Mtoto Samwel Paulo akiwa   hospital baada ya kufanyiwa kitendo cha kinyama na mama yake   mzazi.
  Dunia   haina huruma! Mtoto Samwel Paulo (13), anayesoma darasa la nne Shule ya Msingi   Amani wilayani Ilala, Dar, amelazwa wodi ya watoto katika Hospitali ya Taifa ya   Muhimbili, akiendelea kuuguza majeraha yaliyotokana na kile kinachodaiwa ni   kulipuliwa kwa moto na mama yake mzazi aliyetajwa kwa jina la Doricus Iganga.   Tukio hilo la   kusikitisha lilitokea nyumbani kwao maeneo ya Mombasa Gongo la Mboto, Dar   mwishoni mwa wiki iliyopita, saa 8:00 usiku ambapo mwandishi wa habari hii   alimtembelea wodini hapo.
"Najisikia vibaya sana   kutokana na maumivu makali ya moto. Sikutegemea kama mama yangu mzazi   angenifanyia hivi kwa kunituhumu kuwa nimemuibia fedha zake shilingi elfu   kumi.
"Amekatisha ndoto yangu   ya masomo, kwa sasa wenzangu wanajiandaa na mtihani wa muhula, mimi nipo wodini   (huku akiangua kilio).
"Matukio kama haya huwa   nimekuwa nikiyasikia yakifanywa kwa watoto wenzangu kutoka kwa mama wa kambo na   siyo kwa mama mzazi kama ilivyotokea kwangu.
  "Kwa hali hii hakuna mtu   anayeweza kunionea huruma kama mzazi wangu hana uchungu na mimi.
"Sitegemei kuendelea   kuishi na mama endapo Mungu akinisaidia nikapona.
  "Ninachokikumbuka ni kwamba siku hiyo   nilitoka shule, ilipofika saa 12:00 jioni, mama akawa amerudi kutoka katika   kibarua chake.
"Alitupatia fedha ya   kununua chipsi kwa sababu alikuwa anaondoka kwenda kwenye shughuli yake nyingine   ya kuuza chakula maeneo ya Ukonga-Mazizini.
  "Aliporudi usiku, mimi na   mdogo wangu Salim Paulo (10), tulikuwa tumeshalala.
"Nakumbuka ilikuwa saa   8:00 usiku, mama alituamsha akawa anasema mimi na mdogo wangu tumemuibia fedha   hasa mimi.
"Nilimkatalia kwamba   sijachukua wala sikujua alipoiweka, hakunisikiliza, alichukua mafuta ya taa na   kunimwagia kisha akanilipua na kutokomea kusikojulikana.
  "Mdogo wangu alichukua   maji kwenye ndoo na kunimwagia hadi moto ukazimika.
"Niliungua vibaya sana.   Baada ya muda mfupi alirudi akijifanya yeye hahusiki, niliishiwa nguvu,   nilipoteza fahamu.
"Nilikuja kujitambua   nikiwa hospitalini Amana. Hali ilikuwa mbaya ndipo nikaletwa hapa Muhimbili na   ninauguzwa na bibi yangu baada ya mama kukamatwa na polisi.
"Nawashukuru sana   madaktari na wauguzi kwa kunihudumia kwa karibu.
Naona mabadiliko kidogo   ingawa tumbo linaniuma kwa ndani," alisema mtoto huyo kwa masikitiko   makubwa.
  Kwa upande wake, bibi yake,   Helen Barnaba anayemuuguza mtoto huyo baada ya mama yake kukamatwa na polisi   alikuwa na haya ya kusema:
"Nikiwa kwangu Igunga,   Tabora, nilipigiwa simu kuwa mjukuu wangu kaunguzwa moto, nilizimia,   nilipozinduka nikaanza maandalizi ya kuja Dar.
  "Nilipofika na kukuta   hali kama hii, sikuamini kama mwanangu angeweza kufanya jambo kama   hili.
"Hata hivyo, hii siyo   bure bali ni mzunguko wa shetani, hawa wajukuu nilikuwa nikiishi nao kwa muda   mrefu hadi pale nilipougua, nikamwambia mama yao   awachukue."
Mtoto huyo kwa sasa yupo   hospitalini akiendelea na matibabu huku mama yake mzazi akishikiliwa kwenye   Kituo cha Polisi cha Sitaki-Shari, Dar kwa upelelezi ili sheria ichukue mkondo   wake.
  Kwa yeyote atakayeguswa na   kisa cha mtoto Samwel, anaweza kufika katika wodi hiyo ya watoto au kuwasiliana   na bibi yake anayemuuguza kwa namba 0762 389774. Pia anaweza kumpatia msaada wa   fedha kwa namba hiyo, tunamuombea mtoto huyo apone ili akajiunge na wanafunzi   wenzake katika masomo.
0 comments:
Post a Comment