RC-Dar-es-Salaam
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiq.
Na Mwandishi wetu
Baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wamemuunga mkono Mkuu wa Mkoa Saidi Meck Sadiq, na Mkurugenzi wa Jiji Wilson Kabwe kwa hatua walizochukua dhidi ya wamachinga.Kufuatia uungwaji mkono wakaazi hao wamemtaka Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu (CCM), kuacha kuwatetea wafanyabiashara wadogo (Wamachinga), wanaofanya biashara katika maeneo ya siyo rasmi.Hivi karibuni Mbunge huyo, akiwa bungeni alikaririwa na vyombo vya habari akiwashutumu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik na Mkurugenzi wa Jiji, Wilson Kabwe, kuwa wamekuwa wakilivuruga jiji hilo kwa kuwakamata Wamachinga.Wakizungumza kwa nyakati tofauti na jijini wakazi hao, walisema ni jambo la kushangaza, baadala ya  mbunge kusimama kidete kwa kupigania sheria baadala yake anaungana na kuwatetea watu wanaovunja sheria.

Walisema wanamuunga mkono mkuu wa mkoa na Mkurugenzi wa Jiji kwa sababu  baada ya kubaini kazi yao imeleta tija kwani mitaa mingi ya Kariakoo imekuwa safi pia msongamano wa magri na watu umepungua.
Kitwana Seif, ambaye ni mkazi wa Kinyerezi, alisema ukiona kiongozi yeyote anatetea watu wanaovunja sheria basi hiyo ni ishara tosha kuwa ameshindwa majukumu yake na hana uhakika wakuendelea na kazi anayoifanya.
Alishangaa kumsikia Zungu akitamka maneno haya "Sadik na Kabwe hawafai hata kidogo, wanachokifanya pale Dar es Salaam ni hatari kwetu maana wanawaondoa wapiga kura wa katiba mpya na wa uchaguzi mkuu, wakiachwa waendelee na utaratibu wao tusidhani kama tutapata kura," alinukuu kauli.
wilson-kabwe
Mkurugenzi wa Jiji Wilson Kabwe.
Kwa upanade wake Mwanaharakati wa Mazingira Amos Joseph, alisema, haingii akilini kwa mbunge huyo kuwatetea watu wanaovunja sheria eti kwa kisingizio cha kuwa ni wapiga kura wake.
"Wamachinga ni tatizo jijini Dar es Salaam kwa sababu wanachangia msongamano wa magari pia kufanya watembea kwa miguu kukosa uhuru kwasababu wanafanya biashara hata kwenye maeneo ya hifadhi ya barabara ambako wakati mwingine ni maeneo ya watembea kwa miguu,"alisema Joseph.
Alitoa wito kwa Mkuu wa Mkoa na Mkurugenzi wa jiji kuwa waendelee na kazi hiyo nzuri ya kuwadhibiti Wamachinga huku wakimpuuza mbunge huyo ambaye hajui wajibu wake.
Mmoja wa Watendaji wa  Manispaa moja jijini, alisema sio kweli kama wanapinga utaratibu unaondelea wa kuwaondoa wamachinga kwani hata wao walikuwa hawapendezwi na uwepo wafanyabiashara hao katika maeneo yasio rasmi.
Alisema kama ingekuwa sio wanasiasa kuingilia kati majukumu yao anahakika kwa kushirikiana na askari mgambo wangefanikiwa kuwazuia kwenye maeneo hayo tangu awali.
Zungu alitoa shutuma hizo juzi bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa bajeti ya serikali ya mwaka 2014/2015 ambapo alisema viongozi hao wawili wametangaza vita dhidi ya wamachinga, mama na baba lishe kwa kupora bidhaa zao na kuwavunjia maeneo wanayofanyia shughuli zao za kujipatia kipato.
"Sadik na Kabwe hawafai hata kidogo, wanachokifanya pale Dar es Salaam ni hatari kwetu maana wanaowaondoa wapiga kura wa katiba mpya na wa uchaguzi mkuu, wakiachwa waendelee na utaratibu wao tusidhani tutapata kura," alisema.