June 16, 2014

  • askari wawili wapoteza maisha katika ajali chalinze leo



    askari wawili wapoteza maisha katika ajali chalinze leo
    Na John Gagarini, Kibaha 

    WATU wawili wamefariki dunia huku mmoja akijeruhiwa baada ya magari waliyokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso.
     Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa Polisi mkoani Pwani, kamishna Msaidizi mwandamizi wa polisi (SACP) Ulrich Matei  (pichani) amesema kuwa ajali hiyo ilihusisha lori na gari dogo. 
    Kamanda Matei alisema kuwa ajali hiyo ilitokea Juni 16 mwaka huu majira saa 1:15 usiku eneo la Chamakweza kata ya Pera tarafa ya Chalinze wilayani Bagamoyo. 

    Alisema ajali hiyo ilihusisha lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 164 AUS na tela namba T 498 AZ likiendeshwa na Hassan Shaban mkazi wa Dar es Salaam ambaye aligongana na gari aina ya Isuzu Carry lenye namba za usajili Z 190 DR likitokea mkoani Morogoro. 
    "Waliokufa ni dereva wa gari dogo Meja Edward Mosi ambaye ni ofisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kikosi cha Kinonko na mkaguzi Msaidizi wa Polisi wa wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Johnson Zakaria," alisema Matei. 
    Aidha alisema katika ajali hiyo mtu mmoja alijeruhiwa na kukimbizwa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi kwa ajili ya matibabu huku miili hiyo nayo ikiwa hospitalini hapo kusubiri ndugu kwa ajili ya mazishi. 
    "Kutokana na ajali hiyo jeshi la polisi linamtafuta dereva wa lori ambaye alikimbia mara baada ya tukio hilo, ili aweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria," alisema Matei.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.