Mkuu wa majeshi nchini Thailand ametangaza mapinduzi , akisema jeshi sasa linachukua udhibiti wa serikali.Katika taarifa iliyotolewa kupitia kwa televisheni, mkuu huyo wa majeshi alisema jeshi litarejesha utawala wa kisheria na kufanya mageuzi ya kisiasa.
Majeshi yalizingira eneo la tukio mjini Bangkok ambapo makundi ya kisiasa yamekuwa yakifanya mazungumzo kwa siku ya pili na kuwachukua viongozi wao.
Mapinduzi haya yanakuja baada ya miezi kadhaa ya ghasia za kisiasa na kuwekwa kwa sheria ya kijeshi.Jeshi litatuma vikosi na magari kuwasindikiza waandamanaji kutoka maeneo ya maandamano , afisa wa kijeshi alilieleza shirika la habari la Reuters.
Ghasia za hivi karibuni zialianza katika mji mkuu wa Thailand mwishoni mwa mwaka jana, wakati waziri mkuu Yingluck Shinawatra alipovunja bunge la nchi hiyo .
Waandamanaji waliweka vizuizi kwenye maeneo ya mji wa Bangkok katika kipindi cha mwezi mmoja.
Mapema mwezi huu , mahakama ilimuamuru kuondolewa madarakani kwa Bi Yingluck kwa madai ya kutumia vibaya mamlaka.
Thailand imekabiliwa na mzozo wa kupigania mamlaka tangu kaka yake Bi Yingluck , Thaksin Shinawatra, kung'olewa mamlakani na jeshi kama waziri mkuu mnamo mwaka 2006.
0 comments:
Post a Comment