WAZIRI MKUU Mizengo                Pinda amesema Serikali haitataifisha shule, zahanati,                hospitali wala Vyuo Vikuu vinavyoendeshwa na taasisi za                kidini na amewahimiza wajenge zaidi na zaidi ili kuisaidia                jamii kubwa ya Watanzania.
        Ametoa wito huo wakati                akizungumza na walimu, wazazi na wahitimu wa kidato cha                nne wa shule ya sekondari Magnificat iliyoko Sanya Juu,                wilayani Siha mkoani Kilimanjaro.
        Waziri Mkuu ambaye                aliwasili Sanya Juu jana asubuhi (Jumamosi, Septemba 20,                2014) akitokea Dodoma, alisema huko nyuma Serikali                ilitaifisha shule na vyuo lakini kwa kiasi fulani                ilishindwa kuviendesha ikaamua kuvirudisha kwa wamiliki                wake ambao ni taasisi za kidini.
        "Ni kweli huko nyuma                tulikuwa navyo, lakini tumevirudisha kwenu tunataka na                ninyi ni washirika katika kuleta maendeleo kwa wananchi                walio wengi," alisema Waziri Mkuu.
        "Nilishawahi kusema huko                nyuma na leo nasisitiza tena kwamba hatutaifisha shule,                zahanati, hospitali wala Chuo Kikuu chochote cha taasisi                ya kidini. Ninawasihi mjenge zaidi na zaidi," aliongeza.
        Waziri Mkuu ambaye                alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa shule hiyo                iliyoanzishwa Januari 15, 2011, aliwakabidhi vyeti                wanafunzi 42 wa kidato cha nne wanaotarajia kufanya                mtihani wa kidato cha nne Novemba, mwaka huu ikiwa ni mara                ya kwanza kwa shule ya sekondari ya Magnificat kufanya                mtihani huo.
        Waziri Mkuu aliwapongeza                wanafunzi hao kwa kushika nafasi ya kwanzawilayani Siha                kwenye mitihani ya utamirifu (yaani mock) katika kidato                cha nne. "Vilevile, shule hii imekuwa ya 12 kati ya shule                316 za Mkoa wa Kilimanjaro na ya 16 kati ya shule 564 kwa                Kanda ya Kaskazini Mashariki zilizofanya mtihani huo. Mimi                napata imani kuwa watafanya vizuri kwenye mtihani wao wa                kidato cha nne Novemba 2014," aliongeza.
        Mapema,Mkuu wa Shirika                la Masista la Kazi ya Roho Mtakatifu na Meneja wa Shule                hiyo, Sista Inviolata Kessy alisema shule hiuo ilianzishwa                kwa lengo la kutoa elimu bora na kuwashawishi watoto wa                kike wa Kimasai waone umuhimu wa elimu na hivyo kuwaepusha                na ndoa za utotoni. Vile vile, kuwapa msingi mzuri wa                elimu kama sehemu ya maandalizi yao ya kupata elimu ya                juu.
        Alisema shule hiyo                ambayo ni ya mchanganyiko na ya mchepuo wa sayansi na                biashara, imefanikiwa kujenga maabara tatu za kemia,                fizikia na baiolojia pamoja na chumba cha kompyuta.
        Akisomarisalakwa niaba                ya wahitimu, Anastazia Kimaro alisema shule hiyo                inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo ukosefu wa jengo                la utawala pamoja na basi la shule la kuwapeleka                wananfunzi kwenye ziara za mafunzo.
        Aliomba pia wawe                wanapelekewa magazeti ya kila siku na kila wiki ili                wanafunzi wa shule waweze kupata taarifa mbalimbali za                mambo yanayojiri nchini na duniani.
        
0 comments:
Post a Comment