Najua utakubaliana na mimi kwamba wengi wetu hatutathmini nini tunasema vinywani mwetu, nini tunaimba, nini tunasikiliza, nini tuna soma na hata nini tunaangalia, kwasababu labda hatujui kwamba vile tunavyovisikiliza, kuvisoma au kuviangalia mara kwa mara vinachangia sana kwenye nini tunachokizungumza, na pia vile tunavyo vizungumza vinywani mwetu, ama kwa kujua au kwa kutokujua vina athari chanya au hasi katika maisha yetu ya kila siku. Unaweza ukaidharau nguvu iliyoko kwenye maneno ya kinywa chako au kutokujua umaana na umuhimu wake na hivyo ukawa msema chochote wakati wowote. Inawezekana kabisa kwamba uko vile ulivyo kwa sababu ya yale unayoyatamka kinywani mwako mara kwa mara, hapa namaanisha kwamba, siku utakayoamua kubadili unavyozungumza, hususani juu yako mwenyewe na katika mazingira yanayokuzunguka basi utaweza kubadili na hali yako kwa ujumla. Kwa kinywa tunajenga, kwa kinywa tunabomoa, kwa kinywa tuna bariki na kwa kinywa tuna laani, kwa kinywa tuna nyanyua roho na nafsi za watu na kwa kinywa hicho hicho tunaziua roho na nafsi hizo, kwa kinywa tunadumisha penzi, kwa kinywa tunaua penzi, ni uchaguzi wako kuamua unatumiaje kinywa chako. Maneno ya vinywa vyetu ni “roho” yana nguvu ya kuua na kuhuisha, unaweza kabisa kuumba utakacho kwenye maisha yako kupitia yale usemayo, na unaweza kabisa kudumaza hali ya maisha yako kupitia yale usemayo. Naomba nimnukuu kaka yangu Joel Nanauka “Maneno yako ni malighafi safi katika kutengeneza mustakabali wako” Sasa kama unataka mustakabali “future”yako iwe nzuri basi chagua maneno mazuri ya kusema kuhusu mustakabali wako. Usiseme tu kila neno kwasababu tu na wengine nao wanasema neno hilo, usiimbe tu kila wimbo kwasababu tu na wengine wanauimba, sio kila kisikilizwacho au kiangaliwacho kinakupasa na wewe kukisikliza au kukiangalia, kuwa mchambuzi yakinifu. Maandiko yanasema.... “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi, na wao waupendao watakula matunda yake” (Mithali 18:21)…..! Fahamu kwamba “You can build or destroy your own future simply by your words” – Chris Mauki
0 comments:
Post a Comment