May 23, 2014

  • RAIA WAWILI WA ROMANIA KOTINI KWA KUIHUJUMU TCRA

     
     
     


    Na Mwene Said wa Blogu ya Jamii, Mahakamani
     
     
    WATU wawili raia wa Romania wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi ikiwemo udanganyifu,kutumia kadi zisizosajiliwa, kuingiza nchini na kutumia mitambo ya simu bila kibali, kutoa huduma ya mawasiliano ya kimataifa bila kibali cha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kuisababishia hasara ya Sh. Bilioni 2.1 Mamlaya ya Mawasiano Tanzania (TCRA).
     
    Washtakiwa hao ni, Meneja wa Kampuni ya Razvan Pimtilie (47) na Robart Kraus (27) wakazi wa Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam na walisomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mfawidhi, Isaya Arufani.
     
    Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka akisaidiana na Mwanasheria Mkuu wa TCRA, Joannes Karungura na Inspekta wa Polisi, Jackson Kinunda.
     
    Kweka alidai kuwa alidai shitaka la kwanza, kati ya Aprili na Mei, mwaka huu huko Raha Data Centre, eneo la Banda la Ngozi, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, bila halali na kwa makusudi washtakiwa wakiwa na nia ya kukwepa malipo halali walitoa huduma ya mawasiliano ya kimataifa bila leseni ya TCRA.
     
    Shitaka la pili, ilidaiwa kuwa siku na tarehe za tukio la kwanza, washtakiwa walitoa huduma za simu za kimataifa bila kuwa na leseni ya TCRA.
     
    Upande huo wa Jamhuri uliendelea kudai kuwa, shitaka la tatu, siku na tarehe isiyofahamika washtakiwa waliingiza nchini mitambo ya elektroniki bila leseni ya TCRA.
     
     
    Wakili huyo Mwandamizi alidai katika shitaka la nne kuwa, siku na mahali pasipofahamika jijini Dar es Salaam, washtakiwa waliingiza nchini mitambo ya elektroniki bila leseni ya TCRA.
     
    Katika shitaka la tano, ilidaiwa kati ya Aprili na Mei, mwaka huu huko Banda la Ngozi, jijini, kwa nia ovu na kwa makusudi, washtakiwa alitumia kadi za simu zenye namba nne tofauti zisizokuwakuwa na usajili wa TCRA.
     
    Ilidaiwa katika shitaka la sita, Aprili mwaka huu jijini Dar es Salaam, mshtakiwa wa kwanza (Pintilie), akiwa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Xplora Ltd, alisajili namba za simu mbili tofauti kutoka Kampuni ya Zantel (T) Ltd na kuzihamishia Global COM bila leseni.
     
    Kweka alidai katika shitaka la saba, kwamba kati ya Aprili na Mei, mwaka huu huko Banda la Ngozi, jijini, washtakiwa wakiwa hawana  leseni ya kuwaruhusu kufanya huduma za mawasiliano alichepusha simu za kimataifa na kuisababishia Serikali na TCRA hasara ya Sh. 2,109,888,000.
     
     
    Kwa mujibu wa sheria ya uhujumu uchumi, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote, kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi hadi upelelezi utakapokamilika kesi hiyo itahamishiwa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
     
    Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika.
     
    Hakimu Arufani alisema kesi hiyo itatajwa Mei 27, mwaka huu na washtakiwa warudishwe rumande.
  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.