June 04, 2014

  • Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Pandu Ameir Kificho Avunja Ukimya na Kujibu Tuhuma Zilizotolewa Dhidi yake kuhusu Mfumo wa Serikali Tatu



    Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Pandu Ameir Kificho Avunja Ukimya na Kujibu Tuhuma Zilizotolewa Dhidi yake kuhusu Mfumo wa Serikali Tatu
     Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Pandu Ameir Kificho akivunja ukimya wa muda mrefu dhidi ya tuhuma zilizotolewa dhidi yake kuhusu mfumo wa Serikali Tatu wakati akifafanua hoja hiyo kwenye mkutano wa hadhara wa Jimbo la Magogoni hapo uwanja wa Kwamabata.
     Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif akigawa Seti za Jezi kwa baadhi ya timu za soka za Jimbo la Magogoni zilizotolewa msaada na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia CCM Hapo uwanja wa Kwamabata Magogoni.
    Wana CCM wa Jimbo la Magogoni wakionyesha Vidole kuashiria mbili zatosha wakimaanisha kuendelea kuunga mkono Sera ya CCM ya kutetea mfomo wa Serikali mbili kama baadhi ya machapisho yao yanavyosomeka mitaani. Picha na Hassan Issa-Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar
    --
    Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi ameeleza kwamba tabia ya matusi inayoonekana kubebwa na baadhi ya wanasiasa inachochea kuendeleza uhasama na chuki miongoni mwa Jamii hapa Nchini.
     
    Alisema tabia za matusi kwa muda mrefu zimeipelekea Zanzibar kukosa utulivu wa kisiasa na jamii kushuhudia matendo mbali mbali yaliyo kinyume na maadili ambayo yalikuwa yakifanywa na baadhi ya watu hasa Vijana kufuatia ushawishi wa matusi hayo.
     
    Balozi Seif alieleza hayo wakati akizungumza na Viongozi, wanachama  wa CCM na Wananchi mbali mbali katika Mkutano wa hadhara wa Chama cha Mapinduzi uliofanyika katika uwanja wa Kwamabata Jimbo la Magogoni ambao umeandaliwa na Wajumbe wa Baraza ala Wawakilishi kupitia CCM ukilenga kuimarisha chama hicho.
     
    Balozi Seif ambae pia ni makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba upo ushahidi wa wazi kwa baadhi ya wanasiasa waliokosa mvuto wa kukubalika kisiasa wakitumia kuendeleza matusi yanayowatoa kwenye maadili wanasiasa hao.     
                 
    " Tumeshuhudia wazi na kwa muda mrefu sera za matusi zilizokuwa zikibebwa na baadhi ta wanasiasa zimekuwa zikiwatoa kwenye maadili sahihi ya Kisiasa ". Alisema Balozi Seif.
     
    Akizungumzia Bunge Maalum la Katiba lililokuwa na kikao chake kabla ya kuanza kwa Bunge la Bajeti Balozi Seif alisema kilichokuwa kikijadiliwa na Wajumbe wa Bunge hilo ni Rasim na wala si Katiba kama baadhi ya wanasiasa walivyokuwa wakipotosha wananchi.
     
    Walisema Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba wana haki ya kujadili, kupendekeza na hata kubadilisha baadhi ya vipengele vilivyomo ndani ya rasimu hiyo kwa mujibu wa kanuni ambavyo wanahisi vitakuwa na maslahi kwa Umma wa Watanzania.
     
    " Aliyoleta Bungeni Mwenyekiti wa Tume ya mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Sinde Warioba ni mapendekezo tu ambayo Wabunge wana haki ya kuyapitia kwa kuyajadili, kupendekeza na hata kurekebisha baadhi ya vifungu ili kupata rasimu itakayopelekwa kwa Wananchi kuipigia kura endapo wameafikiana nayo ". Alisema Balozi Seif.
     
    " Msimamo wa Chama cha Mapinduzi uko wazi katika mustakabali wa Nchi hii wa kupendekeza mfumo wenye Serikali Mbili zilizofanyiwa marekebisho makubwa tofauti na mapendekezo ya rasim hiyo iliyoelezea Serikali Tatu ". Alifafanua Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa.
     
    Balozi Seif aliwatoa hofu Viongozi, Wana CCM na Wananchi hao kwamba Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanatarajiwa kuendelea na mjadala wao mwezi Agosti mwaka huu kwa kuendelea na Ibara zilizobakia baada ya kukamilisha sura ya kwanza na sita ambazo zinahusu mfumo wa muundo wa Serikali.
     
    Akivunja ukimwa wa muda mrefu kufuatia shutuma zilizompata za kuhusishwa na utiaji saini waraka wa Baraza la Wawakilishi wa kutaka mfumo wa Serikali tatu kwenye mabadiliko ya Katiba ya Muungano  Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Pandu Ameir Kificho alisema kilichojadiliwa na Wajumbe wa Baraza hilo kwa pamoja  ni mfumo utakayoipa Zanzibar nguvu zaidi za kujitegemea Kiuchumi.
     
    Mh. Kificho ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa aliwaeleza wana ccm na viongozi hao wa Magogoni kwamba waraka wa Baraza la Wawakilishi kamwe hauna kipengele hata kimoja kilichoelezea kwamba Baraza hilo limependekeza mfumo wa Serikali Tatu.
     
    Aliwahakikishia wana ccm na wananchi hao kwamba ataendelea kuwa muumini wa Chama cha Mapinduzi na hiyo inatokana nay eye kuzaliwa ndani ya mifupa ya Chama cha Ukombozi cha Afro Shirazy Party na kulelewa na Chama cha Mapinduzi.
     
    " Si walaumu wazee wangu wa CCM waliotoa matamshi mazito dhidi yangu nah ii inatokana na baadhi ya watu wakiwemo viongozi kujaribu kuupotosha ukweli halisi uliomo ndani ya waraka huo ". Alifafanua Mh. Kificho.   
    Akitoa salamu Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar Vuai Ali Vuai aliupongeza uamuzi wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kupitia CCM kwa kujizatiti kutetea chama cha Mapinduzi kwa pamoja katika maeneo mbali mbali Nchini.
     
    Ndugu Vuai alisema Wawakilishi hao sasa wameelewa na kufahamu kwa undani kero na mahitaji wanayoyataka wanachama wao pamoja na wananchi katika kujitelea maendeleo yano ndani ya majimbo yao. 
     
    Mapema Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia Chama cha Mapinduzi ambao ndio walioandaa Mkutano huo waliwatahadharisha Wana CCM na wananchi  wote kujaribu kuwa mbali na baadhi ya watu wanaojaribu kuuchezea Muungano.            
     
    Wawakilishi hao wa CCM walisema wameamua kwa makusudi kufanya ziara za mara kwa mara katika maeneo mbali mbali nchini ili kuwaelimisha Wananchi juu ya hatari inayoonekana kupaliliwa na baadhi ya watu hao katika kuyachezea maisha ya Watanzania.
     
    " Tumeamua kuwa wazi katika kutetea mfumo wa Serikali mbili ndani ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania tukielew kwamba nje ya mfumo huu ndugu zetu wanaoendesha maisha yao upande wa Pili wa Muungano Tanzania Bara watakuwa hatarini. Hili liko wazi kutokana na baadhi ya kauli za viongozi wa vyama vya upinzani upande wa  Bara ". Walisema Wajumbe hao wa Baraza la Wawakilishi wa CCM.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.