June 27, 2014

  • APRM yapata CEO mpya




    APRM yapata CEO mpya

    Na Mwandishi Wetu, Malabo

    MPANGO wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) umempata Mtendaji wake Mkuu mpya atakayeongoza ofisi ya taasisi hiyo katika ngazi ya Bara la Afrika iliyoko mjini Midrand, Afrika Kusini.

    Uamuzi huo umefikiwa katika Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi za APRM uliofanyika mjini hapa, ambapo aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Mpango wa NEPAD, Dkt. Ibrahim Assane Mayaki kutoka Niger ndiye amehamishiwa APRM.

    Mabadiliko hayo yamekuja wakati ambapo wakuu wa Nchi za APRM waliokutana mjini hapa wakiwa wamesisitiza umuhimu wa mageuzi na APRM kutekeleza majukumu yake kwa wakati katika kufanya tathmini za utawala bora Barani Afrika.

    Dkt. Mayaki ambaye kabla ya uteuzi huo alipata kuisimamia APRM ilipokuwa taasisi moja na Nepad anaingia katika APRM akichukua nafasi ya Bw. Assefa Shifa raia wa Ethiopia.

    Akizungumza mjini hapa, Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, Bi. Rehema Twalib anayehudhuria mikutano hiyo, alithibitisha kufanyika kwa uteuzi huo. Tanzania ni miongoni mwa nchi 35 za Umoja wa Afrika zilizokwishajiunga na APRM.

    Kitaaluma Dkt. Mayaki anashahada ya umahiri Kutoka Chuo Kikuu kiitwacho National School of Public Administration (Enap), Quebec, Canada na pia ana shahada ya uzamivu (PhD) katika sayansi za utawala kutoka Chuo Kikuu cha Paris I.

    Kati ya mwaka 1996 na 2000 alitumikia nafasi mbalimbali katika Baraza la Mawaziri nchini mwake kabla ya kuhamia katika masuala ya utafiti na uhadhili.

    Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika juzi, Rais wa Liberia Mama Ellen Johnson-Sirleaf ambaye ndiye Mwenyekiti wa APRM katika ngazi ya Afrika, aliziasa nchi wananchama kutekeleza Mpango huo kwa umakini na kutaka mageuzi makubwa.

    Katika mkutano huo pia wakuu wa nchi walipitisha wazo la kuwa na semina mbalimbali za uhamasishaji ambapo Tanzania iliteiuliwa kuwa mwenyeji wa semina itakayohusisha nchi za Afrika Mashariki.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.