisani na taasisi za fedha kutoka Ndani na Nje ya nchi.

    Baadhi ya miradi iliyotekelezwa kupitia misaada na mikopo hiyo katika matumizi mbalimbali kwa pande mbili za Muunganoni pamoja na usambazaji wa maji kutoka Ruvu Chini kwenda Miji ya Chalinze, Pwani, Dar es salaam, Unguja na Pemba.

    Kwa upande wa elimu, Wizara ya Fedha imesimamia utekelezaji wa ujenzi wa vyuo vikuu nchini miongoni mwao ikiwa ni Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA).

    Miradi mingine ya Elimu ni ujenzi wa shule za sekondari za Kimuteni Unguja na Mkanyageni Pemba.

    Kwa upande waMawasiliano, Wizara kupitia wahisani ilipokea misaada mbalimbali, na kufanikiwa kuboresha miradi ya Tehama ambapoMkongo wa Taifa umejengwa Tanzania Barana kuwezesha kuwepo kwaSerikali mtandao Zanzibar.

    Katika kuhakikisha askari wanapata na kuwajengea mazingira mazuri ya kazi, Wizara imefanikiwa kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa nyumba za makazi ya askari polisi maeneo ya barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaa pamoja naUnguja na Pemba.

    Miradi mingine iliyotekelezwa kupitia Wizara ya Fedha niujenzi na ukarabati wa barabara mbalimbali nchini.

    Barabara hizo ni pamoja na zilizoko Pemba ambazo ni barabara za Wete – Gando, Wete – Konde, Raha – Hukunjwi, Mtuhaliwa – Chake na kwa upande wa Unguja barabara za Kidmni – Kitope na Machui – Ring.

    Kwa upande wa Tanzania Bara, barabara zilizojengwa na kukarabatiwa kupitia Wizara ya Fedha ni pamoja na barabara ya Dar es Salaam hadi Dodoma, Chalinze hadi  Segera na Dar es Salaam kupitia Lindi hadi Mtwara.

    Kwa kuwa kilimoni uti wa mgongo wa taifa, Wizara ya Fedha imekuwa ikipokea misaada na mikopo mbalimbali na kuielekeza kwenye Wizara husika ili iweze kusimamia miradi iliyokusudiwa.

    Miradi ya Kuendeleza Kilimohaikuachwa nyuma ambapokilimocha mpunga kwa njia ya umwagiliaji kinatekelezwa Zanzibar, Kilimanjaro, Morogoro.Kumekuwepo pia  na usambazaji wa mbolea kwa wakulima katika pande zote mbili za muungano ili kuboresha uzalishaji na kuongeza tija kwa mazao ya chakula na biashara na hivyo kuleta maendeleo endelevu ya taifa kwa lengo la kuiwezesha nchi ifikie uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

    Mafanikio haya ya Wizara yanatokana na msingi imara uliojengeka ndani ya watumishi kwa kuzingatia taaluma zao, ubunifu, kuwajali wageni na wateja wanaofika ofisini kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali ofisini humo, kujitoa kufanya kazi kwa moyo kwa kuzingatia weledi wa taaluma zao na kwa kufuata maadili ya utumishi wa umma na kutoa huduma hizo kwa wakati.

    Mafanikio haya yanatokana nausimamizi mzuri wa sera za uchumi ili kuweka mazingira mazuri ya kisera kwa lengo la kuwezesha kufikiwa kwa malengo ya maendeleo ya Taifa.

    Ili Wizara iendelee kufanya vizuri katika kumhudumia Mtanzania, inaendelea kuandaa mafunzo mbalimbali ya muda mfupi na mrefu kwa mujibu wa mahitaji.

    Kwa kuzingatia umuhimu wa rasilimali watu, Wizara imejipanga kufanikisha uendelezaji wa watumishi kwa kuwaongezea ujuzi na maarifa ya ukusanyaji, uchambuzi na uwasilishaji wa takwimu zinazoonesha hali halisi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

    Tukubali kuwa "Palipo na nia pana njia", Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaheshimu na kuzingatia misingi ya utu, uhuru, haki, usawa, udugu, amani, umoja, na mshikamano katika nyanja zote za maisha yetu.

    Hali hii itaifanya nchi isonge mbele na Muungano uendelee kuimarika na kuufanya kuwa ni mfano wa kuigwa kwa mataifa mengine Afrika na Dunia kwa ujumla, ndio maana wimbo wetu wa taifa unadhihirisha nchi yetu kudumisha uhuru na umoja.

    Hivyo Tanzania ni moja, na watu wake ni wamoja ni wajibu wetu sote kuimarisha na kudumisha uzalendo wa Taifa miongoni mwa Watanzania ili kuendeleza dhamira yetu ya kulinda, kuimarisha na kudumisha Muungano ulioasisiwa kwa kuchanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar.   

  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.