June 19, 2014

  • TFF NA PLAN INTERNATIONAL KUSHIRIKIANA KUHAMASISHA HAKI ZA MTOTO NCHINI



    TFF NA PLAN INTERNATIONAL KUSHIRIKIANA KUHAMASISHA HAKI ZA MTOTO NCHINI
    Rais wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Jamal Malinzi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kuzungumzia ushirikiano wa TFF na Shirika la kutetea haki za watoto la Plan International kwa ajili ya kutetea na kuhamasisha juu ya ulinzi wa haki za mtoto hapa nchini.Hafla hii imefanyika leo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa TFF,jijini Dar es Salaam.Wapili Kulia ni Mkurugenzi wa Plan International Tanzania, Jorgen Haldorsen.Picha na Othman Michuzi.
    Mkuu wa Kampeni ya kutetea na kuhamasisha juu ya ulinzi wa haki za mtoto hapa nchini,Bi. Elena Ahmed akielezea namna kampeni hiyo itakavyoendeshwa kupitia Michezo kwa maeneo mbali mbali hapa nchini wakati Mkutano na waandishi wa habari jijini Dar leo.Kushoto ni Rais wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Jamal Malinzi.
    Rais wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Jamal Malinzi (wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Plan International Tanzania, Jorgen Haldorsen wakisaini mkataba wa makubaliano wa Kampeni ya kutetea na kuhamasisha juu ya ulinzi wa haki za mtoto hapa nchini.Wengine pichani ni Golikipa wa timu ya Taifa (Taifa Stars) ambaye pia ni Balozi wa Kameni hiyo,Deogratius Munish (kulia),Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF,Boniface Wambura (katikati) na Mkuu wa Kampeni ya kutetea na kuhamasisha juu ya ulinzi wa haki za mtoto hapa nchini,Bi. Elena Ahmed (kushoto) wakishuhudia.
    Picha ya pamoja mara baada ya kusainishana mikataba ya makubaliano.

    Wakati mamilioni ya Watanzania wakifuatilia Fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil, Shirika la kutetea haki za watoto la Plan International limeingia ubia na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya kutetea na kuhamasisha juu ya ulinzi wa haki za mtoto hapa nchini.

    Kwa lengo hilo, mkataba wa ushirikiano umesainiwa leo katika ofisi za makao makuu ya TFF jijini Dar es Salaam baina ya Mkurugenzi wa Plan International Tanzania, Jorgen Haldorsen na Rais wa TFF, Jamal Malinzi. Ushirikiano huo unalenga kufanya kazi pamoja katika kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia, ndoa na mimba za utotoni.

    Kwa mujibu wa Haldorsen, mchezo wa mpira ndio unaoongoza nchini na kote duniani kwa kuwa na ushabiki mkubwa na kwamba joto kali juu ya Fainali za Kombe la Dunia linaloendelea Brazil ni ushahidi tosha.

    "Tunatambua uwezo wa mchezo huu wa kuwajumuisha watu. Sasa tunataka tuwajumuishe watu sio tu kwa ajili ya furaha lakini pia kama njia ya kuleta mabadiliko juu ya usawa wa kijinsia kwa kutetea na kuhamasisha juu ya haki za mtoto wa kike," aliongeza.

    Mkurugenzi huyo alidokeza kuwa ushirikiano na TFF ni sehemu ya kampeni ya kimataifa inayoendeshwa na shirika hilo kote ulimwenguni inayoitwa 'Because I Am A Girl'-BIAAG au kwa Kiswahili- KWA SABABU MIMI NI MSICHANA ambayo inalenga kuwatoa mamilioni ya wasichana kutoka katika umaskini kupitia uhamasishaji juu ya haki zao, elimu na stadi za maisha.

    "Kwa kupitia ubia huu tutakuwa na uwezo wa kuwafikia mamilioni ya Watanzania na tutawapa wasichana ujumbe kuwa KWA SABABU MIMI NI MSICHANA, lazima nipate fursa sawa na wavulana. KWA SABABU MIMI NI MSICHANA, lazima niwe na uwezo wa kufunga magoli ya kufikia ndoto zangu katika maisha," Haldorsen alieleza.

    Kwa upande wake, Rais wa TFF, ambaye ni mjumbe katika Kamati ya Huduma kwa Jamii ya Shirikisho   la Mpira wa Miguu Ulimwenguni- FIFA, alisema kuwa ubia huo ni sehemu ya utekelezaji wa sera za huduma kwa jamii ya TFF na kwamba wana furaha kushirikiana na Plan International kwa lengo hili muhimu.

    "Ushirikiano huu ni muhimu sana kwetu kwani unakileta chombo kikubwa kabisa cha michezo hapa nchini pamoja na shirika la Plan International hususan kwa ajili ya haki za mtoto wa kike. Tunategemea kutumia mtandao wetu nchi nzima kuelimisha juu ya usawa wa kijinsia na uhamasishaji wa haki za mtoto wa kike," alisema Rais Malinzi.

    Kwa pamoja tutashughulikia masuala ya usawa wa kijinsia, hususan kupambana na ndoa za utotoni ambazo zinawazuia mamilioni ya watoto wa kike nchini wasiweze kumaliza shule, kufikia ndoto zao katika maisha, na vile vile kuwaacha waendelee kuteseka katika umaskini," Rais Malinzi aliongeza.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.