July 18, 2014

  • WAZIRI WA MAZINGIRA AKIPA ONYO KIWANDA CHA NIDA


    WAZIRI WA MAZINGIRA AKIPA ONYO KIWANDA CHA NIDA
    DSC_0054Jengo la kiwanda cha NIDA likionekana kwa nje
    Winner Abraham-MAELEZO
    WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk. Mhandisi Binilith Mahenge ametoa onyo kwa kiwanda cha NIDA Textile Mills Ltd, kutokana na kutititirisha maji yasiyo salama kwa mazingira na afya ya wakazi wa eneo la kiwanda hicho.Waziri Mahenge alitoa onyo hilo wakati alipotembelea kukagua kiwanda hicho kilichopo Kigogo Mkuyuni jijini Dar es Salaam, baada ya kupata taarifa kuwa kiwanda hicho kinatiririsha maji machafu yanayoathiri mazingira.Awali kiwanda hicho kiliomba cheti cha usafi wa mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) na Waziri huyo aliombwa kutia saini cheti hicho ili kuthibitisha usafi wa kiwanda hicho.Hata hivyo, Wazari Dk Mahenge alikuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya NIDA kukiuka taratibu za usafi kwa kutiririsha maji machafu yanayowaathiri wananchi.Waziri pamoja na timu yake akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, alifanya ukaguzi wa kustukiza kwenye kiwanda hicho na kukuta kikitiririsha maji yasiyo salama kwenye mto Kibangu unaopita maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.Hata hivyo, baada ya Waziri na timu yake kuingia kiwandani hapo, walitembelea maeneo mbalimbali ya kiwanda hicho na baadaye aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kwenda kujionea maji machafu yanayotoka kiwandani humo.

    Kwa mshangao mkubwa, Waziri pamoja na timu yake walikuta maji yaliyokuwa yakitiririshwa ni tofauti na yale waliyoyashuhudia awali wakati walipokagua kabla.
    "La kwanza ambalo ninataka Watanzania walifahamu ni kwamba tunataka sana wawekezaji na Serikali imeweka mazingira mazuri sana kuvutia wawekezaji, lakini mwekezaji mzuri atakuwa ni yule tu anayejali mazingira" alisema Waziri Dk. Mahenge na kuongeza:
    "Ukiona kinachofanyika hapa ni kama vile mwekezaji anajali cha kwake hajali maisha ya Watanzania….mimi kwangu nimepewa malalamiko ofisini karibu mara nne, tulipita mara kwanza na sasa tumeona haya, maana yake ni kama wenzetu hawa wanaidanganya sekta ya uwekezaji"
    Alisema kuwa walidhani ili wapate ushirikiano mzuri ni lazima wajali mazingira ya mto huo hutumiwa kupandwa mbogamboga, watoto wadogo wanavuka humo, hivyo wakipata kemikali hizo watapata madhara makubwa sana.
    "Maji tuliyoyakuta asubuhi sio haya ambayo mmeenda kuyafungua sasa hivi, maana yake mitambo nyinyi mnayo isipokuwa ama kwa gharama zenu mnazoogopa au umeme au nini hamfungulii, vilevile mnaonekana hamuwajali Watanzania" alisema Waziri Dk. Mahenge.
    Alibainisha kuwa kwa mtindo huo hawawezi kupewa cheti cha usafi wa mazingira kama hatapata uhakika kwamba maji yataendelea kuwa mazuri kwa muda wote huku akinoesha hofu kuwa iwapo watapewa cheti wataendelea kudanganya Watanzania.
    Afisa Tawala wa kiwanda hicho Mohamed Honelo aliahidi kuwa watafanya marekebisho na kuweka mazingira katika hali ya usafi kwa muda wote na kuomba radhi kwa Serikali kutokana na hali hiyo.
    Naye Mkurugenzi Mkuu wa   NEMC Bonaventure Baya   alisema wanajipanga kuhakikisha kuwa wanaweka utaratibu wa kuhakikisha kuwa kiwanda hicho kinazingatia masharti ya usafi wa mazingira kwa muda wote.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.