June 02, 2014

  • Waziri Mkuu Pinda mgeni rasmi mkutano wa mashauriano ya awamu ya kwanza uwekezaji DART leo



    Waziri Mkuu Pinda mgeni rasmi mkutano wa mashauriano ya awamu ya kwanza uwekezaji DART leo
    Waziri Mkuu Mizengo Pinda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa mashauriano ya  uwekezaji wa awamu ya kwanza ya Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) unaoanza leo.

    Mkutano huo wa siku mbili unawakutanisha wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje kwenye kituo cha mikutano Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

    Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi yaendayo haraka Dar es salaam (DART), Bi. Asteria Mlambo, amewaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa mkutano huo wa mashaurino utatoa nafasi kwa wawekezaji kuzijua fursa mbalimbali za uwekezaji zitakazopatikana kwenye mradi huo unaojengwa kwa mabilioni ya pesa.

    "Washiriki wote kwenye mkutano wa majadiliano watapata fursa ya kutembelea eneo la mradi na watapata nafasi ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi wake kuhusu mradi," Bi. Mlambo alisema na kuongeza kuwa mkutano huo ni muhimu sana.

    Akifafanua zaidi, Mtendaji huyo Mkuu alisema   mabenki  na taasisi mbalimbali za kifedha, makampuni ya kutengeneza mabasi, makampuni ya mawasiliano, mifuko ya kijamii na mengineyo mengi yamealikwa kwenye mkutano huo.

    "Mada mbalimbali kuhusu mradi zitatolewa ambapo Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw.Jumanne Sagini atawasilisha mada kuhusu mradi wa DART," alisisitiza.

    Hivi karibuni, Wakala huo uliandaa mkutano ambao uliwakutanisha wamiliki wote wa daladala jijini Dar es Salaam pamoja na Kampuni ya Usafirishaji Dar es Salaam (UDA) na wadau wengine ili kuwafahamisha na kushaurina ni jinsi gani wataweza kunufaika na mfumo mpya wa usafiri jijini Dar es Salaam.

    Katika mkutano huo, wadau hao walielezwa faida na fursa zitakazopatikana kwenye mfumo mpya wa usafirishaji jijini na jinsi wao watakavyoweza kuwa sehemu ya mradi.

    Mwezi April mwaka huu, wakala wa DART ulikamilisha zoezi la kusajili mabasi ya daladala yanayopita katika barabara ya Morogoro au kukatiza katika njia hiyo.
     
    Hatua hiyo ya kuandikisha mabasi hayo ilikuwa moja ya matayarisho ya kupisha mradi huo wa mabasi yaendayo haraka.
     
    Kwa sasa wakala huo uko kwenye mchakato wa kuwezesha upatikanaji wa watoa huduma kwenye mfumo mpya wa mabasi yaendayo haraka awamu ya kwanza ambayo inajumuisha barabara ya Morogoro, Kawawa na mtaa wa Msimbazi kwa njia kuu na nyingine za kiungo. 

    Kulingana na mpango wa uendeshaji wa mfumo wa DART, barabara zinazohusika zitapaswa kutumiwa na mabasi ya mfumo huo pekee.

    Jumla ya njia 64 jijini Dar es Salaam zitakoma kutumika kutokana na kuanza kwa mradi huo.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.