MCHARAZA gitaa la solo aliyeacha muhuri wake hapa Tanzania, Dekula Kahanga Vumbi, akiwa na bendi yake, mwezi huu anatarajia kuzindua albam yake mpya hii ikiwa ni mara ya kwanza baada ya miaka sita.
Vumbi ambaye kwa sasa maskani yake yako Stockholm, Sweden anakofanya vizuri katika soko la kimataifa, ameiambia Saluti5 kwa njia ya simu kuwa albam hiyo itajulikana kama "Shujaa Mamadou Ndala" ambayo ndani yake itakuwa na jumla ya nyimbo nane zenye mahadhi ya Swahili Rumba (muziki wa dansi), Soukouss na Salsa.
Mwanamuziki huyo ambaye pia ni mwimbaji na mtunzi mahiri amesema albam hiyo itachangia kurudisha hadhi ya muziki wa dansi wa Tanzania.
Uzinduzi huo utafanyika Mei 23 na 24 katika ukumbi wao wa nyumbani Little Nairobi ulioko katika jiji la Stockholm.
Wimbo uliobeba albam "Shujaa Mamadou Ndala" ni mahsusi kwaajili ya kumuenzi Mamadou Ndala aliyekuwa mmoja wa wanajeshi wa Kongo waliopambana kurejesha amani nchini humo kwa kusaidiwa na jeshi la Tanzania.
Vumbi aliyetamba sana hapa Bongo na bendi ya Maquis kuanzia miaka ya 90, alizitaja nyimbo zingine zinazounda albam hiyo kuwa ni Mama Afrika, Kuna Mambo, Liverpool, Wabibi wa leo,Tucheze Salsa, Kigeugeu na Agnes ambazo zote ni utunzi wake kasoro mmoja tu "Wabibi wa leo" uliotungwa na Bobo Sukari.
Wanamuziki walioshiriki kurekodi albam hiyo iliyorekodiwa katika studio za Sensus na Joji hapo Stockholm ni Bobo Sukari (mwimbaji), Joseph Semafumu (bass), Rafael Sida (congas, bongos), Ulf Linden Baryton (sax), Celso Paco (drums), Henry Matano (drums na keyboard) huku Vumbi mwenyewe akingurumisha magitaa yote pamoja na kuimba.
Kesho tutakuwekea hapa Saluti5 wimbo "Shujaa Mamadou"
0 comments:
Post a Comment