September 15, 2014

  • Simba Chawene awataka Watanzania kuacha kuingia barabarani kufanya maandamano ya kupinga mchakato wa Katiba



    Simba Chawene awataka Watanzania kuacha kuingia barabarani kufanya maandamano ya kupinga mchakato wa Katiba
    Na Benedict Liwenga, MAELEZO-Dodoma.

    MJUMBE wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. George Simba Chawene amesikitishwa na kauli zilizotolewa na baadhi ya Wajumbe walioko nje ya bunge hilo kuhusiana na uhalali wa bunge hilo linaloendelea Kisheria.

    Kauli hiyo ameitoa leo wakati akichangia mada katika mjadala ndani ya bunge hilo huku akisisitiza kuwa huo ni upotoshwaji mkubwa na watu hao wanapaswa kuangaliwa kuhusu uzalendo wao.

    Mhe. Chawene ameeleza kuwa inasikitisha zaidi hasa pale shutuma zinapoelekezwa kwa Mwenyekiti wa bunge hilo, Mhe. Samuel Sitta, kuwa bunge hilo sasa linaonekana ni mali ya Mwenyekiti wa bunge hilo wakati si kweli.

    "Gazeti linachukua kurasa tatu hadi nne kuzungumzia habari Sitta king'ang'anizi, hivi hili bunge lipo kama liliitishwa na Sitta ama na Rais wa nchi?, hili bunge liko kisheria", alisema Mhe. Chawene.

    Aliongeza kuwa kwa niaba ya Watanzania wanafanya kazi ya bunge hilo kwa mujibu wa sheria huku akisisitiza kuwa wajumbe waliotoka nje ya bunge hilo wamevunja sheria na kwamba hawawezi kutafuta uhalali nje ya sheria.

    "Wanamlazimisha Rais avunje bunge hili, Rais wa kufuata utawala bora anavunja kwa mamlaka yapi? Mamlaka ya Rais yako kwa mujibu wa sheria", alisema Mhe. Chawene.

    Aidha, ameeleza kuwa Sheria inayoendesha mchakato wa Katiba ni Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo imetungwa kutoka katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye hatua tatu zikiwemo hatua ya kukusanya maoni ambayo Tume ya Warioba ilifanya kazi hiyo na kumaliza, hatua ya Pili ni bunge hilo kujadili kwa niaba ya wananchi wa Tanzania kwa uwakilishi uliopo ndani ya bunge hilo na hatua ya tatu ni wananchi kwenda kutunga Katiba.

    "Sisi hapa tunatoa Katiba inayopendekezwa, inayofuata ni Watanzania kwenda kutunga Katiba kwa kutunga kwa kupiga kura ya kusema ndiyo au hapana yale tuliyoyajadili na kuletwa na Tume", alisisitiza Mhe. Chawene.

    Aidha, amewataka watanzania kuwaona watu hao kuwa ni watu wabaya na wasio na nia nzuri na nchi na kuepuka kuingia barabarani kufanya maandamano ya kuipinga Katiba hiyo.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.