Dodoma. Mbunge wa viti   maalumu kwa tiketi ya CUF, Amina Abdallah Amour amemjia juu katibu wa itikadi na   uenezi wa CCM, Nape Nnauye kwa kuufananisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)   na kundi la Boko Haramu na kutaka alaaniwe.
Ukawa iliundwa wakati wa   Bunge Maalumu la Katiba na unahusisha wajumbe kutoka vyama vya NCCR-Mageuzi,   Chadema na CUF.(Martha Mageesa)
Akizungumza bungeni   mjini Dodoma juzi, mbunge huyo alisema kauli ya Nnauye ni ya uchochezi na   inapaswa kulaaniwa.
  Mbunge huyo alikuwa   akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Wanawake,   Jinsia na Watoto kwa mwaka 2014/2015 iliyowasilishwa na waziri wake, Sophia   Simba.
  "Gazeti la Uhuru (jana)   lilimnukuu Nape Nnauye akisema Ukawa ni sawa na Boko Haramu... Hii ni kauli   chafu na ya uchochezi. Haikubaliki na ninailaani kwa nguvu zangu zote,"   alisema.
  Mbunge huyo alihoji   "wazazi wao hawajui watoto wao wanaishije, wanakula nini wala wanalala vipi....   Leo hii Nape Nnauye amethubutu kusema Ukawa ni sawa na Boko   Haramu?"
  Hata hivyo, wakati   akihoji hivyo, baadhi ya Wabunge wa CCM nao walisikika wakihoji "na Intarahamwe   Je?".
  Ukawa ilitumia jina hilo   la Interahamwe wakati mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akitangaza   uamuzi wa kundi hilo kujitoa kwenye Bunge la Katiba, akiifananisha CCM na kundi   hilo la nchini Rwanda.
  Katika gazeti hilo,   Nnauye amenukuliwa akisema Ukawa ni kundi hatari linaloeneza chuki na kusambaza   uongo kwa Wananchi kwa nia ya kuwagawa na kusema silaha wanazotumia ni zaidi ya   Boko Haramu.
  Nnauye anadaiwa kutoa   kauli hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika mkoani Tabora, akisema silaha   za uongo wanazotumia viongozi wa Ukawa ni hatari zaidi kuliko silaha za moto   zinazotumiwa na Boko Haramu.
  Viongozi wa CCM na wale   wa Ukawa wamekuwa wakizunguka nchi nzima kufanya mikutano ya hadhara kufafanua   kile kilichojitokeza ndani ya Bunge la Katiba na kusababisha Ukawa kususia Bunge   hilo.
  CHANZO:MWANANCHI

0 comments:
Post a Comment