September 17, 2014

  • Rais Wa awamu ya Pili Mh. Ali Hassan Mwinyi kuwa mgeni rasmi Mkutano wa 22 wa AQRB



    Rais Wa awamu ya Pili Mh. Ali Hassan Mwinyi kuwa mgeni rasmi Mkutano wa 22 wa AQRB
    Na Beatrice Lyimo- MAELEZO

    Rais mstaafu wa Awamu ya pili wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Ali Hassan Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa 22 wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) utakaofanyika Septemba 18 2014.

    Msajili wa Bodi ya AQRB Bwana Jehad Abdalah Jehad amesema hayo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.

    Bwana Jehad alisema kuwa lengo kuu la mkutano huo ni kuendeleza wataaluma wa fani ya wakadiriaji majenzi na kuzijua changamoto zilizopo katika sekta hiyo.

    "Jukumu kuu la bodi hii ni kusajili wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi pamoja na kuratibu mienendo yao ya kitaalamu. Mkutano huu utasaida sana kuitangaza taalum hii," alisema Jehad.

    Aidha, bodi imeandaa mashindano ya insha kwa wanafunzi wa kidato cha pili nchini yalionza tangu 2008 ili wazifahamu taaluma hizi na kuamua kusomea taaluma hiyo ya sayansi kwa kuwa wanafunzi ni wadau muhimu wanaohitaji kuelewa fani hii.

    Mwaka 2013 wanafunzi walishindanishwa kuandika insha yenye mada inayohusu "Uongozi wa shule yako una mpango wa kujenga majengo mawili ya madarasa na maabara bora kushinda yaliyopo kwa sasa, toa ushauri juu ya utaratibu unaotakiwa kutumika katika mchakato wa kupata majengo hayo ikiwa ni pamoja na wataalamu wanaotakiwa ukiainisha majukumu ya kila mmoja."

    Bwana Jehad alisema kuwa tangu walipoanzisha mashindano ya insha, wamebaini kuwa dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii kuwa wasichana hawawezi somo la sayansi ni potofu.

    Tangu mwaka 2008 mashindano hayo yalipoanzishwa,imeonekana wazi kuwa kati ya wanafunzi 109 waliopata tuzo, kati ya hao 66 ni wasichana na wavulana ni 43.

    Kwa mujibu wa Msajilii wa bodi ya usajili wa ubunifu majengo, bodi imeanzisha mafunzo kwa wanafunzi kwa kuwapatia mazoezi yanayohusu taaluma hiyo ili kuhamasisha wanafunzi kupenda somo la sayansi hususani taaluma hizi kuziba pengo la upungufu wa wataalamu nchini.

    Zaidi ya washiriki 400 kutoka katika sekta mbalimbali za wahandisi nchini watashiriki mkutano huo.
    Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu bw. Ambwene Mwakyusa (Kulia) akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa 22 wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) utakaofanyika Septemba 18 2014 ambapo Rais wa awamu ya pili wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajia kuwa mgeni rasmi kushoto ni Msajili wa Bodi ya AQRB Bwana Jehad Abdalah Jehad .
    Msajili wa Bodi ya AQRB Bwana Jehad Abdalah Jehad(kushoto) akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu maandalizi ya kuhusu mkutano wa 22 wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) utakaofanyika Septemba 18 2014, ambapo Rais wa awamu ya pili wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajia kuwa mgeni rasmi kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu bw. Ambwene Mwakyusa.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.