September 15, 2014

  • NEWS ALERT: WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI KUANZA ZOEZI LA KUHAKIKI VYAMA VYA KIJAMII HAPA NCHINI MWEZI UJAO


    NEWS ALERT: WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI KUANZA ZOEZI LA KUHAKIKI VYAMA VYA KIJAMII HAPA NCHINI MWEZI UJAO
    Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuanzia mwezi ujao, Oktoba 2014, itaanza zoezi la kuvihakiki Vyama vya Kijamii hapa nchini.

    Pamoja na mambo mengine, zoezi hili linalenga kuvifuta kutoka katika daftari la Msajili vya Vyama vya Kijamii vyama ambavyo vitabainika kuwa havina sifa tena ya  kuendelea kuwa katika daftari hilo.

    Vigezo ambavyo vinaweza kusababisha chama kufutwa kutoka katika Daftari la Msajili wa Vyama vya Kijamii ni pamoja na kutolipa ada za mwaka kwa wakati na kutowasilisha kwa Msajili taarifa za kila mwaka za utendaji kazi na mapato na matumizi ya fedha za chama husika.  Kigezo kingine ni kwa chama kufanya shughuli tofauti na zile zilizoandikishwa katika katiba ya chama husika.
    Ili kuvishirikisha vyama husika, Wizara wakati wa kuanza zoezi hili itachapisha katika baadhi ya magazeti majina ya vyama vyote vya kijamii vilivyopo katika kumbukumbu za daftari la Msajili wa Vyama vya Kijamii.
    Baada ya kutangaza majina hayo, kila chama cha kijamii kitatakiwa kuhakikisha kuwa kimetekeleza matakwa ya kisheria yaliyobainishwa wakati wa usajili wa chama husika.
    Baada ya  kipindi cha miezi mitatu tangu kutangazwa kwa tangazo hilo, Wizara itaanza kuchukua hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kukifuta katika daftari la Msajili chama cha kijamii ambacho kitakuwa hakijatekeleza matakwa hayo. 
    Aidha, pamoja na mambo mengine, taarifa zitakazopatikana kutokana na zoezi hili la uhakiki pia zitawezesha kuanzishwa kwa database ya vyama vya kijamii ambayo itasaidia kuboresha mawasiliano kati ya Msajili wa Vyama na vyama hivyo.
    Hadi sasa Daftari la Msajili wa Vyama vya Kijamii linaonyesha kuwepo kwa vyama vya kijamii 9,554 kote nchini. Kati ya hivyo, vyama vya kidini ni 956 na vyama vingine 8,598.
    Jukumu la kusajili na kusimamia Vyama vya Kijamii linafanyika chini ya Sheria ya Vyama vya Kijamii SURA 337 (Societies Act Cap. 337) iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002.
    Vyama vinavyosajiliwa chini ya Sheria hii ni pamoja na vyama vya kidini, vyama vya kitaaluma  na vyama vya maendeleo ya kijamii.

    Imetolewa na:
    Isaac J. Nantanga
    MSEMAJI

    WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI



  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.