June 18, 2014

  • IPTL yapiga jeki ujenzi wa kituo cha polisi cha Mbweni- Malindi




    IPTL yapiga jeki ujenzi wa kituo cha polisi cha Mbweni- Malindi
     Meneja Mkuu wa Utawala na Rasilimali wa Jeshi la Polisi la Tanzania, Kamishna wa Polisi Thobias Andengenye (kulia) akifurahia jambo na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Bw. Harbinder Sethi (kushoto), wakati akipokea hundi ya shilingi milioni 10 iliyotolewa na IPTL kuchangia ujenzi wa kituo cha Polisi cha Mbweni-Malindi. Katikati ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalum la kipolisi Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi, Suleiman Kova.
    Meneja Mkuu wa Utawala na Rasilimali wa Jeshi la Polisi la Tanzania, Kamishna wa Polisi Thobias Andengenye (kulia) akipokea hundi ya shilingi milioni 10 Kutoka kwa Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Bw. Harbinder Sethi (kushoto) iliyotolewa na kampuni yake kuchangia ujenzi wa kituo cha Polisi cha Mbweni-Malindi.  Katikati ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalum la Kipolisi Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi, Suleiman Kova.
    ======  ========
    KAMPUNI ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) imepiga jeki mradi wa ujenzi wa kituo cha polisi cha Mbweni Malindi kwa kuchangia zaidi ya silingi milioni 10, ikiwa na lengo la kuyafanya maeneo hayo kuwa maeneo salama kibiashara.

    Wakati akikabidhi mchango huo kwa maafisa wa polisi kanda maalum la kipolisi Dar es Salaam katika eneo la ujenzi mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti Mtendaji wa IPTL, Harbinder Sethi alisema kampuni yake imeitikia wito wa kusaidia ujenzi huo sababu inaamini kuwa usalama thabiti utasaidia maendeleo ya haraka kiuchumi katika eneo husika. 
      
    "IPTL inaelewa kuwa ili kupata maendeleo thabiti ya kiuchumi katika sehemu yoyote ile, ni lazima eneo hilo liwe na usalama wa kutosha. Utakapo boresha usalama, wawekezaji wataleta fedha  sababu watakuwa na uhakika kuwa fedha zitakuwa salama. "Ongezeko la uwekezaji katika jamii pia litabadilisha hali ya kiuchumi na maisha ya watu. 

    Hii ndiyo maana tumetenga sehemu ya pato letu ili kusaidia miradi mbali mbali ya kijamii ikiwa ni sehemu ya shughuli zetu za kusaidia miradi ya kijamii inayotuzunguka," alisema.

    Bw. Sethi alisema kuwa IPTL imejikita katika kusaidia miradi mbali mbali yenye chachu kubwa ya kuwaletea watu maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa ujumla.

    Akipokea hundi hiyo kwa niaba ya Jeshi la Polisi, Meneja Mkuu wa Utawala na Rasilimali katika Jeshi la Polisi la Tanzania, Kamishna wa Polisi, Thobias Andengenye alisema mchango huo utasaidia kukamilisha mradi huo utakaogharimu zaidi ya shilingi milioni 700."Kwa niaba ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu, napenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa mchango huu.

    Ninaamini kwamba baada ya mradi huu kukamilika na kuzinduliwa, uwepo wa polisi utasaidia kuboresha hali ya usalama katika eneo hili la Mbweni. Kama mnavyofahamu, hakuna maendeleo ya kiuchumi yanayoweza patikana katika eneo lisilokuwa na usalama. Tunakushukuruni sana," alisema. 

    Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa kituo hicho cha polisi, Reeves Mutalemwa alisema maombi ya ujenzi wa kituo hicho cha polisi yalitumwa na wakazi wa Mbweni ambao pia wamekuwa wakichangia katika mradi.



  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.