Baadhi ya waandishi wa habari              wanaosafiri kwenda Malawi wakiwa wanamsikiliza Katibu tawala              msaidizi wakati wa kuagana.
                 Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Mbeya,              Leonard Magacha akizungumza na waandishi wa Habari              wanaotarajia kusafiri.
                 Mwenyekiti wa safari ya Malawi,              Ulimboka Mwakilili, akitoa ufafanuzi wakati wa kuagana na              ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
                 Mwandishi Christopher Nyenyembe, mmoja              wa Waandishi wanaosafiri akifafanua jambo.
                 Katibu tawala Msaidizi akiwa katika              picha ya pamoja na waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya.
                Kaimu Mkurugenzi wa Jiji Akiongea na Waandishi wa                Habari wanaokwenda Safarini Malawi
         Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Jiji la              Mbeya, Dk. Samwel Lazaro, akiwasikiliza waandishi wa habari              walipoenda kumuaga ofisini kwake.
                 baadhi ya Waandishi wa Habari wakiwa              ofisini kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya              wakimsikiliza kwa makini walipoenda kumuaga tayari kwa              safari ya Malawi.
                 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la              Mbeya, Dk. Samwel Lazaro akiwa katika picha ya pamoja na              waandishi wa habari wanaotarajia kusafiri baada ya kuagana.
        BAADHI ya  Waandishi              wa habari Mkoa wa Mbeya wanaotarajia kufanya ziara ya              kimafunzo nchini Malawi na Zambia wameagwa rasmi na viongozi              wa Serikali.
        Waandishi hao wapatao 15 wanatarajia              kuanza safari Septemba 14, Mwaka huu hivyo kabla ya kuondoka              wameagana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Halmashauri              ya Jiji la Mbeya.
        Maagano hayo yamefanyika leo kwa nyakati              tofauti na kupata Baraka zote kutoka kwa wawakilishi wa              Ofisi hizo na kuwataka waandishi kuuwakilisha vema Mkoa wa              Mbeya na Taifa kwa ujumla.
        Katibu Tawala Msaidizi, idara ya Utawala              na rasilimali watu, Leonard Magacha, kwa niaba ya Katibu              Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja, alisema matarajio              ya Mkoa ni kupata mrejesho kutoka kwa waandishi baada ya              kurudi kutoka safarini.
        Alisema hiyo ni fursa pekee ambayo              waandishi wanaitumia kuvitangaza vivutio mbali mbali              vilivyopo katika Mkoa wa Mbeya kwa watu wa Malawi ili waweze              kutembelea pamoja na fursa zilizopo.
        Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa              Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dk. Samwel Lazaro, amewataka              waandishi wa habari kutumia nafasi hiyo kuitangaza timu ya              Mbeya City kimataifa zaidi.
        Alisema hivi sasa Halmashauri imekuwa na              mahusiano mazuri na wananchi kutokana na uwepo wa timu ya              mpira wa miguu ambayo hivi sasa inajulikana nchi nzima hivyo              ni fursa iliyotokea ya kuitangaza nchi za Nje ili ijulikane              kimataifa zaidi.
        Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Msafara wa              Waandishi wa Habari kwenda nchini Malawi, Ulimboka              Mwakilili, ametoa shukrani kwa wadau mbali mbali              waliowezesha safari hiyo kwa hali na mali.
        Alisema mbali na kila mwandishi kuchangia              gharama za kwenda na kurudi lakini kuna wadau walioweza              kuchangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya safari hiyo.
        Aliwataja baadhi ya wadau kuwa ni              Mkurugenzi wa Hifadhi ya wanyama pori(Ifisi Zoo), Leirner,              WYCS, Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Ofisi ya Katibu tawala              Mkoa wa Mbeya, Faraja nursing na Maridadi Shop.
        Aliongeza kuwa wadau wengine              wanakaribishwa kuchangia safari hiyo kutokana na umuhimu              wake katika kutangaza fursa ambazo zinapatikana katika Mkoa              wa Mbeya kwa wafanyabiashara na wananchi wa Nchi ya Malawi.
        Naye Mratibu wa Safari hiyo, Venance              Matinya, alisema maandalizi ya safari yamekamilika kwa              asilimia kubwa hivyo kinachosubiriwa ni tarehe ya kuondoka.
        Alisema waandishi wa habari              wameshaajiandaa kwa mahitaji yote ya safari za nje ya nchi              ikiwa ni pamoja na kukata Hati za kudumu za kusafiria pamoja              na cheti cha chanjo ya ugonjwa wa manjano kwa mujibu wa              sheria.
        
0 comments:
Post a Comment