June 27, 2014

  • MAOFISA WA TUME YA HAKI ZA BINADAMU WAANZA KUPOKEA MALALAMIKO YA WANANCHI KWA NJIA YA SIMU




    MAOFISA WA TUME YA HAKI ZA BINADAMU WAANZA KUPOKEA MALALAMIKO YA WANANCHI KWA NJIA YA SIMU
    Na Allan Ntana, Tabora

    TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora hapa nchini imeanza kuboresha huduma zake kwa jamii baada ya kuanzisha huduma mpya ya kupokea malalamiko ya wananchi kwa njia ya ujumbe mfupi kupitia simu za kiganjani.

    Hayo yalibainishwa jana na Maofisa wa Tume hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa stendi ya zamani mjini Tabora ambao ulilenga kutambulisha na kuhamasisha matumizi ya huduma hiyo kwa wananchi na wadau mbalimbali wenye malalamiko yoyote au kutotendewa haki mkoani hapa.

    Afisa uchunguzi  na mwanasheria  wa tume hiyo Caroline Shayo alisema tume hiyo iliyoanzishwa Julai 2001hapa nchini imelenga kulinda na kutetea maslahi ya wananchi ambapo imejiwekea utaratibu wa kupokea na kushughulikia malalamiko mbalimbali ya wananchi kuanzia ngazi ya serikali kuu mpaka ngazi ya vijiji.

    'Mpaka sasa tume hii ina ofisi katika kanda  4 tu ambazo ni Lindi, Mwanza, DSM na Zanziba, lengo letu ni kuelimisha umma ili wafahamu wajibu wao ni nini, haki zao ni zipi, wanawezaje kuzipata na kwa utaratibu gani', aliongeza Shayo.

    Mchambuzi Mkuu wa mifumo ya habari na mawasiliano wa tume hiyo Wilfred Warioba, alisema ili kurahisisha mawasiliano ya tume hiyo na wananchi, wameamua kuanzisha teknolojia hiyo ya kutuma malalamiko moja kwa moja kupitia mitandao ya simu zao kwa njia ya ujumbe mfupi yaani 'sms'.

    Aliongeza kuwa tume ya haki za binadamu na utawala bora ni chombo huru ambacho kiko kwa ajili ya kutetea wananchi wote na hakitozi gharama yoyote ya kuwasilisha malalamiko.

    Mtaalamu huyo aliongeza kuwa tume inapokea malalamiko ya aina yoyote ile bila kujali yameletwa na nani ili mradi yawe na ukweli ndani yake, kinachotakiwa ni mhusika kuandika malalamiko yake kwenye sehemu ya kuandika ujumbe mfupi kwenye simu yake ya mkononi na kisha kuutuma kwenye namba 0754 460 256.

    Ujumbe huo ukishapokelewa mhusika (mlalamikaji) atapigiwa simu na kuulizwa baadhi ya mambo ili kujua kiini cha malalamiko yake kwa lengo la kujiridhisha ikiwa ni pamoja na kufahamu anaitwa nani, yuko wapi na mambo mengine yatakayoturahisishia kushughulikia malalamiko yake kwa wepesi zaidi, aliongeza.

    Aidha Warioba alisema mwananchi yeyote atakayeleta malalamiko yake kwa 'sms' anatakiwa kutumia majina yake halisi na kutaja mahali alipo na si kusema uongo lengo likiwa kurahisisha kazi ya kushughulikia malalamiko yake.

    Alifafanua kuwa tume hii haina upendeleo wowote wa kijinsia katika kushughulikia malalamiko ya wananchi yanayopokelewa huku akibainisha kuwa wananchi walio wengi  bado hawajajua wajibu wao kwani wanayo matatizo mengi ila wanayanyamazia tu ndio maana tumewatembelea ili waseme waziwazi.

    Naye Catherin Malimbo, Afisa Uchunguzi Mwandamizi idara ya haki za binadamu, aliwataka wananchi wote wenye malalamiko ya masuala ya ardhi, viwanja, biashara na ndoa kuleta malalamiko yao pia kwani wapo tayari kuyafanyia kazi sambamba na kutoa ushauri kwa mamlaka husika namna ya kumaliza kero hizo kisheria.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.