JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambalo mwezi huu limetimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake Septemba Mosi, mwaka 1964, limetajwa kuwa miongoni mwa majeshi bora na yenye weledi, uzoefu na ujuzi mkubwa wa mapambano katika Bara la Afrika na nje ya Bara hilo.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu Dar es Salaam jana, imekitaja Kikosi cha Majeshi Maalum (Special Forces) cha JWTZ kinacholinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuwa miongoni mwa vikosi bora 30 vya majeshi maalum duniani kwa mafunzo, uwezo na weledi.
TPDF lilihitimisha sherehe za miaka 50 ya uhai wake kwa Onyesho la Medali la Operesheni Maliza Matata lililofanyika kwenye eneo la mafunzo la Jeshi hilo la Langururusu, Wilaya ya Monduli, Mkoa wa Arusha, ambako Rais Jakaya Kikwete na Amiri Jeshi Mkuu, alikuwa mgeni rasmi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo katika miaka yote 50 ya uhai wake, si tu kwamba JWTZ imetekeleza ipasavyo malengo na shabaha zake za msingi kikwelikweli, lakini pia limebakia jeshi imara, lenye uzalendo, lenye utii na nidhamu ya hali ya juu.
"Hizi ni sifa ambazo mataifa mengi hususan katika Afrika zimeshindwa kufanikisha, tunaweza kusema kwa uhakika kabisa kuwa amani, utulivu na usalama wa nchi yetu katika miaka yote 50 umechangiwa sana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania," ilieleza taarifa hiyo ikimnukuu Rais Jakaya Kikwete.
Alieleza kuwa JWTZ limelinda ipasavyo mipaka ya Tanzania na uhuru wake kwa vitendo kwa kuyapiga na kuyasambaratisha kabisa majeshi ya uvamizi ya Idd Amin wa Uganda katika vita ya 1978/79 ambalo kwa mara ya kwanza jeshi la nchi moja limelipiga kabisa jeshi la nchi nyingine na kulifuta kabisa. Shughuli hii iligharimu maisha ya wanajeshi wa Tanzania.
JWTZ limeshiriki kikamilifu kufanikisha harakati za ukombozi barani Afrika kwa kufundisha majeshi ya vyama vya ukombozi, kushiriki moja kwa moja kwenye vita vya ukombozi Kusini mwa Afrika na kuchangia kupatikana kwa uhuru wa Angola, Msumbiji, Zimbabwe, Namibia na Afrika Kusini. Kama ilivyokuwa vita dhidi ya Amin, vita vya ukombozi pia viligharimu maisha ya baadhi ya askari wa TPDF.
Jeshi hilo, limeendelea kushiriki katika shughuli za ulinzi wa amani duniani na kupata mafanikio makubwa kwenye operesheni za kulinda amani katika Liberia, Darfur (Sudan), Lebanon, Ivory Coast, Visiwa vya Shelisheli, Visiwa vya Comoro na sasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambako majeshi hayo yamekiangamiza kabisa kikundi cha waasi wa M23.
Wanajeshi wa JWTZ wameshiriki kikamilifu kwa kushirikiana na mamlaka za kiraia katika uokoaji na maafa hususan majanga yakiwemo – ajali ya Mv. Bukoba, ajali ya meli Zanzibar, mafuriko ya Kilosa, Morogoro, ambako Jeshi lilitengeneza hata reli iliyokuwa imezolewa na mafuriko hayo.
Pia taarifa hiyo ilieleza kuwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi limeendelea kutoa huduma mbalimbali za kijamii katika sekta za elimu na afya.
Watanzania wengi wamenufaika na shule na hospitali zinazomilikiwa na kuendeshwa na Jeshi katika maeneo mbalimbali nchini.Kupitia JKT na JKU, Jeshi la Wananchi limekuza na kuendeleza elimu ya kujitegemea kwa vijana wa Tanzania.
CHANZO: Majira
0 comments:
Post a Comment