Kinana aliyasema hayo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Peoples, ikiwa ni hitimisho la ziara yake mkoani Singida.
Alisema anatambua kuwa kuna upungufu na makosa ya kiutendaji kama kushamiri kwa rushwa na upendeleo serikalini jambo ambalo linasababisha wananchi kuilalamikia serikali na CCM.
"Watendaji serikalini wanatumia ufumbuzi wa muda wa kuzima moto, lazima tujenge utaratibu wa kumaliza matatizo ya wananchi kwa mipango ya muda mrefu," alisema.
Aliongeza, "upungufu mwingine ni uwajibishaji wa watendaji wabovu, wakati anaharibu utawala bora haushiriki ila akishaharibu ndio utawala bora unaanza…"
"Inaundwa tume na uchunguzi kisa utawala bora, sipingi utawala bora bali napinga unaolalia upande mmoja… dhambi kabla haijatendaka hatua hazichukuliwi ila ukishakamilika ndiyo unachukuliwa," alisema.
Alikosoa utaratibu wa kuwahamisha watendaji wanaotuhumiwa kwa utendaji mbovu na wizi, huku ikielezwa kwamba hakuna ushahidi wa kutia hatiani.
Kinana, alisema ni lazima nidhami iongezeke serikalini, uwajibishaji, kuchukua hatua mapema, na kwamba imekuwa kawaida kwa jambo dogo kuachwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na watu kwenye kituo kingine kabla ya kuchukuliwa hatua.
"Wapo watendaji inawachukua muda mrefu kuchukua hatua,tutasimamia mapungufu ndani ya CCM na serikali yake," alisema.
Aidha, aliwaahidi wananchi utumishi uliotukuka na siyo utumishi na kwamba kinachomshinda kushughulikia ni baadhi ya viongozi kupenda utukufu kwa kuitwa waheshimiwa bila utumishi uliotukuka.
Aidha, alisema alipokwenda kuna migogoro ya wakulima na wafugaji, wakulima na hifadhi, wakulima na misitu, wafugaji na hifadhi na wafugaji na misitu na kwamba Kamati Kuu, imeagiza kuchukuliwa hatua za kumaliza hatua zilizopo.
Alisema watendaji serikalini wanatumia ufumbuzi wa muda wa kuzima moto, lazima tujenge utaratibu wa kumaliza.
ATUMIA BAJAJI
Awali, Kinana, Naibu Katibu Mkuu wake, Mwigulu Nchemba na baadhi ya mawaziri, walitumia usafiri wa pikipiki na bajaji kuingia uwanjani hapo.
Mbali na mkutano huo, wananchi wakizunguzia ujio wa katibu huyo mkuu wa CCM katika mkoa wa Singida wanasema kuwa ni wazi kuwa uhai wa chama umerejea mahali pake kama ilivyo kuwa enzi za hayati Mwalimu Nyerere.
Magnalena Philemon mkazi wa Singida alisema CCM kilikuwa kimepoteza muelekeo lakini hadi sasa chama kimerudi mahali pake baada ya Kinana kuwepo madarakani.
Shabani Magita alisema CCM ni nzuri isipokuwa 'imevamiwa' na walafi na waroho wa madaraka waliokuwa wakitaka kukitumbukiza shimoni.
Mkuu wa mkoa huo, Dk. Perseko Kone, alisema wamepiga hatua kubwa ya kuondoka kwenye hali ya umasikini na balaa la njaa kupitia kilimo bora.
Alisema pamoja na juhudi za serikali, wamepiga hatua katika sekta ya elimu kwa kuongeza ufaulu wa wanafunzi wa shule za msingi kwa asilimia 100.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji, Amosi Makala alisema serikali inaendelea na mkakati wa kuhakikisha inaboresha na kukamilisha reli ya kati, ili usafirishaji mizigo na kukuza uchumi wa nchi.
Source: Nipashe
0 comments:
Post a Comment