June 20, 2014

  • Tundu Lissu Ailipua Tena Serikali Kwa Kutoa Taarifa za Uongo



    Tundu Lissu Ailipua Tena Serikali Kwa Kutoa Taarifa za Ungo
    Serikali imeumbuliwa bungeni ikidaiwa kuwasilisha taarifa za uongo kupitia Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu ugawaji wa madawati yaliyonunuliwa kwa 'chenji ya rada'.

    Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alitoa tuhuma hizo jana, wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2013/2014, akisema Serikali imewadanganya wabunge kwa kuwa hakuna kitu kilichofanyika.

    Alisema katika majibu ya Serikali kumekuwa na mkanganyiko mkubwa kwa kuwa imetangaza kununua madawati 93,740 na kuyagawa katika halmashauri mbalimbali nchini wakati siyo kweli.

    Alisema kwa mtindo huo, Serikali imelidanganya Bunge pamoja na Watanzania kwa kuwa imetangaza madawati hewa ambayo hayapo.

    "Wabunge kama kweli mnatimiza majukumu yenu na hampo hapa kwa masilahi yenu tu, hebu hojini halmashauri zetu zimepelekewa haya madawati 93,000 yanayozungumzwa humu au mnapiga makofi tu? Serikali inadanganya tunatakiwa tuihoji tuiwajibishe," alisema.

    Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alitoa mfano wa mgawo huo kwenye Halmashauri ya Ikungi, Singida kwamba ilitangazwa kupelekewa madawati 508 lakini amekwenda jimboni na hakukuta dawati hata moja.

    Alisema uchunguzi wake umebaini kuwa hata katika wilaya mbalimbali ikiwamo ya Iringa, hakuna kitu kama hicho.

    "Jana sikuwa hapa bungeni nilikwenda kwenye halmashauri yangu, hakuna dawati hata moja. Hata Halmashauri ya Iringa kwa Mchungaji Msigwa (Peter) hapa ananiambia hakuna dawati hata moja, mnatudanganya ili iweje?" Aliwashauri wabunge wengine kufanya utafiti katika maeneo yao iwapo kuna madawati ambayo yamepelekwa kutokana na fedha zilizorejeshwa na Serikali kama chenji ya rada.

    Lissu alisema ni maneno matupu ambayo yamekuwa yakiwahadaa wabunge na kuwafanya wasahau wajibu wao wa kuisimamia Serikali na kujikuta ni washangiliaji wakati wote. Lissu alisema kinyume na taarifa hizo za Waziri Mkuu, Bunge jana lilikuwa limeelezwa na Naibu Waziri (hakumtaja) kuwa madawati hayo hayajagawanywa.

    Katika kipindi cha maswali na majibu, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Kassim Majaliwa akijibu swali la nyongeza la Ibrahim Sanya (Mji Mkongwe - CUF), kuhusu madawati hayo, alisema kwa kuwa madawati hayo bado yanagawanywa, watakaa na kuangalia utaratibu mzuri wa kuyafikisha Zanzibar.

    Lissu pia alisema fedha ambazo zilitajwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospter Muhongo kuwa ni pato la Watanzania ni uongo kwa kuwa ni mali ya wamiliki wa migodi.

    Alisema takwimu za waziri zimesababisha Watanzania kuamini kuwa wameingiza fedha nyingi ilihali kiasi kilichoingia hakifikii hata asilimia 10 ya pato la wawekezaji.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.