Wananchi wameshauriwa kufuata kanuni na taratibu sahihi za upatikanaji wa huduma za Maji ili kujiepusha na utapeli unaofanywa na baadhi ya wananchi wachache wenye lengo la kuharibu utendaji kazi wa dawasco na kuleta hasara kubwa kwa jamii.
Hayo yameelezwa na Afisa Uhusiano wa Dawasco Bi Everlasting Lyaro wakati wa maadhimisho ya wiki ya Utumishi iliyofunguliwa rasmi jana jijini Dar.
Alisema kauli mbiu ya mwaka huu inaendana na dhima nzima ya utumishi uliotukuka unaoainsha misingi na kanuni za utumishi ili kuimarisha utawala bora na uwazi sehemu ya kazi.
"Taratibu na kanuni sahihi za upatikanaji wa huduma ziko wazi kwa taasisi yetu kufuata taratibu sahihi ikiwepo kufika ofisi ya dawasco iliyo kwenye kanda yake na kupewa fomu sahihi iliyo na maelezo binafsi ya Mteja, na ikiwa mwombaji ni kampuni au shirika atatakiwa kuja na barua ya maombi iwe na muhuri wa Shirika" alisema Lyaro.
Aliongeza kuwa taratibu hizo ziko wazi na wananchi wanapaswa kufika kwenye ofisi za Dawasco ili kupunguza malalamiko wanayopokea baada ya kuhujumiwa na watu wachache wanaotoa huduma hiyo kinyume na taratibu.
Aliwahakikishia wananchi kuwa mwombaji atarajie kuunganishiwa huduma ya Maji katika kipindi cha siku 14 hadi 21 baada ya kukamilisha malipo ya ada / gharama ya kuunganishiwa Maji.
Maadhimisho ya wiki ya utumishi wa Umma yameanza rasmi wiki hii na kitaifa yamefunguliwa na Waziri Ofisi ya Rais, Utawala Bora Mh George Mkuchika ikiwa na kauli mbiu ya " Mkataba wa Msingi na kanuni za Utumishi wa Umma barani Afrika ni chachu ya kuimarisha Utawala Bora na uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi"
Afisa Uhusiano wa DAWASCO,Bi Everlasting Lyaro (katikati) akitoa ufafanuzi wa shughuli na huduma zinazotolewa na DAWASCO kwa mwananchi aliyefika kwenye banda la DAWASCO wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma inayoendelea katika viwanja vya Mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam. Pembeni ni Meneja wa huduma kwa mteja Bi Tumakwezi Sayi
0 comments:
Post a Comment