KIKUNDI cha ngoma cha selo kilichopo katika kijiji cha Kweingoma, wilayani Handeni, mkoani Tanga, kimesema kimepania vikali Desemba 13 mwaka huu kufanya balaa katika tamasha la Handeni Kwetu 2014, litakalofanyika wilayani hapa.
Shauku ya kikundi hicho imetolewa na Kiongozi wao Zaina Selemani, alipozungumzia umuhimu wa tamasha hilo, ambalo mwaka jana walishindwa kushiriki kutokana na wasanii wake wengi kukabiliwa na mambo ya kifamilia, ikiwamo kuugua na kuuguliwa.
Akizungumza kwa furaha kubwa, Zaina alisema ngoma ya selo ni nzuri inayoshawishi kuangalia wasanii wanapokuwa jukwaani, hivyo mashabiki na wadau wote watapata burudani nzuri.
"Mwaka huu tutashiriki kwa nguvu zote kwasababu ni tamasha lililoanza vizuri kwa mkoa huu wa Tanga, maana vikundi vingi kutoka sehemu mbalimbali za Handeni na mkoa wa Tanga vinashiriki," alisema.
Naye Mratibu Mkuu wa tamasha hilo, Kambi Mbwana, alisema kuwa kwa siku kadhaa walikuwa wakifanya ziara kadhaa katika vijiji ambavyo vina vikundi vya ngoma za asili ili vishiriki, hususan vile ambavyo mwaka jana havikushiriki.
"Tunataka kuongeza wigo wa vikundi kutoka ndani ya Tanga na nje pia, ukizingatia kuwa tunahitaji tamasha lenye nguvu na mguso pia ili kukuza sekta ya utamaduni na uchumi wa nchi yetu," alisema Mbwana.
Tamasha la Handeni Kwetu lililopangwa kufanyika Desemba 13 katika Uwanja wa Azimio (Kigoda Stadium), ni moja ya matukio makubwa mkoani Tanga yanayokutanisha mamia ya watu kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania.
0 comments:
Post a Comment