September 04, 2014

  • TANZANITEONE KUTOA AJIRA ZAIDI KWA WAZAWA



    TANZANITEONE KUTOA AJIRA ZAIDI KWA WAZAWA
    cutting tanzanite                    tanzaniteoneNa Greyson Mwase, Manyara
    Imeelezwa kuwa katika   kuhakikisha kuwa wataalamu wa kitanzania wananufaika katika soko la ajira kupitia mgodi wa uchimbaji wa madini ya vito aina ya tanzanite wa Tanzanite One, mgodi huo umeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa unaajiri wataalamu wa kitanzania zaidi badala ya kuingia gharama ya kuajiri wataalamu kutoka nje ya nchi.Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa mgodi huo Bw. Farai Manyemba mbele ya timu ya majaji wanaoendesha zoezi la kumtafuta mshindi wa Tuzo ya Rais ya Huduma za Jamii na Uwezeshaji ilipofanya ziara kwenye mgodi huo.Bw. Manyemba alisema kuwa mgodi huo unaomilikiwa kwa asilimia hamsini kwa hamsini kati ya TanzaniteOne na Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) umeanza kuajiri vijana wa kitanzania na kusisitiza kuwa mgodi huo utaendelea na mkakati wa kuhakikisha kuwa wataalamu wenye taaluma na uwezo mkubwa wanaajiriwa katika mgodi huo na kupunguzia Serikali ghrama ya kuajiri wataalamu kutoka nje ya nchi.

    " Ugunduzi wa madini umepelekea sekta ya madini nchini kukua kwa kasi kubwa sana, wawekezaji wanaongezeka kila kukicha, hivyo ni jukumu letu kama kampuni ya madini ya vito kuhakikisha kuwa vijana wa kitanzania wenye uwezo mkubwa kutoka vyuo vyetu nchini wanaajiriwa ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo," alisema Bw. Manyemba
    Aliendelea kusema kuwa katika kuhakikisha kuwa sekta ya madini inachangia ipasavyo kwenye pato la taifa nchi zilizoendelea zimewekeza kwa kuwasomesha wataalamu wake katika masuala ya madini ambapo wataalamu hao wamekuwa na mchango mkubwa.
    Alisisitiza kuwa nchi zilizoendelea zimewekeza katika teknolojia ambayo imeziwezesha kupiga hatua katika sekta hiyo na kuongeza kuwa mtaji mkubwa wa fedha unahitajika ili kukuza sekta ya madini.
    Akizungumzia juu ya mchango wa makampuni ya madini katika kuongeza pato la taifa Bw. Manyemba alisema kuwa iwapo makampuni yote ya madini nchini yatasimamia vyema sheria na kanuni za madini pamoja na mapato yake, sekta hiyo ina uwezo mkubwa wa kuiwezesha nchi kupiga hatua kubwa kimaendeleo.
    Akielezea mchango wa mgodi huo katika huduma za jamii Bw. Manyemba alisema kuwa kwa kipindi cha mwaka 2013 kampuni yake ilitoa ufadhili kwa wanafunzi 11 kutoka katika familia maskini kusoma katika shule za sekondari za Msitu wa Tembo, Terrari, Naisinyai na Benjamin William Mkapa zilizopo katika mkoa wa Manyara.
    Bw. Manyemba aliainisha michango mingine kuwa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha polisi cha Naisinyai kilichopo Manyara ambapo ujenzi wake uligharimu dola za Marekani 37,500
    Aliongeza kuwa mgodi pia ulifadhili kikundi cha wakinamama wa kimasai kijulikanacho kama Ebeneza kwa ajili ya mradi wa kutengeneza urembo na mapambo mbalimbali.
    "Pamoja na kufadhili kikundi cha Ebeneza, tumekuwa tukitangaza bidhaa zake katika masoko mbalimbali nchini Marekani." Alisisitiza Bw. Manyemba
    Bw. Manyemba alitaja michango mingine ni pamoja na kuanzisha kampeni ya kupanda mlima Kilimanjaro ili kuchangia kituo cha watoto yatima cha New Vision kilichopo Mirerani ambapo kiasi za Dola za Marekani 34,000 zilipatikana.
    Aliongeza kuwa katika kukabiliana na mafuriko ambayo hutokea katika kipindi cha masika kampuni ya TanzaniteOne ilijenga ukingo katika eneo la Naisinyai ambalo ndilo eneo linaloathirika na mafuriko wakati wa mvua.
    Akizungumzia changamoto katika kampuni hiyo Bw. Manyemba alisema kuwa ni pamoja na wachimbaji wadogo wasio waaminifu kutorosha tanzanite na kwenda kuuza nchi za jirani kama Kenya.
    Alitaja changamoto nyigine kuwa ni pamoja na uvamizi kwenye mgodi huo uliosababisha hasara ya dola za Marekani milioni tano kutokana na mali za kampuni kuharibiwa, mauaji ya wafanyakazi na kuongeza kuwa kwa sasa mgodi umeimarisha ulinzi katika kila eneo.
    Akielezea mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo Bw. Manyemba alisema kuwa mgodi utaendelea kutoa elimu kwa jamii inayouzunguka hususan wachimbaji wadogo, kujenga mahusiano mazuri kwa jamii pamoja na kuimarisha ulinzi kila eneo la mgodi.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.