May 19, 2014

  • TWANGA YAANDAA USIKU WA MWANA DAR ES SALAAM … Chaz Baba, Chokoraa, Rogart Hegga, Diouf, Amigo wote ndani ya nyumba

     
     
     
     
    TWANGA YAANDAA USIKU WA MWANA DAR ES SALAAM … Chaz Baba, Chokoraa, Rogart Hegga, Diouf, Amigo wote ndani ya nyumba

    BENDI ya The African Stars "Twanga Pepeta" inatarajiwa kufanya onyesho kubwa la "Usiku wa Mwana Dar es Salaam" litakalofanyika baadae mwezi ujao.

    Kiongozi wa bendi hiyo, Luizer Mbutu alisema Jumapili usiku kuwa onyesho la Mwana Dar es Salaam litafanyika Jumamosi 21, Juni ndani ya Mango Garden Kinondoni.

    Mwana Dar es Salaam ni moja kati ya albam za Twanga Pepeta, zilizopata mafanikio makubwa.

    Albam hiyo ilizinduliwa Diamond Jubilee, Jumamosi ya tarehe 6 Juni mwaka 2009 ambapo mgeni rasmi alikuwa Mgeni rasmi Waziri wa Ofisi ya Rais Utawala Bora, Bi Sophia Simba.

    Akiongea mbele ya mashabiki waliohudhuria onyesho la Twanga Jumapili ndani ya Leaders Club, Luizer alisema tayari maandalizi ya onyesho hilo la aina yake, yameanza.

    Lakini kubwa zaidi, Luizer akajinasibu kuwa waimbaji wote walioshiriki albam hiyo wakiwemo wale ambao hawako tena kundini, watakuwepo katika onyesho hilo.

    "Siku hiyo atakuwepo Chaz Baba (Kutoka Mashujaa Band), Khalid Chokoraa (Mapacha Watatu), Rogart Hegga, Amigolas na Msafiri Diouf (Ruvu Stars), watakuwepo Mango Garden," alisema Luizer.

    Kiongozi huyo wa Twanga Pepeta akasema mbali na waimbaji, pia wapiga hala pamoja na madansa kama Aisha Madinda, Lilian Internate, Super Nyamwela, Bokilo na wengineo walioshiriki albam hiyo nao watakuwepo.

    Saluti5 inaamini kuwa kama kweli Twanga itafanikiwa kuwakusanya nyota wote hao, basi hakika litakuwa ni onyesho la kukumbukwa.

    Lakini swali kubwa linabaki wazi: Ni rahisi kuwapata wanamuziki wote hao kwa wakati mmoja hasa kwa kuzingatia kuwa karibu wote hao ni waajiriwa katika 'ofisi' zingine na wanamajuku yao ya kila weekend kumtumikia mwajiri wao? …Ni jambo la kusubiri.

  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.