Fainali ya michuano ya mpira wa miguu ya ufukweni (beach soccer) kati ya timu za Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) inachezwa kesho (Mei 25 mwaka huu) kwenye ufukwe wa Escape One uliopo Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Timu hizo zimepata nafasi ya kucheza fainali baada ya kushinda mechi zao za nusu fainali dhidi Chuo Kikuu cha Ardhi (AU) na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) zilizochezwa wikiendi iliyopita.
Mgeni rasmi katika fainali hiyo itakayooneshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Azam Tv atakuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na itaanza saa 4.15 asubuhi. Fainali hiyo itatanguliwa na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu kati ya AU na TIA kuanzia saa 3 kamili asubuhi.
Michuano hiyo ambayo ni ya kwanza kufanyika nchini ilishirikisha vyuo 13 vya Dar es Salaam, na ilianza Aprili 20 mwaka huu katika fukwe za Escape One na Gorilla iliyopo Kigamboni.
Vyuo vingine vilivyoshiriki ni Chuo Kikuu cha St. Joseph Tanzania (SJUIT), Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (TUDARCO), Taasisi ya Ustawi wa Jamii (ISW) na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Vingine ni Chuo cha Utumishi wa Umma Magogoni, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Utawala wa Kodi (ITA), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es Salaam (DSJ).
Tanzania itashiriki katika michuano ya Afrika ya mpira wa miguu wa ufukweni itakayofanyika mwakani nchini Shelisheli.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
0 comments:
Post a Comment