September 21, 2014

  • Mh. Silima awataka Askari wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji nchini kuwa waadilifu



    Mh. Silima awataka Askari wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji nchini kuwa waadilifu
    Na Lydia Churi, MAELEZO

    Askari wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji nchini wametakiwa kuwa waadilifu, waaminifu, watii na watekelezaji wa sheria zote za nchi kwa kuwa hizo ni miongoni mwa sifa za askari bora.

    Akifunga rasmi mafunzo ya awali ya uzimaji wa moto katika viwanja vya ndege kwa askari  100 wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji katika kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Airwing, Ukonga jijini Dar es salaam, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Pereira Ame Silima amewataka askari hao kujiepusha na vitendo vya rushwa kwani vitawapelekea kufukuzwa kazi na kukatisha ndoto za maisha yao.

    Alisema nidhamu ya kazi, Ushirikiano na kujituma katika mema ni miongoni mwa mambo matatu yatakayowasaidia askari hao kufanikiwa katika kazi zao  pamoja na maisha yao kwa ujumla.

    Naibu waziri huyo aliwahakikishia askari hao kuwa Serikali itaboresha miundombinu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ikiwa ni pamoja na kuwapatia vitendea kazi vya kisasa ikiwemo mitambo ya kisasa ya uzimaji wa moto na uokoaji na  vyuo vya mafunzo ili jeshi hilo liondokane na changamoto zilizopo kwa haraka. 

    Akizungumza awali, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Viwanja vya ndege Mhandisi Thomas Haule  aliiomba serikali kuimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kuwapatia vifaa vya mafunzo vya kisasa pamoja na mafunzo ili kuendeleza huduma bora zinazotolewa na viwanja vya ndege nchini.

    Alisema teknolojia ya kisasa na hasa magari ya zimamoto ya kisasa yanahitajika ili kupanua viwanja vya ndege nchini. Hivi sasa kuna kituo kimoja cha zimamoto katika kiwanja cha ndege cha Dar es salaam na baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Sehemu ya tatu (Terminal 3) ya uwanja huo kitahitajika kituo kingine ikiwa ni pamoja na kupanda hadhi kwa kiwanja hicho kutoka category 9 hadi ya 10.

    Wakati huo huo, Kaimu Kamishna Generali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Lt. Col Lidwino Simon Mgumba alisema lengo la mafunzo hayo kwa askari wa Zimamoto na Uokoaji ni kukabiliana na upungufu wa askari katika vituo vilivyoko kwenye viwanja vya ndege.  Aliongeza kuwa mafunzo hayo yalianza na askari 101 na kumalizika na askari 100 ambapo askari mmoja alitoroka mafunzo baada ya kushindwa kuhimili mafunzo hayo.

    Aidha kabla ya kufunga mafunzo hayo, Mgeni rasmi alishuhudia onyesho la uzimaji wa moto kwenye ndege iliyowaka likifuatiwa na gwaride ambalo  alilikagua na baadaye kulifuatiwa na kiapo cha utii kwa askari waliofuzu mafunzo hayo 

    Mafunzo hayo ya miezi miwili ya uzimaji wa moto kwenye viwanja vya ndege kwa askari wa jeshi la Zimamoto na uokoaji yamefanyika katika awamu ya pili ambapo awamu ya kwanza yalifanyika mwaka jana. 


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.