May 12, 2014

  • NORA AFUNGUKA KUACHIKA KWENYE NDOA

     
     
     
     
    Makala: Gladness Mallya
    BAADA ya kusoma Exclusive Interview ya staa wa filamu za Kibongo, Blandina Chagula 'Johari', leo katika kona hii tunakuletea mwanadada mkongwe katika ulimwengu wa filamu, Nuru Nassoro 'Nora' aliyezaliwa jijini Dar.
    Mwanadada mkongwe katika ulimwengu wa filamu, Nuru Nassoro 'Nora'
    Amezungumza mambo mengi yahusuyo tasnia ya uigizaji na maisha yake binafsi, mahojiano yalikuwa hivi:
    Gladness: Wasomaji wangependa kujua Nora ni nani?
    Nora: Ni msanii mkongwe wa filamu Bongo.
    Gladness: Una elimu gani na uliipata wapi?
    Nora: Nina elimu ya kidato cha nne, nilisoma Shule ya Msingi Ananasifu iliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam na baada ya hapo nikajiunga na Shule ya Sekondari Kinondoni Muslim ambapo nilihitimu masomo yangu ya kidato cha nne.
    Gladness: Ulianza lini kujishughulisha na sanaa ya uigizaji?
    Nora: Niliingia kwenye sanaa mwaka 2000 kupitia Kundi la Sanaa la Kaole baada ya kujaza fomu kuomba nikakubaliwa na kuanza mazoezi.

    Gladness: Ulichukua muda gani kwenye mazoezi hadi kuonekana runingani?
    Nora: Nilifanya mazoezi kwa muda wa miezi mitatu tu, nikaanza kuonekana kwenye runinga kwani ilikuwa inategemeana na juhudi za mtu kwa hiyo nilikuwa na juhudi sana ndiyo maana nikafanya mazoezi kwa muda mfupi.
    Gladness: Unakumbuka ni mchezo gani ulioanza kuonekana nao runingani?
    Nora: Ndiyo nakumbuka ulikuwa unaitwa Hujafa Hujaumbika ambao tulikuwa tukicheza na kina Muhogo Mchungu, Kemmy, Swebe, Kenny na wengine wengi.
    Gladness: Ulitokaje kwenye michezo ya runingani mpaka kwenye filamu?
    Nora: Baada  ya watu kuona kipaji changu kwamba najua kuigiza tena kwa hisia nilianza kushirikishwa kwenye filamu mbalimbali ambapo ya kwanza ni ile ya Sikitiko Langu.
    Gladness: Je, mpaka sasa una filamu ngapi za kwako?
    Nora: Nina filamu mbili ambazo ni Msimamo Wangu na Ndoa Goli la Tatu.
    Gladness: Je, umeshashirikishwa filamu ngapi mpaka sasa?
    Nora: Nimeshirikishwa kwenye filamu nyingi sana, zaidi ya kumi na mbili.
    Gladness: Ni filamu gani ambayo unaipenda sana na kwa nini?
    Nora: Naipenda sana filamu ya Sikitiko Langu kwa sababu ni filamu ambayo nilishirikishwa ya kwanza ikanipatia mashabiki wengi na marafiki kutoka nje na ndani ya nchi.
    Gladness: Kwa nini uliachana na mumeo Luqman?
    Nora: Huwa sipendi kuzungumzia sababu ya ndoa yetu kuvunjika kwani niliteseka sana ila kubwa ni kwamba mume wangu alinioa ili apate ustaa kupitia mimi kwani alikuwa akifanya kazi zile nilizokuwa nikifanya mimi na kunikataza nisiendelee na sanaa.
    Gladness: Inasemekana ndoa yako ilivunjika kutokana na tabia zenu nyie wasanii kuendekeza ustaa mpaka kwenye ndoa kama ilivyo kawaida ya mastaa wengi ndoa zao hazidumu?
    Nora: Hapana siyo kweli, baada ya mwanaume kutimiza lengo lake la kupata ustaa kupitia mimi ndipo mateso yalizidi tukafikia hatua ya kuachana.
    Gladness: Una watoto wangapi?
    Nora: Nina mtoto mmoja.
    Gladness: Je una mpango wa kuolewa tena?
    Nora: Ndiyo ila sijui nitaolewa lini na mwanaume gani.
    Gladness: Tangu uvunje ungo ulishakuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanaume wangapi?
    Nora: Mh, hilo siwezi kujibu ni siri yangu.
    Gladness: Wasanii wa kike mna tabia ya kuchukuliana mabwana, je ulishawahi kuibiwa bwana?
    Nora: Mimi sijawahi kuibiwa bwana wala sijawahi kuiba.
  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.