October 17, 2015

  • CCM Na Chadema Watwangana Ngumi....Wachoma Moto Maduka,Pikipiki na Magari



    CCM Na Chadema Watwangana Ngumi....Wachoma Moto Maduka,Pikipiki na Magari
     
    Zikiwa zimebakia siku saba kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu, hali ni tete katika Kijiji cha Nyamiyaga, Kata ya Bugomora wilayani Kyerwa, Mkoa wa Kagera baada ya wafuasi wanaodaiwa kuwa wa vyama vya CCM na Chadema kupigana kisha kuharibu magari, pikipiki na kuchoma moto maduka.
     
    Tukio hilo lililotokea Jumatano kuanzia saa 12.00 jioni hadi saa 4:00 usiku, chanzo kikielezwa kuwa ni baada ya misafara ya wagombea udiwani wa kata hiyo kukutana eneo la Stesheni ya Nyamiyaga na wafuasi wao kuanza kurushiana maneno. 
      
    Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyamiyaga, Ferdinand Bashasha ambaye pia ni Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Bugomora, alisema wafuasi wa CCM walikuwa kwenye stesheni hiyo wakiendelea na kampeni zao, huku wakipiga muziki, wenzao wa Chadema walifika eneo hilo ambalo pia kuna saluni ya mgombea wao wanayoitumia kama ofisi.
     
    Kwa mujibu wa ofisa mtendaji huyo walipofika walianza kurushiana maneno na Bashasha aliingilia kati kuzima muziki wakati huo pamoja na kuwasuluhisha.
     
    Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyamiyaga, Hilalius Yustad alisema hali tete katika eneo hilo ilianza tangu uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa sababu wapo baadhi ya watu hawaamini mpaka sasa kuwa yeye ndiye mwenyekiti.
     
    Magari mawili, maduka matatu na pikipiki mbili viliteketezwa moto, huku pikipiki moja ikiwa haijulikani ilipo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Ollomi Augustine alisema watu 20 wamekamatwa kwa mahojiano.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.