May 18, 2014

  • Elimu ya Ukweli: ASASI YA TAHA YATOA MAFUNZO KWA WAKULIMA WA KABEJI SIMAMBWE MBEYA

     
     
     
     

    Afisa Ufundi kutoka TAHA, Isaack Ndamanyile, alisema lengo la kutoa mafunzo hayo ni kutoa teknolojia bora za kisasa kwa wakulima na kutumia mbolea na madawa.


    Baadhi ya wakulima waliofika katika mafunzo hayo wakimsikiliza kwa makini mkufunzi wao

     
     

    Baadhi ya wakulima waliofika katika mafunzo hayo wakisoma jarida la kilimo

     

    Baadhi ya wakulima wakiwa katika mafunzo ya shamba Darasa

     
     

    Baadhi ya wakulima wakitembelea shamba la mfano eneo la Simambwe






    ASASI ya Tanzania Horticulture Associatino(TAHA)yenye makao makuu mkoani Arusha imetoa mafunzo kwa wakulima wa mazao ya Kabeji kutoka vijiji 12 vya Wilaya ya Mbeya yaliyofanyika kwa vitendo katika mashamba darasa yaliyopo Simambwe kata ya Tembela wilaya ya Mbeya mkoani hapa.
     
    Akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo, Afisa Ufundi kutoka TAHA, Isaack Ndamanyile, alisema lengo la kutoa mafunzo hayo ni kutoa teknolojia bora za kisasa kwa wakulima na kutumia mbolea na madawa.
     
    Alisema mafunzo hayo hadi sasa yamewanufaisha wakulima kutoka vikundi 12 kati ya 35 ambavyo vimeshiriki mafunzo hayo moja kwa moja ambapo wamejifunza jinsi ya kuandaa mashamba matumizi ya mbolea na mbegu bora za mazao ya kabeji.
     
    Alisema mbali na mafunzo hayo wakulima pia watatafutiwa masoko ya mazao yao ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha na wafanyabiashara wakubwa wa kununua mazao yao.
     
    Aliongeza kuwa wakulima wamefundishwa kulima mazao hayo kutokana na kutoa matunda baada ya muda mfupi hivyo kumnufaisha mkulima moja kwa moja badala ya kusubiri muda mrefu.
     
    Alitoa mfano wa zao la kabeji kuwa linavunwa baada ya miezi mitatu baada ya kupandwa hivyo mkulima anakuwa na uhakika wa kupata mavuno kwa muda mfupi baada ya kulima kwa kuzingatia kanuni na ushauri wa kitaalamu.
     
    Baadhi ya wakulima waliofika katika mafunzo hayo walisifia Asasi hiyo kwa hatua yao ya kuwafikia wakulima na kutoa mafunzo katika mashamba yao na kwamba hilo litasaidia kuwainua kiuchumi.
     
    Aidha walisema baada ya kulima kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu wameanza kusumbuliwa na wanunuzi mashambani kabla ya mazao kukomaa kutokana na mwonekano ulivyo.
     
    Walisema jinsi walivyofundishwa kilimo cha kisasa mkulima anao uwezo wa kujua thamani ya mazao yake hata kabla ya kuvuna kutokana na mpangilio uliowekwa ambao utaondokana na kudhurumiwa na wachuuzi wa mazao mashambani.
     
    Mwisho.

    Na Mbeya yetu
     
     
  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.