Na Nathaniel Limu, Babati
WAKALA wa Mbegu za Kilimo wa Taifa (ASA)
umejiwekea mikakati madhubuti ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2015, uzalishaji wa
mchele nchini uwe umefikia tani 1.5 milioni ili kutekeleza agizo alilotoa Rais
Jakaya Kikwete.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Meneja Masoko
na Usambazaji ASA,Philemon Kawamala kwa nyakati tofauti wakati akikagua mashamba
darasa ya mazao ya alizeti,mtama,uwele,mahindi,mpunga wa mabondeni na ule wa
mpunga mpya ambao unalimwa kwenye ardhi ya nyanda za juu.
Akifafanua,amesema mpunga huo mpya ambao
unalimwa kwenye ardhi inayolimwa mazao mengine ya kawaida kama mahindi na
uwele,ni new rice for Africa (NERICA),mbegu zake ni za aina ya Nerica 1,2,4 na
7, pia kuna aina nyingine ambayo ni WAB 450.
“Kwa mara ya kwanza mpunga huo mpya umepandwa
katika mikoa ya Dodoma,Morogoro,Singida,Manyara,Tabora,Simiyu.Kagera,Shinyanga
na Geita.
Aina hizi za mpunga zinapandwa katika maeneo
ya nyanda za juu (nchi kavu) hususan maeneo yanayolimwa mazao kama
mahindi”,alifafanua zaidi Kawamala.
Amesema ujio wa mpunga huo pamoja na mchele
uliozoeleka wa mabondeni kwa vyovyote endapo hali ya hewa na mvua zitaendelea
kunyesha vizuri basi agizo la Rais Kikwete la kutaka nchi kuzalisha tani 1.5
milioni mwakani litafikiwa na pengine na kuzidi hapo.
Kawamala amesema pamoja na mbegu hizo za
mpunga mpya,ASA ina aina nyingi za mbegu bora zikiwemo za mazao ya mahindi na
mtama ambazo zinakomaa kwa muda mfupi na mazao yake ni mengi ilikilinganishwa na
mbegu za asili.
“Kwa sasa kwa kutumia mashamba darasa
yanayosimamiwa na wakulima viongozi,wakulima wamepanda mbegu hizo kwa lengo la
kuwapa fursa wakulima kuchagua aina ya mbegu watakazozipenda zaidi ili
uzalishaji wake uongezwe kadri ya mahitaji yao”amesema na kuongeza;
“Nimefarijika mno kuona wakulima viongozi
wamefanya kazi nzuri msimu huu kwa mazao ya alizeti,mahindi,mpunga wa mabonde ya
umwagiliaji,majaruba na huu mpya uliolimwa kwenye nyanda za juu”.
Kwa upande wao wakulima viongozi,wameupongeza
ASA, kwa madai kwamba mbegu zake zitasaidia kuondoa kabisa uhaba wa chakula na
wakati huo huo kuongeza kipato cha mkulima.
“Mbegu kutoka ASA zimeonyesha dhahiri
zitasaidia Tanzania kujitosheleza kwa chakula na kwa sababu zinatoa mazao mengi
ikilinganishwa na mbegu za asili,mazao ya ziada yatakayopatikana yatasaidia
kumkomboa mkulima kiuchumi”,amesema mkulima kiongozi wa kijiji cha Orongadida
kata ya Qash.
Naye Simon Lohay wa kijiji cha Mwakantisi kata
ya Mamire,amesema mpunga mpya unaolimwa kwenye ardhi isiyo na maji sambamba na
mazao ya mtama na mahindi umevutia wakulima wengi na msimu ujao wakulima karibu
wote wameonyesha nia ya kuulima.
0 comments:
Post a Comment