June 16, 2014

  • VIINGILIO MECHI ZA TAIFA STARS SASA KARIBU NA BURE - MALINZI



    VIINGILIO MECHI ZA TAIFA STARS SASA KARIBU NA BURE - MALINZI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    JAMAL Malinzi, rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) amesema kwamba kuanzia sasa viingilio vya mechi za timu ya taifa, Taifa Stars kwa maeneo yasiyo ya VIP vitakuwa vya bei nafuu ili kutoa fursa kwa watu wengi kwenda kuishangilia timu hiyo.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Malinzi amesema kwamba wamejifunza hilo kutoka kwa Zimbabwe ambao kwenye mechi za timu ya taifa viingilio vya eneo la mzunguko huwa vya chini mno.

    "Tumeona Zimbabwe, walifanya kiingilio cha mechi yetu na wao dola moja ya Kimarekani, ambayo ni chini ya shilingi 2,000 ya Tanzania, na watu walifurika uwanjani,"alisema.

    Malinzi amesema mashabiki wa soka watarajie viingilio nafuu mno kuanzia sasa katika mechi za timu ya taifa na amewataka wawe wanajitokeza kwa wingi bila kujali mvua wala jua kwenda kuisapoti timu hiyo.
    Taifa Stars inatarajiwa kuondoka nchini wiki ijayo kwenda Botswana kuweka kambi ya mwezi mmoja kujiandaa na mchezo dhidi ya Msumbiji kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani Morocco.
    Wachezaji wote wa Taifa Stars waliruhusiwa kurejea makwao jana kwa ajili ya kujiandaa na safari hiyo na watakutana tena kesho.
    Stars inayofundishwa na Mholanzi, Mart Nooij itaondoka nchini Juni 27 kwenda Gaborone, ambako itaweka kambi ya mazoezi hadi Julai 7 itakaporejea nchini.  
    Taifa Stars itamenyana na Msumbiji 'Mambas' katika hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco baada ya kuitoa Zimbabwe juzi kwa jumla ya mabao 3-2, ikianza kwa ushindi wa 1-0  nyumbani na kumaliza kwa sare ya 2-2 juzi mjini hapa.
    Mechi yake kwanza itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Julai 19 na 20 mwaka huu, wakati mechi ya marudiano itafanyika Msumbiji kati ya Agosti 2 na 3 mwaka huu. 
    Stars pia inatarajiwa kuwa na mchezo wa kujipima nguvu na Uganda kabla ya kumenyana na Msumbiji.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.