June 27, 2014

  • WASTAAFU WAHIMIZWA KUUDUMISHA MUUNGANO NA UHIFADHI WA MAZINGIRA



    WASTAAFU WAHIMIZWA KUUDUMISHA MUUNGANO NA UHIFADHI WA MAZINGIRA
    Watumishi waliostaafu katika Ofisi ya Makamu wa Rais wametakiwa kuendelea na moyo wa kuudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na uhifadhi wa mazingira.

    Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano),  Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa rai hiyo jana wakati alipokuwa akizungumza katika hafla ya kuwaaga wastaafu wapatao 12 wa kada ya maafisa katika ofisi hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa jijini Dar es salaam.

    Mheshimiwa Samia alisema wastaafu hao wanapaswa kuendelea na moyo huo kwani jukumu la kuudumisha Muungano na uhifadhi wa mazingira ni la kila mmoja katika jamii.

    "Natambua kwamba ninyi nyote mliostaafu na mtakao staafu ni mabalozi wazuri katika kuelimisha jamii kuhusu majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais yanayohusu kuudumisha Muungano wetu pamoja na kuhifadhi mazingira," alisema Waziri Samia na kuongeza

    "Natarajia mtakuwa mfano katika kuendeleza jitihada za kudhibiti uharibifu wa mazingira katika jamii inayowazunguka."

    Aidha, aliwaasa  wastaafu hao kushirikiana na Asasi na Taasisi mbalimbali zilizoko kwenye maeneo yao ili kupitisha mawazo ambayo yatasaidia kuwaletea wananchi maendeleo 

     "Kupitia mawazo yenu Taasisi kama hizi zitaweza kujenga uwezo zaidi katika masuala ya maendeleo ya jamii hususan fursa za ajira kwa vijana wetu," alisema

    Kwa wale wanaoendelea na utumishi wa umma Waziri Samia aliwataka waige mfano kwa watumishi waliostaafu na kuendelea kujenga tabia ya uadilifu, uaminifu na uchapakazi.

    Wastaafu hao walipatiwa zawadi ya jiko la gesi kila mmoja jambo ambalo Naibu Katibu Mkuu katika Ofisi ya Makamu wa Rais Eng. Angelina Madete alipokuwa akizungumza wakati wa kumkaribisha mgeni rasmi alisema ofisi iliandaa zawadi hiyo ili  wastaafu hao wakawe mabalozi wazuri wa kuhimiza matumizi ya jiko la gesi na hivyo kusaidia katika suala zima la uhifadhi wa mazingira.



  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.