September 16, 2014

  • HOJA YA KUSITISHA BUNGE MAALUM LA KATIBA YAHITIMISHWA RASMI



    HOJA YA KUSITISHA BUNGE MAALUM LA KATIBA YAHITIMISHWA RASMI
    Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba toka Kamati namba Tano, Mhe. Dkt. Asha-Rose Migiro akisoma taarifa wakati wa mjadala wa jioni bungeni hapo jana 15 Septemba, 2014 mjini Dodoma.
    Na Benedict Liwenga, 
    MAELEZO-Dodoma 
    HOJA ya kusitisha Bunge Maalum la Katiba imehitimishwa rasmi Kisheria kwa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutamka kwamba bunge hilo linaweza kuendelea na shughuli zake. 
    Taarifa hiyo imetolewa jana 15 Septemba, 2014 na Mjumbe wa Kamati namba Tano, Mhe. Dkt. Asha-Rose-Migiro wakati wa mjadala wa jioni bungeni hapo.
     
    Akisoma taarifa hiyo, Dkt. Migiro amesema kuwa mjadala wa kusitisha bunge umefungwa rasmi hapo jana licha ya kuwepo kwa madai kuwa bunge hilo halina uhalali wa kisiasa. 
    "Kwaajili ya kuondoa shaka yoyote ningependa kuwaambieni takwimu tulizonazo hivi sasa, bunge hili lina jumla ya Wajumbe 630, kati ya hao waliotoka ni wajumbe 130 ambao ni sawa na asilimia 21% tu ya wajumbe wote, wajumbe waliobaki ndani ya bunge ni 500 hii ni sawa na asilimia 79% ya wajumbe wote na tukizichambua takwimu hizi, ningeomba kutambua wingi wa Kundi la 201", alisema Dkt. Migiro. 
    Akikanusha juu ya kuwepo kwa dhana iliyojitokeza ya kwamba wajumbe waliobaki ndani ya bunge hilo ni wa aina moja, Dkt. Migiro alisema kuwa taarifa hizo si za kweli, kwani kati ya wajumbe 500 walioko ndani ya bunge hilo wajumbe wanaotokana na kundi la 201 ni wajumbe 189 ambapo wajumbe wanaotoka Tanzania bara jumla yao ni 348 na kati ya hao, 125 ni wajumbe wanaotoka katika kundi hilo la 201. 
    "Ukitazama takwimu hizi kwa jicho lolote lile basi wajumbe wa 201 ni sehemu kubwa na ni sehemu muhimu ya wajumbe hawa waliobaki", alisema Dkt. Migiro. 
    Akizungumzia juu ya wajumbe toka upande wa Zanzibar, Dkt. Migiro alisema kuwa wajumbe waliobaki ni 152 na kati ya hao wajumbe 64 wanatokana na kundi la 201. 
    "Tunasisitiza takwimu hizi kwa wajumbe wa 201 kwasababu wajumbe hawa ndiyo wajumbe ambao kwa wingi wao kitakwimu lakini pia kwa wingi wao kimakundi wanawakilisha sura zote Kitaifa, hivyo ni dhairi kwamba kwa namna yoyote ile waliobaki ndani ni wengi, ni idadi kubwa, ni idadi wakilishi na tukiangalia kwa takwimu hizi, wajumbe walioamua kususia bunge kwa pande zote mbili hizi hawafikii hata theluthi moja ya wajumbe waliobaki", alisisitiza Dkt. Migiro. 
    Kwa kuzingatia matakwa ya kisheria, Dkt. Migiro alieleza kwamba uamuzi upatikane kwa maridhiano, kwa majadiliano na kwa kushawishiana kwa hoja wajumbe waliobaki na walio wengi wanaweza wakatumia wingi wao na wana uhalali wa kisiasa na wa kisheria. 
    Dkt. Migiro aliendelea kusema kuwa, wajumbe waliotoka hawakuona kuwa utaratibu huo ungekuwa na manufaa kwao licha ya kuwepo na maridhiano katika bunge hilo, pia kupitia wadau mbalimbali Vyama vya siasa vyote vimekuwa vinazungumza nje ya bunge kupitia Msajili wa Vyama vya siasa, kupitia Kituo cha Demokrasia (TCD) na kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.