June 09, 2014

  • CHANZO WA UGONJWA WA WASICHANA KUANGUKA SHULENI CHATAJWA




    CHANZO WA UGONJWA WA WASICHANA KUANGUKA SHULENI CHATAJWA
    Ugonjwa wa kuanguka na kupiga kelele unaowakumba baadhi ya  wasichana katika shule mbalimbali nchini, umetajwa kusababishwa  na  maambukizi ya hofu inayosababisha mwili kupata dalili za magonjwa yasiyokuwepo.
    Mtaalamu wa saikolojia na theolojia, Mchungaji  John Rowse  kutoka taasisi ya The Uhakika Christian Education Trust Fund kutoka Mbeya, alisema hayo hivi karibuni baada ya kutembelea  shule zinazopata tatizo hilo mara kwa mara na kuzungumza na wazazi, wanafunzi na walimu wa shule hiyo.
    Alisema kuna mambo kadhaa yanayochangia kujenga hofu hiyo ambayo mwili hujitayarisha kuambukizwa, ikiwemo vitisho vya maisha kwa wanafunzi vinavyotokana na mambo mbalimbali kama vile ugomvi na mabadiliko ambapo miili yao inahangaika kujihami.
    Kwa mujibu wa Mchungaji huyo, upo uwezekano kuwa baadhi ya  wanaoanguka, ni wasichana wanaonyanyaswa nyumbani, wengine wanafundishwa kujidharau na wengine wanabaguliwa na kufanyiwa unyanyapaa shuleni.
    Sababu nyingine ya kuanguka kwa wasichana shuleni kwa mujibu wa Mchungaji  Rowse, ni hofu wanayopewa wasichana hao na waganga wa kienyeji  wanaotabiri au kupiga ramli, pamoja na wachungaji au wainjilisti wanaokemea mapepo huku wakiwashika  kichwani, begani au kwenye shingo na kuwatetemesha wasichana hao.
    Mchungaji  Rowse  alisisitiza kuwa  dawa pekee ya  kutibu ugonjwa huo,  ni utulivu kwani wanafunzi hao hususani  wasichana  huambukizana kwa hofu hivyo matibabu yake  ni kupunguza hofu na mawazo.
    "Hofu  hiyo  kwa wasichana  hao  husababishwa  kwa imani potofu, waganga wa kienyeji  wanaotabiri au kupiga ramli ... waganga  hawa  wanapenda kujenga hofu ya uchawi, ili baadaye wajidai kwamba ni wao waliondoa laana na kuleta uponyaji.
    "Dawa ya kusaidia kuzuia matukio hayo ni kuwa na mipango ya kupunguza msongo wa mawazo shuleni, hasa miongoni  mwa  wasichana," alisema.
    Mchungaji  Rowse alipendekeza machifu na waganga  wa jadi  wasikaribishwe shuleni kuwaombea wasichana hao kwa kuwa watawaongezea hofu.
    Pia alipendekeza wachungaji au wainjilisti wanaopenda kushika mtu kichwani, begani au kwenye shingo na kumtetemesha, wasikaribishwe shuleni kwa kuwa nao pia ni hatari.
    "Hata wale wanaokemea mapepo kwa sauti kubwa na wakati wakifanya hivyo hupenda kumwangalia msichana kwa ukali jicho kwa jicho.
    "Katika mazingira hayo,  watoto  watapata  tena  hofu na wakianguka  tena watasema ni pepo, lakini sivyo. Afadhali mchungaji wa amani, amwombee kila mwanafunzi aliyekumbwa na ugonjwa huo kwa sauti ndogo tu na kwa upole na upendo na kumfariji na utulivu. Asitamke wazi neno lo lote juu ya mapepo," alisisitiza.  
    Alishauri kuwa kila shule iwe na mwalimu au mshauri wa kike ambaye hatoi adhabu kwa wasichana, atakayepaswa kujenga urafiki nao na kuwa karibu nao, ili wamwamini na kumwelezea mateso yao ya maisha, nyumbani na shuleni.
    Alisisitiza kuwa  wanafunzi  wa kike  wapewe nafasi za kukutana katika  vikundi,  ili wajadiliane pamoja kuhusu mambo yoyote, pia  walimu  wajitahidi kumpa kila msichana nafasi ya kusikilizwa.
    Alitoa mfano wa Shule ya Msingi Inyonga wilayani Mlele katika Mkoa wa Katavi, ambayo aliitembelea na kuzungumza wazazi, wanafunzi  na walimu wa shule hiyo.
    Alisema baada ya shule hiyo kuanza kutekeleza ushauri huo,   Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Casto Ismail, alimwambia kuwa kasi ya matukio imepungua.
    "Mwalimu Mkuu huyo alinieleza kuwa wamekuwa na mitihani ya darasa ya saba, ambao kwa kawaida husababisha msongo wa  mawazo kwa wanafunzi, lakini hakuna mwanafunzi wa darasa ya saba hata mmoja aliyeanguka wakati huo…katika madarasa mengine ni wachache walioanguka. 
    "Niliwaambia walimu wawe na uvumulivu. Mambo yatatulia kweli baada ya mabadiliko ya imani ya wazazi na jamii… lakini watalaamu bado wanashindwa kuelewa kwa nini hali hiyo inakutwa sana kwa wasichana na wanawake," alisema Mchungaji  Rowse.  
    Mwandishi alifika katika Shule ya Msingi Inyonga na kuzungumza na Mwalimu Ismail, ambaye alieleza kuwa  ugonjwa  huo  ulidumu kwa  zaidi ya miezi  sita tangu ulipowakumba wasichana wanaosoma katika shule  hiyo Novemba mwaka jana.
    Alifafanua kwamba kasi ya kuanguka  kwa wasichana hao  shuleni  hapo  imepungua baada ya kuanza kufanyia kazi ushauri wa Mchungaji Rowse, aliyefika  shuleni hapo na kuzungumza na wanafunzi.  Pia alitoa  semina  kwa wanafunzi, walimu  na wazazi.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.