October 15, 2016

  • VITENDO VYA KISHIRIKINA DHIDI YA WATUMISHI WA HALMASHAURI VYAMKERA JAFO


    VITENDO VYA KISHIRIKINA DHIDI YA WATUMISHI WA HALMASHAURI VYAMKERA JAFO

    foja1

    Naibu Waziri Ofisi ya Rais , Tawala za mikoa na serikali za mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo, akiwa na Mkuu wa wilaya ya Igunga na viongozi mbalimbali akipewa taarifa juu ya ujenzi wa nyumba za walimu, madarasa na vyoo vya shule za sekondari wilayani humo.

    foja2

    Naibu Waziri Ofisi ya Rais , Tawala za mikoa na serikali za mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo, akipewa maelekezo juu ya matumizi ya mfumo wa kukusanyia mapato.

    foja3

    Naibu Waziri Ofisi ya Rais , Tawala za mikoa na serikali za mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo, akiwa na mbunge wa Nzega Hussein Bashe katika ukaguzi wa bweni la wasichana wilaya ya Nzega.

    KUTOKANA na baadhi ya wananchi kuwafanyia vitendo vya ushirikina watumishi katika Halmashauri mbalimbali nchini, Naibu Waziri Ofisi ya Rais , Tawala za mikoa na serikali za mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo ameonyeshwa kukerwa na tabia hiyo huku vimesababisha watumishi kupata msongo wa mawazo na wengine kuomba kuhamishwa.

    Jafo alitoa kauli hiyo alipokuwa akikagua zahanati mpya iliyopo kijiji cha Ziba ndani ya Jimbo la Manonga wilayani Igunga mkoani Tabora na alipokuwa akizungumza na watumishi wa wilaya hiyo.

    Alimuagiza mkuu wa wilaya ya Igunga kutenga muda yeye na kamati yake ya ulinzi na usalama kuwafikishia ujumbe wananchi wa wilaya ya Igunga kuwakemea wenzao wenye tabia hiyo wilayani humo ili kuacha tabia hiyo ovu. 

     Jafo alisisitiza kwamba tabia hiyo imewasababishia baadhi ya watumishi walio tendewa vitendo visivyo kupatwa na msongo wa mawazo na kuomba kuhama maeneo walio pangiwa.

    Naibu Waziri alisema kwamba jamii inapaswa kuwathamini watumishi kwani wametoka maeneo mbalimbali ya nchi ili kuja kuwatumikia wao hivyo wanatakiwa kuwathamini na kuwaheshimu kwa kulinda utu wao.

    " Watani zangu mliopo hapa Wasukuma na Wanyamwezi mmepata zahanati nzuri naomba muitunze. Pia sitaki kusikia daktari au mhudumu  amelala asubuhi anajikuta ng'ambo ya barabara au katika kiwanja cha mpira,"alisema Jafo

    Kadhalika, alikemea kitendo cha sungusungu walio mchapa viboko mwalimu mkoani humo huku akiwaagiza wakuu wa wilaya maeneo yote kupambana na tabia za udhalilishaji wanazo fanyiwa watumishi wa umma katika jamii ili waweze kufanya kazi kwa amani na kujiamini.

    Aliwapongeza viongozi wa mkoa wa Tabora kwa umoja na ushirikiano wao katika kuwaletea maendeleo wananchi wa mkoa huo. (P.T)



  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.