Na Baraka Mbolembole
Leo, ndiyo siku ya hukumu! Katika uwanja wa Estadio da Luiz, jijini, Lisbon, Ureno wakati miamba ya soka nchini Hispania itakapokuwa ikiwania taji la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Ni fainali ya kwanza baada ya miaka 14 timu za Hispania kukutana katika mchezo wa fainali wa michuano hiyo mikubwa na yenye mvuto mkubwa barani ulaya kwa ngazi ya klabu. Real, iliichapa Valencia kwa magoli 3-0, mwaka 2000 katika fainali ya mwisho kuhusisha klabu za Hispania.
Atletico, kwa upande wao wamekuwa na msimu wa kuvutia. Wametwaa taji la LaLiga, wiki iliyopita, na wanaweza kutwaa taji lao la pili kubwa msimu huu kama watafunga ' msimu wa ulaya' kwa kuwanyuka mahasimu wao wa jiji la Madrid, usiku wa leo.
Bjorn Kuipers, raia huyu wa Uholanzi mwenye miaka 41 atachezesha pambano hilo ambalo kwa mara ya kwanza litahusisha timu za mji mmoja, akiwa na rekodi ya kutoa kadi nyekundu mbili, na njano 16 katika michezo tofauti aliyocheza msimu katika michuano, Kuipers itambidi kuwa ngangari kuchezesha wachezaji ' wababe-wachapa viatu' wa timu zote mbili. XABI ALONSO kiungo huyo wa kimataifa wa Hispania hatakuwepo katika mchezo wa leo, hivyo kocha, Carlo Ancelotti anataraji kumuanzisha kiungo, Mjerumani, Sami Khedira ambaye alicheza kwa nusu ya mchezo wa mwisho wa timu yake katika ligi kuu. Alonso, alikuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Real, atakosa mchezo huo kwa kuwa anatumikia adhabu ya kadi mbili za njano ambazo alizipata katika michezo ya nusu fainali dhidi ya Bayern Munich.
Luka Modric na Angel Di Maria wanataraji kuanza na Khedira na kikosi hicho cha ' watu watatu' kinaweza kujikuta katika wakati mgumu dhidi ya timu ya Diego Simeone ambayo imekuwa ikiwachezesha viungo wa nne hadi watano katikati ya uwanja. Koke, Thiago Mendes, ArdaTuran, ni wachezaji wagumu uwanjani, wanakaba kwa nguvu hadi hatua ya mwisho, wanachezesha timu na kuzuia kwa pamoja, na siri kubwa ya mafanikio ya timu hiyo msimu huu ni kucheza kwa ushirikiano, huku wachezaji wote wakiwa na majukumu sawa. Ni tofauti na Real ambayo imekuwa timu inayotegemea zaidi uwepo wa Cristiano Ronaldo na kiwango cha Mreno huyo katika mchezo wa leo ndicho kinaweza kuamua kama mabingwa hao mara tisa wa kihistoria kutwaa ubingwa wao wa kwanza baada ya miaka 11.
Katika muda wa miaka miwili, timu hizo zimekutana mara sita katika michuano tofauti. Real iliifunga, Atletico kwa magoli 2-1 , april, mwaka jana katika uwanja wa Vicente Calderon, na mara ya mwisho kwa kikosi cha Simeone kuwashinda mahasimu wao ni katika mchezo wa kwanza wa msimu uliomalizika, mwezi, septemba walipoilaza, Real kwa goli 1-0, pale Santiago Bernabeu. Timu hizo zimekutana mara nne msimu huu. Tarehe 5, februari, Real iliichapa, Atletico kwa magoli 3-0 katika nusu fainali ya Copa del Rey, na wakawatandika tena magoli 2-0 katika nusu fainali ya pili na kutinga fainali ambayo walitwaa ubingwa. Atletico haijaifunga, Real katika michezo mitatu ya mwisho walipoteza mchezo mmoja na kulazimisha suluhu mchezo mmoja katika michezo miwili ya La Liga. Hivyo, Real wanaweza kujiamini kupita kiasi na kujikuta wakishindwa kutimiza lengo la kutwaa, ' La Decima'.
Kufikia hatua ya fainali, Atletico haijapoteza mchezo wowote kati ya 12 waliyocheza katika michuano hiyo msimu huu, wakati Real walipoteza dhidi ya Borussia Dortimund kwa magoli 2-0 katika mchezo wa pili wa hatua ya robo fainali ambao nyota wake, C. Ronaldo hakuwepo uwanjani. Kikosi cha Simeone kimefunga magoli manne tu dhidi ya mahasimu wao wa Madrid katika michezo sita ya mwisho wakati Real imetikisa nyavu za wapinzani wao mara tisa. Kitu kinaweza kutokea leo? Inaweza kuwa fainali nzuri na yenye magoli mengi kama ilivyokuwa miaka 10 iliyopita wakati timu za FC Port na AS Monaco zilipocheza fainali' isiyotarajiwa'na Monaco walilala kwa magoli 3-0, au inaweza kuwa fainali ngumu na ya kuvutia kama ile ya Mocsow, 2008 wakati mshindi alipopatikana baada ya dakika 120 kwa timu za England, Manchester United na Chelsea kukutana fainali, au inaweza kuwa fainali ya kusisimua kama ile ya Liverpool na AC Milan, 2005.
Hii ni mechi ya fainali, hivyo si rahisi kutabiri mshindi wake. Atletico wanashambulia kuanzia nyuma huku wakisogea mbele kwa uangalifu mkubwa, hawafunguki sana uwanjani dhidi ya timu kali na hiyo ndiyo imekuwa sababu ya wao kuzishinda, FC Barcelona na Chelsea katika hatua za robo na nusu fainali. Walifunguka dhidi ya Milan na waliweza kuitoa timu hiyo ya Italia kwa jumla ya magoli 4-1 Katika hatua ya 16, lakini kukutana kwao na ' BBC' iliyo katika mwendo kasi inaweza kuwa tabu kwao. Walifungwa magoli matano katika michezo miwili ya robo fainali mwezi February katika kombe la Mfalme ila bado silaha yao muhimu' ya kujilinda' inaweza kuwasaidia kunyanyua kikombe cha nne cha ulaya ndani ya miaka minne.
Washindi hao wa ligi ya ulaya miaka ya 2010 na 2012, na taji la Uefa Super Cup wamekuwa na mafanikio makubwa katika michuano ya ulaya katika miaka ya karibuni, tofauti na wapinzani wao ambao wamefuzu fainali ya kwanza baada ya miaka 11. Real iliifunga, Bayer 04 Leverkusen ya Ujerumani katika mchezo wa fainali mwaka 2002 na timu imefuzu fainali msimu huu baada ya kukwama mara tatu mfululizo katika hatua ya nusu fainali. Tamaa yao ya ubingwa wa' kumi' inaweza kumalizwa na timu inayosaka taji la kwanza usiku wa leo.
Real humaliza mechi kwa kushambulia kwa kasi ikitokea kulia mwa uwanja, upande wa kushoto na wakati mwingi wakishambulia na kufunga wakitokea katikati ya uwanja. Gareth Bale, alifunga goli la ' ajabu'katika mchezo wa fainali wa kombe la mfalme dhidi ya Barcelona, machi mwaka huu, kocha, Carlo humtumia mchezaji huyo katika kuvuruga mbinu za kijilinda za mabeki wa timu pinzani kitu ambacho kimekuwa na mafanikio makubwa hata dhidi ya wapinzani wao wa mchezo wa leo. Karimu Benzema amekuwa mfungaji' huru'na mchezaji anayefunga magoli muhimu. Wakati, Ronaldo ni silaha ya hatari katika mashambulizi ya kushtukiza. Je, mbinu hiyo inaweza kufanya kazi katika mchezo wa leo?
Kama, Atletico watapata goli la mapema, mechi inaweza kuwa ngumu kwa Real, na endapo Real wataanza kufunga mambo yanaweza kugeuka na kuwa fainali ya magoli mengi. Atletico huwa wakicheza kwa kujihami sana mara wanapopata goli la kuongoza, kitu ambacho kimekuwa na mafanikio makubwa kutokana na wachezaji wote kucheza kwa lengo la kulinda ushindi. Ni vigumu kusawazisha goli dhidi ya timu hiyo, ila wana uwezo wa kurudi uwanjani na kufuta matokeo mabaya wanapokuwa nyuma dhidi ya wapinzani wao. Fainali haina mwenyewe, ila kuna historia itaandi kwa leo, iwe ni kwa upande wa makocha au klabu. Simeone anasaka taji lake la kwanza wakati, Carlo anasaka taji la tatu kiufundishaji. Real wanasaka taji la kumi' La Decima' wakati Atletico wanasaka taji la kwanza la mabingwa wa Ulaya. Nani mshindi? Mimi sijui!
0 comments:
Post a Comment