June 28, 2014

  • Dk Salim: Sina Mpango na Urais 2015, Sifikirii Tena, Hii ni Zamu ya Kizazi Kingine



    Dk Salim: Sina Mpango na Urais 2015, Sifikirii Tena, Hii ni Zamu ya Kizazi Kingine
    Asema alipogombea 2005 alibaini kwamba mbali na rekodi ya utendaji, kuna mambo mengine yanayohitajika katika kinyang'anyiro hicho

    Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim amesema hana mpango na hafikirii tena kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

    Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam jana, Dk Salim alisema alipowania nafasi hiyo mwaka 2005, hakuwa na ufahamu mzuri kuhusu mchakato huo lakini baadaye alibaini kwamba, mbali na rekodi ya utendaji, kuna mambo mengine yanayohitajika katika kinyang'anyiro hicho na kwamba hata watu wanaomfikiria na kutaja jina lake miongoni mwa wanaoweza kuwania tena nafasi hiyo, wanakosea.

    "Sifikirii tena, hii ni zamu ya kizazi kingine. Ila nitaendelea kuisaidia nchi yangu katika nyanja mbalimbali kadri ya uwezo wangu," alisema.

    Dk Salim ambaye mbali na uwaziri mkuu amewahi kushika nafasi nyingine mbalimbali kitaifa na kimataifa, alisema uzoefu alioupata katika kinyang'anyiro cha urais unatosha.

    Alipoulizwa kama uzoefu huo ni mbaya au mzuri kwake, alisema ni mchanganyiko.

    Dk Salim aliwahi kugombea nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) na kushindwa kutokana  na kura ya veto ya Marekani, pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), sasa Umoja wa Afrika (AU). Pia aliwahi kuwa Rais wa Bunge Kuu la UN mwaka 1979 na 1980.

    Licha ya kujitokeza mara moja kuomba uteuzi wa CCM kuwania urais 2005, nyota yake katika nafasi hiyo ilianza kuwaka tangu mwaka 1985 akiwa Waziri Mkuu pale aliposhindanishwa katika Kamati Kuu ya CCM na aliyekuwa Waziri Mkuu, Rashidi Kawawa pamoja aliyekuwa Makamu wa Rais wakati huo, Ali Hassan Mwinyi ambaye alipitishwa kiitifaki na kushinda kiti hicho.

    Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa alisimulia jinsi Mwinyi alivyopita, kwa sababu alikuwa Makamu wa Rais, hivyo wajumbe wa Kamati Kuu walikosa hoja na sababu za kumwacha na kumchukua Waziri Mkuu aliyekuwa chini yake kiitifaki.

    "Makamu wa Rais ukimruka maana yake hatoshi, wakaona hawana maelezo hayo, ikabidi wamteue Mwinyi," alisema Msekwa.

  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.