May 18, 2014

  • EPZA yafikia makubaliano na kampuni kuendeleza eneo huru bandari Mtwara

     
     
     
     
    Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA) imefikia makubaliano na kampuni nne za kimataifa kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali kwa kampuni kubwa zinazofanya utafiti wa mafuta na gesi katika mkoa wa Mtwara.
    Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Adelhelm Meru aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kuwa hatua hiyo ni muhimu sana katika undelezaji wa eneo huru la bandari ya Mtwara.
    EPZA inaendeleza hekta 10 za eneo huru la bandari ya Mtwara. Hekta hizo ni kati ya jumla ya hekta 110 za eneo hilo huru la bandari ambalo limetengwa na serikali kwa ajili ya uwekezaji mbalimbali.
    Hekta hizo 10 zitaendelezwa kwa kuwekewa miundombinu inayotakiwa na kisha kugawiwa kwa makampuni ya kimataifa yanayofanya kazi za kutoa huduma mbalimbali kwa makampuni yanayofanya kazi ya utafiti wa mafuta na gesi katika mkoa wa Mtwara.
    Kitakapomalizika, kituo hiki cha huduma kwa makampuni yanayofanya utafiti wa gesi na mafuta mkoani Mtwara kitakuwa cha kipekee si kwa Tanzania pekee bali katika ukanda mzima wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.
    "Leo tunahitimisha safari ndefu ya uanzishaji kituo kipya katika bandari huru ya Mtwara ambacho kitahudumia watafiti wa gesi na mafuta," alisema, na kuongezea kuwa  kampuni hizo sasa zitaenda kuanzisha karakana kubwa kwa ajili ya kuzihudumia kampuni mbalimbali zikiwemo British Gas na Start Oil zinazofanya kazi ya kutafiti gesi na mafuta katika eneo hilo.
    Alizitaja kampuni zilizo saini makubaliano hayo kama Slumberger Seaco Inc ya Marekani, Altus Oil Field Supplies Services ya Singapore, Tans Ocean Industries and Services LTD ya Dubai na Lenna ya Iran. Kampuni nyingine tatu zitasaini makubaliano hayo wiki ijayo.
    "Zoezi la kupata wawekezaji katika eneo hili lilianza mwaka 2010 baada ya kampuni za utafutaji gesi na mafuta kuomba kuwepo kwa kampuni za watoa huduma," alisema.
    Alisema kampuni hizo ni kubwa na zina uzoefu mkubwa wa shughuli hizo na zimepatiwa maeneo katika eneo la hekta 10 kuanza kujenga na kutoa huduma.
    "Katika eneo hilo  watajenga karakana kubwa kwa ajili ya kufanyia ukarabati na matengenezo ya vifaa vya ya mafuta na gesi," alisema.
    Akifafanua zaidi alisema karakana hizo zitajengwaza kisasa na zitakuwa na uwezo pia wa kuhudumia nchi jirani kama Kenya, Msumbiji, na Afrika Kusini.
    Alisema uanzishaji wa kampuni hizo una manufaa makubwa kwa nchi kwa vile wananchi kupata ajira na serikali kuongeza mapato yake.
    Meneja Mradi Mwandamizi wa Kampuni ya Altus Oil Field Supplies Services Singapore, Bw. N.Sankaranarayanan alisema kampuni yake imejiandaa kuanza kufanya kazi ya kutoa huduma kwa makampuni ya utafutaji gesi na mafuta.
    "Tumejipanga kutoa huduma bora kama ilivyokusudiwa,"alisema, na kuongeza kwamba  kampuni yake inauwezo mkubwa na itatumia fursa hiyo kuwekeza katika eneo la kituo hicho kipya ili kutoa huduma bora.
          Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA) Dr. Adelhelm Meru (kulia) akisaini mkataba pamoja na Mkurugenzi wa kampuni ya Lena Holding & Investment Tanzania LTD, Bw. Riyaz Jamal (kushoto) kwa ajili ya kutoa huduma kwa makampuni makubwa ya utafutaji Mafuta na Gesi mkoani Mtwara mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.  Wanaoshuhudia ni Mkurugenzi wa Mipango wa EPZA Bw. Lamau Mpolo (kulia) na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa mamlaka hiyo, Bw. Desidery Kalimwenjuma. 
      Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA) Dr. Adelhelm Meru (kulia) akipongezena na Mkurugenzi wa Kamal Steels LTD, Bw. Satyam Gupta mara baada ya kusaini mkataba na makampuni manne kutoka katika nchi za Marekani, Singapore, Dubai na Iran kwa ajili ya kutoa huduma kwa makampuni makubwa ya utafutaji Mafuta na Gesi katika Mkoani Mtwara.  Tukio hilo lilifanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

    Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA) Dr. Adelhelm Meru akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari wakati wa utiaji saini mkataba na makampuni manne kutoka katika nchi za Marekani, Singapore, Dubai na Iran kwa ajili ya kutoa huduma kwa makampuni makubwa ya utafutaji Mafuta na Gesi Mkoani Mtwara.  Tukio hilo lilifanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.