May 17, 2014

  • HATARI!!! GONJWA JINGINE LAIBUKA

     
     
     
     
    Mbu wa Aedes aegypti anayesambaza gonjwa hatari la Chikungunya pamoja na homa ya Dengue.
    Majanga! Huku hali ya sintofahamu ikiendelea kuwakumba wakazi wengi wa Jiji la Dar es Salaam na nchi nzima kufuatia kuzuka kwa ugonjwa wa homa ya Dengue, gonjwa lingine hatari lisilo na chanjo wala tiba limezuka, Risasi Jumamosi linakuwa la kwanza kukujuza.
    Gonjwa hilo liitwalo Chikungunya, linasambazwa na virusi wa jamii ya 'Alphavirus' ambao huingia kwenye mwili wa binadamu endapo mtu ataumwa na mbu wa Aedes aegypti (wanaosambaza homa ya Dengue).
    Kwa kawaida, mbu wanaobeba ugonjwa huo, hung'ata wakati wa mchana na baada ya virusi hivyo kuingia kwenye mwili wa binadamu, huchukua muda wa siku mbili hadi tatu kabla ya dalili za awali kuanza kuonekana.

    DALILI
    Kwa mujibu wa ripoti ya kitaalamu iliyotolewa na jopo la wataalamu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), dalili za ugonjwa wa Chikungunya zinafanana kwa kiasi kikubwa na zile za homa ya Dengue ambazo ni homa kali, maumivu ya kichwa, viungo kuuma na kuvimba na kutokwa na vipele vinavyowasha mwili mzima. Dalili nyingine ni kutapika, kuhisi kizunguzungu na mwili kuishiwa nguvu.
    Ripoti hiyo imeongeza kuwa, japokuwa ugonjwa huo hausababishi vifo vya ghafla, ukimpata mtu na akachelewa kupata matibabu, husababisha ulemavu wa kudumu kutokana na virusi vya ugonjwa huo kushambulia viungio (joints) vya miguu, mikono, mgongo na shingo.
    MATIBABU
    Mpaka sasa, hakuna chanjo wala tiba ya ugonjwa huo isipokuwa kinachofanyika ni kutibu dalili anazokuwa nazo mgonjwa. Wataalamu hao wakaenda mbele na kueleza kuwa kwa sababu ugonjwa huo hauna tiba wala chanjo, ni vyema watu wakajikinga wasing'atwe na mbu huyo ambao kwa kawaida hung'ata nyakati za mchana.
    Pia wamewatahadharisha watu wote kuhakikisha mazingira wanayoishi ni safi na salama, kuangamiza mazalia ya mbu, kufukia madimbwi, kufyeka vichaka  na kupulizia dawa za kuua wadudu sehemu ambazo mbu hao wanajificha.
    Tangu ugonjwa huo ulipogundulika kwenye mpaka wa Tanzania na Msumbiji miaka kadhaa iliyopita, umeendelea kusambaa kwa kasi kwenye nchi za Burundi, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo, Malawi na nchi nyingine kadhaa zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara. Pia ugonjwa huo umesambaa sehemu nyingine mpaka kwenye Bara la Ulaya, Asia na Amerika.
    Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Seif Rashid alipotafutwa na mwandishi wetu kuzungumzia ugonjwa huu, simu yake haikupatikana.
  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.