Na Mwene Said wa Blogu ya Jamii
CHAMA cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kimeiomba Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam kuwaruhusu kufungua maombi yenye mwelekeo wa kupinga mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba unavyoendelea mjini Dodoma.
Wakili wa TLS Mpale Mpoki alilieleza jopo la majaji watatu linalioongozwa na Mwenyekiti Jaji Augustine Mwarija akisaidiana na Aloysius Mujulizi na Fauz Twaib kuwa kuna mambo kadhaa yanayobishaniwa ambayo yanahitaji Mahakama hiyo kuingilia na kutolea ufafanuzi.
Wakili Mpoki anayesaidiwa na wakili Fulgence Massawe, alieleza kuwa kwa kuangalia nyaraka mbalimbali walizowasilisha mahakamani hapana shaka kuwa mwenendo wa Bunge la Katiba unaovyoendelea hivi sasa unahitaji kutazamwa.
"Katika kutenda haki, haitapendeza mwananchi ambaye anaona haki zake zinaporwa azuiliwe kufungua malalamiko yake mahakamani. Hivyo itakuwa ni haki kama mahakama hii itaruhusu maombi yetu ili tuweze kuwasilisha kesi ambayo inakusudiwa," wakili huyo alisema.
Hata hivyo, naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju anayesaidiwa na mawakili wa serikali Gabriel Malata na Sylvia Matiku, aliiomba mahakama kutupilia mbali maombi hayo kwa vile hayana msingi.
Masaju alipinga uhalali wa maombi hayo kuwasilishwa kwa vile Mahakama Kuu haina mamlaka kwa sababu sheria ambayo inabishaniwa inahusu serikali toka pande mbili za muungano, yaani serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
"Ukiangalia kwa makini nyaraka zilizowalishwa zinaonyesha uwepo wa serikali mbili. Lakini sheria ambayo mwombaji ameitumia inatumika Tanzania bara tu," alisema.
Masaju aliongeza kuwa katika shauri lililopo Serikali ya Zanzibar haijaunganishwa na hivyo kama mahakama itatoa amri itakayoiathiri kutatoke nini. "Hii inaweza kusababisha mgogoro wa kikatiba," alibainisha.
Mara baada ya kusikiliza pande zote mbili, majaji hao walisema kuwa watatoa uamuzi wa juu ya maombi hayo Jumatatu ijayo.
0 comments:
Post a Comment