"Sipo tayari kupoteza tena muda wangu na pesa zangu kama nilivyofanya kipindi kilichopita". Alisisitiza Poppe. |
WEKUNDU wa ,Msimbazi Simba sc wameshamaliza mazungumzo na wachezaji wawili kutoka nchi za Uganda na Kenya na kinachosubiriwa ni safu mpya ya uongozi itakayopatikana juni 29 mwaka huu baada ya kufanyika uchaguzi.
Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba sc, Keptein wa zamani wa Jeshi la wananchi la Tanzania, (JWTZ), Zacharia Hans Poppe ameiambia MPENJA BLOG jioni hii kuwa tayari wamepata `jembe` moja la kazi kutoka Uganda na lingine kutoka Kenya ( hakutaja majina).
Kuhusu wachezaji waliokuwa nao msimu uliopita, mwanajeshi huyo wa zamani wa JWTZ alisema kuwa wameamua kuwabakisha wachezaji 13.
"Wachezaji wa zamani tuliobaki nao ni 13 tu, kwahiyo tutachukua wengine 12 wa hapa nchini na hao wawili kutoka nje".
"Sisi tunaendelea vizuri na usajili, kimsingi nawaasa wenzangu waingize timu nzuri ya Uongozi ambayo tunaweza kufanya nayo kazi"
"Wawe makini kwasababu wachezaji hawa tunaowasajili ni kwaajili ya msimu ujao.
'Waangalie viongozi ambao tutakubaliana kimawazo na sisi, kwasababu tunaweza kuwa na malumbano tena".
Poppe aliongeza kuwa wagombea wengi wanaowania nafasi za uongozi walishawahi kuwa viongozi wa Simba, hivyo wanachama waangalie ni nani alikuwa na mafanikio katika kipindi chake.
"Binafsi najua Aveva ni kiongozi mzuri na akiwa na makamu wake Kaburu, basi timu itakuwa nzuri na tutatengeneza gurudumu la Simba".
"Nikianza na Kaburu, mtu huyu aliweza kuitengeneza timu ya U20 ambayo imezaa wachezaji kama Ramadhani Singano `Messi`, Harun Chanongo, Said Ndemla na wengineo. Haya ni matunda yanayotokana na jitihada kubwa alizofanya Kaburu".
"Aveva alikuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili wakati ambao Simba alikuwa na mafanikio ambayo hayajapatikana mpaka leo".
"Ni kipindi ambacho Simba iliweza kuwa na makombe nane. Ni kipindi ambacho alikuwepo Kassim Dewji aliyejenga jengo ambalo linawaingizia kipato viongozi wa sasa".
"Timu ya Aveva na Kaburu nadhani inaweza kuleta matokeo ambayo yalipatikana kipindi kile, ambayo hayajapatikana mpaka leo. Kwahiyo nafikiri hawa ni watu ambao wanaweza kuleta maendeleo bila tatizo". Alisema Poppe.
Akimzungumzia Jamhuri Kiwhelo na Richard Wambura, Poppe alisema hawajawahi kupata mafanikio katika uongozi wao.
"Wambura alipata mafanikio gani wakati wa uongozi wake. Mimi sioni kama kuna kitu alifanya akiwa Simba. Wadau waseme hawa walifanya A,B C, D. Mimi nimesema Aveva na Kaburu walifanya nini".
"Julio anagombea umakamu mwenyekiti, sijui amefanya nini. Yeye kazi yake ilikuwa ukocha na alikuwa analipwa mshahara. Wasichague mtu kwasababu tu ana wafuasi wengi, eti wanampenda sura au maneno yake. Sisi tunataka uhalisia, je, alifanya kitu gani?". Alihoji Poppe.
Poppe aliweka wazi msimamo wake kuwa endapo wanachama hawatawachagua Aveva na Kaburu itakuwa juu yao, lakini yeye hatakuwepo katika uongozi wa Simba tofauti na safu ya hao wawili.
"Msimamo wangu nausema wazi. Sitaweza kufanya kazi na viongozi tofauti na hao wawili. Kwasababu naelewa uongozi wowote tofauti na hao wawili hautaleta mabadiliko yoyote".
"Sipo tayari kupoteza tena muda wangu na pesa zangu kama nilivyofanya kipindi kilichopita". Alisisitiza Poppe.
Uchaguzi wa Simba sc utafanyika jijini Dar es salaam juni 29 mwaka huu ambapo Rais mpya , makamu wa rais na wajumbe wapya wa kamati ya utendaji watapatikana tayari kwa safari nyingine ya miaka minne ya uongozi.
0 comments:
Post a Comment