Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia IMTU (IMTUSO), (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, wakati akitoa taarifa kwa umma kufuatia maagizo ya Tume ya vyuo vikuu Tanzania (TCU) dhidi ya chuo cha IMTU. Kulia ni Naibu Naibu Waziri wa Mikopo na Ruzuku wa IMTU, Benson Lukwambe na Makamu wa Rais, Walter Nnko.
Na Dotto Mwaibale
WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia IMTU wameiomba Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kuunda tume maalumu itakayoshirikisha uongozi wa wanafunzi kufuatia utekelezaji wa maagizo waliyokiwekea chuo hicho ili kukamilisha kwa muda uliopangwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Rais wa Serikali ya wanafunzi wa chuo hicho,IMTU (IMTUSO), Meekson Mambo alisema wanafunzi wa chuo hicho wana wasiwasi kuhusiana na muda wa miezi mitatu uliotolewa na TCU kuhakikisha chuo cha IMTU kimekamilisha masharti yote waliyopewa vinginevyo kitafungwa.
"Matatizo ya chuo hicho ni ya muda mrefu hivyo kukiwa na kamati maalumu itasaidia kushughulikia suala hilo haraka na kulitafutia ufumbuzi badala ya kukifunga chuo hicho ambako kutaleta athari kubwa katika masomo kwa wanafunzi" alisema Mambo.
Mambo alisema TCU iunde kamati ya muda itakayoshirikiana na uongozi wa chuo uliopo sasa pamoja na uongozi wa wanafunzi waweze kusimamia na kuhakikisha kuwa maagizo ya TCU yanatekelezwa ili kutoa fursa kwa wanafunzi kuendelea na masomo huku mapungufu ya muda mrefu yaliyopo yakiendelea kutatuliwa kwani muda huo wa miezi mitatu waliopewa ni mdogo.
Aliongeza kuwa endapo uongozi wa chuo utashindwa kutekeleza maagizo ya TCU hawaungi mkono hoja ya kufunga chuo badala yake kiwekwe chini ya serikali au chuo kikuu kingine ambacho kina kitakuwa na uwezo wa kusimamia mfano Chuo Kikuu cha Dar es Salaa ambacho hakina kitivo cha afya.
Makamu wa Rais wa Serikali ya chuo hicho, WalterNnko alisema kukifunga chuo hicho kutawaathiri wanafunzi zaidi ya 1000 waliopo chuoni hapo.
0 comments:
Post a Comment